Dhana kwamba muziki wa reggae umepigwa kumbo hapa Tanzania na kudorora, ikilinganishwa na aina nyingine za muziki, imepingwa na kupatiwa majibu ya kuupenyeza muziki huo kwa mashabiki wake kwa kuurudishia mashiko kama ilivyokuwa zamani.

Akizungumza na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, mwanamuziki nguli wa reggae nchini, Innocent Nganyagwa ‘Ras Inno’, amesema yuko katika harakati ya kuufufua muziki huo kuurudishia hadhi yake, kwani muda aliokaa pembeni kwenye muziki huo umetosha na sasa anarudi rasmi kwenye fani hiyo.

 

Anabainisha kwamba aliamua kuutathmini muziki wa reggae akiwa pembeni, ili kubaini matatizo yaliyousibu, na ndipo alipogundua upungufu kadhaa unaougubika muziki huo hapa nchini.


Anataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na ukosefu wa weledi katika kusimamia na kuendesha muziki huo, kwa kuwa sehemu kubwa ya wanamuziki wa sasa wameunasibisha mtindo huo na imani inayoambatana nao, kuliko kuwekeza zaidi katika juhudi za kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na usimamizi sadifu.


“Unajua kiukweli huwezi kujihusisha na muziki huu ukakwepa imani ya kirasta, maana wahafidhina wenye imani hiyo ni wengi katika mtindo huu,” anasema.

 

Ras Inno amekuwa katika imani hiyo kwa takriban miongo miwili na ushei, muda aliofanikiwa kubaini mashiko sahihi na potofu kuhusu imani hiyo na kuamua kufuata njia iliyo sahihi zaidi ndani ya imani hiyo. Baada ya kugundua upungufu uliopo, ambapo malalamiko mengi yanaelekezwa kwenye vyombo vya habari kutoupa nafasi ya kutosha mtindo huo, akaamua kuchukua hatua sadifu ili kurejea kwake kusimnufaishe peke yake bali pia wanamuziki wa reggae kwa ujumla hapa nchini.


Ameanza kusajili taasisi yake ya kusimamia muziki inayoitwa ‘Reggae Production House Inc’ na kufanya majaribio ya miradi michache kutathmini uwezo wake itakapoanza rasmi kujiendesha ili kutimiza malengo yake.

 

Awali kabla hajasajili taasisi yake, Ras Inno alibuni na kusimamia miradi kadhaa ya muziki iliyohusu kupinga mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), kumbukumbu mahsusi ya nguli mwingine wa reggae nchini, hayati Justin Kalikawe.

 

Pia kumbukumbu ya Mfalme wa Reggae barani Afrika, Lucky Dube, lakini pia kwa miaka minne sasa amekuwa mtendaji mwandamizi kwenye kamati za uratibu wa tuzo za muziki nchini.

 

Alianza kukamilisha mikakati hiyo kwa kudhibiti hodhi yake ya miliki-bunifu (copyright) ambayo ilipaswa kuanza rasmi mwishoni mwa mwaka jana, lakini alipofiwa na mkewe aliyekuwa mshirika wake mkuu alisitisha kwa muda pilikapilika za mapinduzi hayo ya reggae.

 

“Kweli ile tanzia ilinivuruga kwa kiasi kikubwa lakini namshukuru Mungu sasa akili imeanza kutulia, onesho mojawapo katika mfululizo wa maonesho yangu litakuwa mahsusi la kuzindua rasmi kitengo cha kijamii ndani ya taasisi kilichopaswa kusimamiwa na mke wangu. Kwa heshima yake, kitengo hicho nitakipa jina lake iwe kumbukumbu ya kudumu ya mchango wake mkubwa kwenye muziki wangu,” amesema.


Ras Inno ameunda bendi yake ambapo mwanzoni mwa mwezi ujao atafanya onesho la utambulisho wa taasisi yake, pamoja na vitengo husika na miradi ya muziki itakayosimamiwa.

 

Baada ya hapo atazindua rasmi albamu yake mpya ya nne, kabla ya kuanza awamu ya kwanza ya ziara ya maonesho mfululizo yasiyopungua tisa akianzia Dar es Salaam na kisha Nyanda za Juu Kusini.


Awamu ya pili ya ziara yake ni katika Kanda ya Kaskazini hadi Kanda ya Ziwa, ambako atatangaza albamu yake mpya ya ‘Kwa Nini’ sanjari na kuibua vipaji vya vijana wanaodhamiria kujikita katika miondoko hiyo yenye hisia kali.


By Jamhuri