Mtandao wa mauaji ya Barlow watajwa

*Jambazi atinga bungeni, afungua makabrasha mpango ulivyosukwa

 

*Awataja polisi, usalama walivyohusika, JWTZ yamwokoa asiuawe

 

*Pinda aelekeza alindwe, Nchimbi akiri kupata taarifa za kutisha

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, aliuawa na genge la uhalifu ndani ya Jeshi la Polisi, siri zilizovuja zimeifikia JAMHURI.

Kutajwa kwa Polisi kuhusika kwenye mauaji hayo kumewekwa hadharani na mmoja wa watu wanaojitambulisha kuwa ni majambazi sugu, ambaye ameamua kujisalimisha katika vyombo vya ulinzi na usalama.

 

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umemtambua mtuhumiwa huyo kwa jina la Mohamed Edward Malele, Mkazi wa Kijiji cha Igoma, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza. Anakisiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 hadi 40.

 

Pamoja na Polisi, washirika wengine kwenye genge hilo la mauaji ni maofisa Usalama wa Taifa, wanasiasa (madiwani) na wafanyabiashara maarufu katika mikoa ya Mwanza na Geita.

Kamanda Barlow aliuawa usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza, alipokuwa akimrejesha nyumbani Mwalimu anayetajwa kwa jina la Doroth Moses, aliyekuwa naye kwenye kikao cha harusi.

 

Kijana huyo kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa maelekezo kutoka ngazi za juu za uongozi wa Taifa. Malele ambaye hajui kusoma wala kuandika, alikamatwa Ijumaa ya Mei 10, mwaka huu katika lango la Bunge mjini Dodoma.

 

Namna alivyokamatwa

Malele anasema kwamba kikundi cha maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kinachojihusisha na matukio ya ujangili, kilimtaka ashiriki kwenda kumuua Kamanda Barlow.

 

Anasema, pamoja na ukweli kwamba ameshiriki matukio mengi ya mauaji, hakutaka kabisa kwenda kumuua Barlow kwa kuwa anamfahamu vema, na kwamba alishafanya kazi nyumbani kwake.

 

“Nilikataa kwenda kumuua Kamanda Barlow, roho iliniuma sana walipotaka nishiriki mauaji hayo, kwa kweli nilihuzunika sana,” anasema.

 

Uamuzi wake wa kukataa kwenda kushiriki kwenye mauaji hayo, uliwatia hofu washiriki hao wa uhalifu, hatua iliyowafanya wamkamate Malele na kumpeleka katika Gereza la Butimba jijini Mwanza, zamu hii akiwa amebambikiwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha.

 

Anasema akiwa gerezani, kikosi cha uhalifu ndani ya Polisi, kilikwenda kumuua Barlow, na kwamba siku chache baadaye, akiwa gerezani, alipata taarifa za mauaji hayo.

 

“Niliposikia Kamanda Barlow kauawa sikushangaa kwa sababu niliwajua wauaji, lakini cha kusikitisha ni pale niliposikia eti kuna Mwalimu amekamatwa akihusishwa na mauaji hayo,” anasema.

 

Malele anamtaja mmoja wa maofisa walioshiriki kumshinikiza ashiriki mauaji hayo, na ambaye anasema inawezekana alishiriki moja kwa moja kumuua Barlow kuwa ni kamanda aliyemtaja kwa jina moja la Muna.

 

Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa Malele baada ya kuwapo gerezani kwa miezi kadhaa, Mkuu wa Gereza aliamua kumwachia kwani hakuona sababu ya kuendelea kumhifadhi mtu ambaye hana chembe ya mashitaka.

 

Inaelezwa kwamba mtandao wa uhalifu uliposikia taarifa za kuachiwa kwa Malele, ulijiandaa kumuua mara baada ya kurejea uraiani. Hatua hiyo ilimfanya kijana huyo agome kwa muda kutoka gerezani akiamini kuwa angeuawa.

 

“Nilimweleza Mkuu wa Gereza mambo yote, naamini kwa maelezo yale aliwasiliana na wahusika, sina uhakika, lakini nilidhani hivyo. Kwa sababu hiyo nikaogopa kuwa nikitoka lazima nitauawa. Baadaye nikapata wazo nikitoka gerezani niende wapi,” anasema kwenye maelezo yake.

 

Maelele akimbilia katika Kikosi cha JWTZ

Baada ya kuachiwa kutoka Gereza la Butimba, Malele alikwenda moja kwa moja kujisalimisha katika Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kilichopo eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

 

Uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa alipojisalimisha, aliwaeleza wanajeshi hao ‘mkanda mzima’ wa mauaji na vitendo vya ujambazi alivyokuwa akivifanya na hatari iliyokuwa ikimkabili endapo kikosi cha uhalifu kingejua yupo uraiani.

 

Inaelezwa kwamba wanajeshi waliomsaidia walijaribu kuwasiliana na wabunge kadhaa wakiwa na matarajio ya kuwapata ili waweze kumsaidia. Hata hivyo, kuna maelezo kwamba wabunge wengi hawakupokea simu, na hata wengine walipopokea, hawakuonesha nia yoyote ya kutaka kukutana na kijana huyo ili kumsaidia.

 

Uchunguzi unaonesha kuwa Mbunge mmoja aliweza kuzungumza na kijana huyo na kumtaka afike mjini Dodoma ili aweze kusaidiwa. Kuna habari kwamba wanajeshi, kwa huruma na kwa kuzingatia uzito wa maelezo ya kijana huyo, walimsaidia nauli ya basi na Sh 10,000 kwa ajili ya chakula njiani.

 

Anaswa akiwatafuta wabunge

Malele alipofika Dodoma jioni, alipumzika na kwenda katika ukumbi wa Bunge asubuhi. Kitendo chake cha kutojua kusoma na kuandika kilimfanya awe na karatasi yenye majina na namba za simu za Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu; na Mbunge Musoma Mjini, Vincent Nyerere.

 

Maofisa Usalama wa Taifa na Polisi waliokuwa katika lango alilofika walipomuuliza anataka kumwona nani, aliwapa majina hayo na namba za simu. Walipombana zaidi kujua shida yake hasa ni nini, inasemekana Malele alianza kuwaeleza historia yake na namna alivyofika hapo bungeni.

 

Polisi waliposikia taarifa hizo, inaelezwa kwamba ziliwashitua, na wakaamua kuwasiliana na viongozi wakuu wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ambao waliamuru awekwe rumande. Polisi hao Mkoa wa Dodoma waliwasiliana na wenzao wa Mwanza, na ndipo ikatolewa amri kwamba arejeshwe Mwanza kwa maelezo kwamba “ni mtuhumiwa hatari wa ujambazi”.

 

Hata hivyo, taarifa zilimfikia mmoja wa mawaziri, na yeye akawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, na kumtaka asimrejeshe Mwanza kijana huyo.

 

Uchunguzi zaidi uliofanywa na JAMHURI unaonesha kuwa baadaye taarifa zilimfikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel  Nchimbi, na ndipo ukaandaliwa utaratibu wa kumhoji. Katika mahojiano hayo walihusishwa pia maofisa wa Usalama wa Taifa.

 

Imeelezwa kwamba kabla ya kuhojiwa, Malele alijengwa kisaikolojia kwa kumhakikishia kwamba asingedhurika wala kupigwa. Alipewa chakula na akawa huru kuzungumza.

 

Habari za uhakika zinasema kwamba Malele alitoa maelezo marefu ya namna alivyoshiriki matukio mbalimbali ya ujambazi katika miji ya Mwanza, Geita, Shinyanga na maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa.

 

Aliweka wazi kwamba yapo matukio mengi ambayo alitumika kama chambo. Miongoni mwa matukio anayoyaeleza kuwa yanamuumiza sana moyoni ni la yeye kutumiwa kumwita mama aliyekuwa Kanisani, na kisha kuondoka naye na kwenda kumuua.

 

“Kwenye mauaji hayo nilimfuata mama kanisani, alipotoka tukamteka na kwenda kumuua. Shida yetu ilikuwa viungo-tulimkata maziwa na viungo vya sehemu za siri- hivi vinatumiwa na wafanyabiashara,” amenukuliwa akisema.

 

Matukio ya ujambazi yalivyofanikishwa

Malele anasema ameshiriki matukio mengi-makubwa na madogo ya ujambazi katika maeneo ya Ukerewe, Kahama, Shinyanga, Mwanza, Geita na kwingineko.

 

Kwenye mauaji ya Barlow, anasema chanzo hasa kilikuwa kwamba Kamanda huyo aliwahi kuwadhulumu wenzake, na kwamba walipomfuata mara kadhaa awape mgawo, aliwaahidi kufanya hivyo baada ya kupata “kazi nyingine kubwa”.

 

Anasema kikosi cha uhalifu kinawashirikisha Polisi, maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa, wafanyabiashara na wanasiasa.

 

Anawataja wanasiasa wengine kuwa wapo katika Kata ya Mwamayombo, Ngudu mkoani Mwanza. Anasema wapo wanasiasa wawili marafiki ambao mwaka 2010 waligombea udiwani (jina la kata tunalihifadhi kwa sasa) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao ni majambazi sugu.

 

Ananukuliwa akisema, “Hawa ni marafiki sana, waligombea vyama tofauti kama kupoteza lengo, lakini walichotaka ni kuhakikisha mmoja wao anakuwa diwani. Kwenye uchaguzi akashinda wa CCM. Hawa ni majambazi, na ndiyo tulioshiriki nao kumuua yule mama wa Geita. Nilikuwa nasimamia miradi yao, nakusanya fedha kwenye maduka yao, waliniamini sana.”

 

Anasema kwenye ujambazi huwa wanatumia bunduki zilizokamatwa kutoka kwa majambazi wengine. “Bunduki walichukua zile zinazokamatwa kwa majambazi, risasi zilikuwa zinapatikana Polisi,” anasema.

 

Uamuzi wa kuacha ujambazi

Malele anasema mama yake ni Mchungaji, na kwamba ameamua kuachana na ujambazi baada ya kuona anapata fedha nyingi, lakini haoni faida yake.

 

“Mama yangu ni Mchungaji, ameshiriki kuniombea sana niache ujambazi nikawa sitaki, lakini sasa nimeona sina sababu ya kuendelea kwa sababu sioni faida, napata pesa lakini sijui zinakwenda wapi,” amenukuliwa akiwambia viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama mjini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda kusikojulikana.

 

Ingawa haijulikani mahali alipo, kuna habari kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameamuru kijana huyo ahifadhiwe na apewe huduma zote za malazi, chakula na ulinzi kwa ajili ya usalama wake. JAMHURI inaendelea kufuatilia ili kujua hatma yake.

 

Kauli ya Waziri Nchimbi

Kwa upande wake, Waziri Nchimbi alipoulizwa juu ya Malele, alikiri kuwa na taarifa zake, lakini hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo akisema ni nyeti.

Awali, uchunguzi wa mauaji ya Barlow ulianza kuelekea katika dhana kwamba zipo sababu zaidi za mauaji hayo.

 

Kikosi cha uchunguzi kilichoko Mwanza ambacho kilifuatilia, kilibaini kwamba Kamanda Barlow hakuuawa kwa sababu zinazohusiana na mapenzi pekee. Mapenzi inaweza kuwa njia moja ya kutaka kupotosha sababu za kweli za mauaji hayo.

 

Taarifa za kikosi cha uchunguzi zinasema kuna uwezekano kuwa mauaji hayo yametekelezwa na vikundi vya kihalifu vya ndani ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mitandao ya kihalifu nje ya Jeshi hilo.

 

By Jamhuri