WASHNGTON, MAREKANI

Seneta wa Chama cha Republican nchini Marekani, Jeff Flake, amemkosoa vikali Rais Donald Trump kwa matamshi yake ya mara kwa mara yanayoonekana kuvishambulia vyombo vya habari .

Akizungumza katika Baraza la Seneti nchini humo, amesema kiongozi aliyeko madarakani anapokuwa na mazoea ya kutamka matamshi yaliyojaa chembe chembe za kibaguzi kwa watu wengine, ni lazima atakuwa na walakini.

Amemkosoa kwa kutumia baadhi ya maneno yaliyowahi kutumiwa na kiongozi wa zamani wa kiimla wa Urusi, Joseph Stalin, kuwashambulia wale aliokuwa akiwaona ni maadui zake kwa kutumia maneno ‘maadui wa watu’ alipovishambulia vyombo vya habari.

Stalin ambaye alitawala iliyokuwa Jamhuri ya Kisovieti katika kipindi cha kuanzia katikati ya miaka ya 1920 hadi mwaka 1953, wakati wa utawala wake alituhumiwa kuhusika na vifo vya mamilioni ya watu waliokuwa wapinzani wake kisiasa.

Seneta huyo wa Arizona (55), ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa Rais Trump ndani ya chama cha Republican, pia alimshambulia kiongozi huyo kutokana na matamshi yake ya kuvidharau vyombo vya habari.

Mashambulizi ya kiongozi huyo dhidi ya Rais Trump pia yamepata kuungwa mkono na viongozi kutoka mataifa ya nje ya Ufilipino, Rodrigo Duterte, Nicolas Maduro wa Venezuela na Bashar Assad wa Syria.

Seneta huyo pia alimshutumu Rais Trump kwa kujaribu kudhoofisha taasisi za serikali nchini humo, akitolea mfano tangu alipohoji juu ya cheti cha kuzaliwa cha mtangulizi wake, Barack Obama, na kuhoji taarifa za mashirika ya kijasusi nchini humo.

Majibu ya Ikulu

Msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House), Sarah Sanders, alionekana kupuuza hotuba hiyo ya Seneta Flake akisema seneta huyo hamkosoi Rais kwa vile ni mkandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari bali ni mtafuta umaarufu.

Hotuba ya Flake inakuja wakati Rais Trump akitarajiwa kutoa tuzo kwa mashirika kadhaa ya vyombo vya habari nchini Marekani alizozipachika jina tuzo kwa ajili ya habari za uwongo (Fake News Awards).

Rais Donald Trump alitoa tangazo hilo siku chache zilizopita kupitia ukurasa wake wa twitter juu ya mpango huo wa vyombo vinavyoongoza kwa rushwa na kutoa taarifa zilizoegemea upande mmoja wa wakosoaji wake.

Seneta huyo ni wa pili kujitokeza hadharani kumshambulia Rais Trump ndani ya chama cha Republican, baada ya Seneta John McCain ambaye aliandika makala katika gazeti la Washington Post iliyo na kichwa cha habari ‘Rais Trump acha kuvishambulia vyombo vya habari.’

5707 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!