Rasilimali za Tanzania na Umaskini wa Watanzania

Na William BHOKE

Mwanza

 

Mjadala huu ninaoenda kuuzungumza ni mtazamo na maoni yangu. Nitashukuru kama mjadala huu utagonganisha fikra na mitazamo ya Watanzania wengi.

Binafsi ninaamini falsafa ya mgongano wa kifkra kwani unazaa mawazo mapya na ambayo hayakuwapo.

Mwezi Agosti 386 akiwa katika bustani, mwanateolojia mashuhuri wa Kanisa Katoliki, Agustino, alisikia sauti ikimwambia, “twaa na usome, twaa na usome.’’

Maneno haya aliyoyasikia mwanateolojia Agustino nami nayanukuu kwa kukuomba kwa kusema, “twaa na usome, twaa na usome.’’

Askofu Fulton J. Sheen alipata kutusihi kwa namna hii, “usiogope kukosolewa kama uko sahihi, na usikatae kukosolewa kama hauko sahihi.’’

Kwa sababu ninaenda kuongelea mustakabali wa Taifa letu, itanilazimu kukosoa na kushauri, itanilazimu kusikitika na kupaza sauti kwa jamii yangu. Ninaamini katika maneno ya Mwanafalsafa George Gordon Byron [1788-1824] kwamba, “tone moja la wino wa kalamu linaweza kuwafanya mamilioni ya watu kufikiri.’’

Kama ni kujipima, tumejipima sana. Kama ni kuona, tumeona sana. Kama ni kutafakari, tumetafakari sana. Kama ni kusikia, tumesikia sana. Kama ni kuchekwa, tumechekwa sana. Kama ni kuvumilia, tumevumilia sana. Kama ni kupembua, tumepembua sana.

Kama ni ukimya, sasa imetosha. Kama ni aibu tumeipata Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wake kuwa wakweli na wenye maadili na akili tafakari na akili bainifu.

Si lazima kufuata falsafa ya watu wengine. Tunaweza kutengeneza falsafa yetu inayolenga kuwatoa Watanzania katika giza na kuwaingiza katika mwanga. Watanzania tuko kwenye wakati mgumu, kama Taifa kuna haja ya kuvisugua vichwa vyetu na kutafakari namna ya kuijenga Tanzania tunayoitaka.

Kama kuna kipindi ambacho Tanzania inahitaji malezi ya kifalsafa ni hiki. Falsafa itatusaidia kuwa na maarifa yatakayotusaidia kufanya uamuzi sahihi kwa kufahamu lipi lifanyike na kwa namna gani, na kwa wakati gani, na lipi tuliache, na kwa nini tuliache.

Falsafa itatusaidia sisi wenyewe na watoto wetu kuwa watu wa tafakari ya kina. Baada ya kufikiri kuwa umaskini tulionao ni mapenzi ya Mungu, tutafikiri umaskini kama matokeo ya kutotumia vyema fikra zetu kwa usahihi katika mipango yetu.

Binafsi uhalisia, tafiti za kisomi, historia na vigezo vya kijiografia vya Taifa letu vinaniaminisha kwamba, Tanzania haina laana ya rasilimali. Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi.

Binafsi sioni sababu zinazofanya taifa kama la Tanzania kuitwa taifa maskini. Watanzania wengi bado tunaishi katika umaskini, huku tukiwa hatuna mahitaji ya msingi ya kimaisha kama vile maji safi na huduma bora za afya.

Hii inawafanya watu wengi kufikiri na kuwaza kuwa Tanzania ni nchi maskini, jambo ambalo halina hata chembe ya ukweli ndani yake. Tanzania ni nchi ya fursa! Tuna utajiri wa maliasili, madini, mafuta, wanyamapori, na aridhi kubwa inayofaa kwa kilimo.

Rasilimali hizi zinaweza kugeuzwa kuwa utajiri wa kumkwamua Mtanzania. Kila niutazamapo Mlima Kilimanjaro ulivyo mrefu na unavyosifika duniani, ninaamini Tanzania ni nchi ya fursa.

Ni wapi kuna madini adimu ya tanzanite? Ni hakika kwamba yapatikana Tanzania. Uhalisia huu unaniaminisha kwamba Tanzania ni nchi ya fursa. Hebu angalia. Kanda ya Ziwa imejaa dhahabu, almasi, nickeli nk.

Kanda ya Magharibi imejaa shaba, mafuta na madini ya fedha. Kanda ya Kati ina madini ya uranium yanayotumika kutengeneza mabomu ya nuclear.  Kanda ya Pwani imejaa gesi na mafuta.

Kanda ya Kusini imejaa makaa ya mawe.  Pamoja na utajiri wote huu bado Watanzania ni maskini wa kupindukia.

Hakika hii ni aibu.  Kila kanda kuna utajiri mkubwa na wa aina yake.  Lakini pia kila kanda wamejaa Watanzania ambao ni maskini, ambao wamejikatia tamaa ya kuishi katika nchi yao.

Kuna jambo la kujifunza hapa. Tunaishi kwenye nchi ya maziwa na asali lakini maisha yetu hayaoneshi kama tunaishi kwenye nchi ya maziwa na asali.

Adui wa Tanzania yupo Tanzania

Taifa kama taifa tumepoteza dira ya kujitegemea kiuamuzi na kimkakati. Tumefika mahala pa kuamini kwamba maendeleo yanaletwa kwa kaulimbiu zinazobadilika kila siku.

Mwanaharakati Martin Luther King Jr alipata kusema, “Maisha yetu yanaanza kufikia mwisho siku tunaponyamazia mambo muhimu.” Pengine ukimya wa Watanzania umechangia kwa kiasi kikubwa watawala wetu kutumia rasilimali zetu ovyo.

Hii ni tahadhari na pia ni fundisho kwetu Watanzania. Aliyepata kuwa kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Paulo wa VI [1963-1978] alipata kuandika maneno yafuatayo, “ukitaka amani, ifanyie kazi haki.’’

Ukweli ni kwamba Watanzania hatuna amani kama inavyohubiriwa kwenye majukwaa ya kisiasa. Amani tuliyonayo Watanzania ni amani ya kisiasa siyo amani ya mioyoni mwetu hata watawala wetu wanalitambua hilo.

Amani itatoka wapi kama keki ya taifa ni ya wachache? Kila panapokosekana haki, hakuwezi kuwa na amani. Kila panapokosekana haki, hakuwezi kuwa na matumaini. Kila panapokosekana haki panapoteza utulivu.

Mark Twain amepata kusema, “andika lakini uwe tayari kulaumiwa.’’ Mimi niko tayari kulaumiwa lakini hisia zangu, manung’uniko yangu yaufikie ulimwengu na viongozi wanaotuongoza.

Ukweli unanisukuma kusema, “Watanzania hatuko salama’’. Hatuko salama kielimu. Hatuko salama kimiundombinu. Hatuko salama kikatiba. Hatuko salama kiafya. Hatuko salama kimaono. Tumegawanyika.

Tunahitaji kuwa na sera ya taifa, ambayo haitafungamana na ilani ya chama chochote kile cha siasa, bali ifungamane na maono ya Watanzania. Hilo linawezekana.

Nchi hii inahitaji mabadiliko kama vile mtu aliyekabwa roho anavyohitaji hewa ya oksijeni. Huyu mtu akicheleweshwa kwa muda mrefu wa kutosha atakufa. Akicheleweshwa lakini si kiasi cha kumuua, anaweza kuibuka akiwa na ubongo ulioumizwa na ni hakika hataweza kufikiri vyema kama awali.

Sisi raia wa Tanzania tunatamani tuendelee kuwa taifa linaloongozwa na utu, umoja, heshima, uzalendo na maendeleo ya wote pasipo kuwa na ubaguzi wa kukusudia au kutokukusudia.

Jaribu kubwa tulilonalo Watanzania ni kwamba baadhi ya viongozi wetu wametusaliti! Wameisaliti Katiba yetu. Wamesaliti miiko na maadili ya uongozi. Tanzania ni moja ya nchi ambazo baadhi ya viongozi wake wana utajiri mkubwa kuliko wa wananchi wanaowaongoza.

Eti mmiliki halali wa rasilimali za Watanzania ni kiongozi na mwekezaji aliyetoka nje, wananchi ambao ni wazawa wa Taifa hili ni vibarua na wala hawana sauti juu ya rasilimali za Taifa lao.

Gazeti la Mail la Julai 15, 1998 lilimnukuu Mark Dodd akisema, “Watanzania ni wanyonyaji wakubwa kupindukia wa Watanzania wenzao, kuliko mnyonyaji mwingine yeyote duniani’’.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, wafanyabiashara wakubwa katika Taifa hili ni viongozi walio na dhamana katika Taifa hili.  Miradi mikubwa inayoendeshwa hapa nchini ina ushirika na baadhi ya viongozi walio na dhamana katika Taifa hili.

Wamiliki wakubwa wa vitalu kwenye mbuga zetu za wanyama ni baadhi ya viongozi walio na dhamana katika Taifa hili.  Wamiliki wakubwa wa mashamba ni baadhi ya viongozi walio na dhamana katika Taifa hili.

Wamiliki wakubwa wa majumba ya kifahari katika Taifa hili ni baadhi ya viongozi walio na dhamana katika Taifa hili. Wenye hisa kubwa katika migodi yetu ni baadhi ya viongozi walio na dhamana katika Taifa hili.

Ninaogopa. Ninaogopa historia kutuhifadhi kwenye kumbukumbu za vitabu vya kihistoria kama taifa la watu wasiokuwa na fikra pevu na yakinifu. Ninaogopa kutafutwa na historia mbaya.

Maneno ya aliyepata kuwa waziri, Arcado Ntagazwa [1993], tusipoyatafakari kwa usahihi na kuyafanyia uchambuzi yakinifu yaweza kututokea.

Arcado Ntagazwa alipata kusema, “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani kwa sababu yaelekea hatufikiri sawasawa.”

Watanzania tunahitaji ukombozi wa fikra

Ninatamani kuiona Tanzania yenye watu wenye fikra pevu. Ninatamani kuiona Tanzania yenye watu wanaothamini tafiti za kisomi. Ninatamani kuwaona Watanzania watafiti na wabunifu.

Ninatamani kuiona Tanzania yenye watu wanaojikubali na kujitambua. Mantiki inatunong’oneza ukweli kwamba, fikra zilizotufikisha katika mazingira tuliyomo kwa sasa na hali tuliyonayo leo, fikra hizo kwa uhalisia wake hazitaweza kututoa kwenye matatizo tuliyonayo kwa sasa.

Ukweli wa niyasemayo hapo juu alipata kuusema mwanafizikia wa Kijerumani, Albert Einstein [1879-1955], kwa maneno haya, “Hatuwezi kutatua matatizo kwa kutumia namna ile ile ya kufikiri tuliyotumia katika kuyaanzisha matatizo.’’

Binadamu wengi wanaishi ni kwa sababu wanaishi. Hawaishi kwa malengo. Ni kweli kama anavyoamini Stephen Richards kwamba, “Namna yetu ya kufikiri inatengeneza matokeo mazuri au mabaya.’’

Huu ni wakati wa kuviona vitu vilivyo na siyo wakati wa kujiona tulivyo. Kila mtu sasa na ajihisi kama mvumbuzi, mtafiti na mtatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu.

Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, la hasha. Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake. Lakini yote katika yote tunahitaji kuandika upya historia mpya ya maisha yetu na Taifa letu.

Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi.

Wahenga walipata kunena, “Penye nia pana njia’’. Hannibal [183-247], mgunduzi wa silaha za kivita, anatushauri hivi, “lazima tuone njia kama haipo tuitengeneze’’.

Ni wakati sasa wa kuitengeneza njia upya. Kwa sababu huko nyuma tumekuwa tukiishi kama wanyama. Hatuwezi kubadili kilichotokea, kwani ni historia tayari. Na sasa tufungue macho yetu tuzione fursa zinazotuzunguka.

Watanzania tuachane na hulka ya kuishi maisha kwa kulalamika. Waandishi wa kitabu cha The Power of No, James Altucher na Claudia Altucher wanasema, “Kulalamika ni kukimbiza fursa. Unapoacha kulalamika unaanza kuona kila hali ya fursa. Unafungua mlango wa kupata mawazo mapya.’’

Watanzania tunahitaji utulivu wa akili ili tuweze kufanikiwa. Maisha bila malengo ni kama suruali isiyo na zipu!

mwisho