RC Katavi awaita wawekezaji Kiwanja cha Ndege Mpanda

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga amewaita
wawekezaji wa usafiri wa anga kuwekeza kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mpanda,
kutokana na kuwa na miundombinu mizuri.
Meja Jenerali mstaafu Muhuga amesema hayo kwa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), iliyofanya ziara kwenye kiwanja hicho, ambapo
ameihakikishia wapo abiria wengi wa kutosha.
Pia amesema kiwanja hicho kitaongeza pato la kila Mwananchi na taifa kwa ujumla
kwa kuwa kipo kwenye Ukanda wa Kitalii kwa kuwa na Hifadhi ya Taifa ya Katavi,
karibu na Ziwa Tanganyika na Hifadhi za Taifa za Gombe na Mahare zilizopo mkoa
wa jirani wa Kigoma.


Naye Mwenyekiti wa MAB, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amesema atahakikisha
anawasiliana na uongozi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ili kujua mipango yao
juu ya ndege zake zianze safari kwenye Kiwanja cha Mpanda.
Prof. Lema amesema endapo ndege nyingi zitatumia kiwanja hiki kitasaidia jamii za
hapa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kipato kukua na kukuza uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela
amesema Mamlaka inaweka mambo mengi kimkakati katika kuhakikisha inatekeleza
sera ya Uchumi wa Viwanda hasa katika sekta ya usafiri wa anga, ambapo ni pamoja
na kuimarisha viwanja vya ndege nchini.
“Mnafahamu kuwa serikali kupitia TAA imekuwa na utaratibu wa kuboresha viwanja vya
ndege kwa maana ya miundombinu, mwaka jana tu peke yake Mhe. Rais amezindua
miradi ya viwanja viwili vya Tabora na Bukoba, ambapo vimetengenezwa kwa viwango
vya lami na vinaweza kuhudumia ndege kubwa zaidi,” amesema Bw. Mayongela.
Bw. Mayongela amesema kwa kushirikiana na Bodi wanatembelea viwanja ambavyo
miradi imekamilika, iliyopo katika hatua mbalimbali za matengenezo na itakayoanza
baadaye, ambapo ni katika viwanja Mtwara, Songwe, Songea, Musoma, Shinyanga,
Sumbawanga na Iringa.
Amesema lengo la uimarishaji na kuboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege ni
kurahisisha wawekezaji kufika maeneo mbalimbali ya nchi kwa haraka na urahisi, hivyo
kwa wataalamu wanapotoka nje ya nchi na malighafi kusafirishwa kirahisi.
Bw. Mayongela amesema miundombinu bora ya viwanja vya ndege itasaidia ujio wa
wataalam wengi wa shughuli mbalimbali, na kupunguza muda mrefu wa kukaa kwenye
mabasi ya abiria kwa wananchi na wafanyabiashara mbalimbali.

2

Pia amesema kukamilika kwa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege kutatoa fursa za
ajira kwa wananchi wengi, na kuongeza pato la taifa, pia viwanja vinachochea ukuaji wa
sekta nyingine ikiwemo ya utalii, ambapo kwa mkoa wa Katavi watalii wengi wanaweza
kutembelea Hifadhi ya Katavi na wagonjwa wataweza kuwahi matibabu kwenye
hospitali kubwa.
Amesema wito wake wananchi watumie fursa za kuwekeza kwenye kiwanja cha ndege
cha Mpanda.
Naye Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Mpanda, Bw. Seneth Lyatuu amesema katika
taarifa yake kuwa kiwanja hiki kilianzishwa mwaka 1954 kikiwa chini ya Kampuni binafsi
ya Uchimbaji wa Madini ya Urwila na kipo umbali wa Kilometa mbili (2) Kaskazini
Mashariki mwa Mji wa Mpanda lakini baada ya Uhuru kilikabidhiwa kwa Serikali na
mwaka 2008 kurefushwa kwa njia ya kutua na kuruka ndege kwa kiwango cha lami
kutoka urefu wa mita 1500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 2000 kwa
upana wa mita 30.
Bw. Lyatuu amesema pia wa eneo la maegesho ya ndege lilikarabatiwa na sasa
linauwezo wa kuegesha ndege mbili aina ya ATR 42, au ndege ndogo aina Cesna 208
zipatazo nane (8) kwa wakati mmoja.
“Hapa Kiwanjani tunaendelea kutoa huduma bora kwa abiria, mizigo na ndege kwa
kuzingatia miongozo ya Usalama kwa kufanya ukaguzi wa mizigo, uegeshaji salama wa
ndege, kuboresha mazingira ya kiwanja,” amesema Bw. Lyatuu.
Wakati huo huo, MAB imefanya ziara kwenye viwanja vya ndege vya Songwe, Njombe
na Iringa.