Mahakimu wanadharau majaji

 

344. Tume inapandekeza kwamba:

i)      Mamlaka ya Mahakama ihakikishe kwamba juzuu za sheria zinapelekwa katika Mahakama zote, hasa za mahakimu, zikiwa zimefanyiwa marekebisho yote yaliyofanywa na Bunge.

ii)     Utaratibu wa kutoa vitabu vyenye kesi zilizoamuliwa (Law reports) urudishwe na vitabu hivyo visambaze kwenye Mahakama zote nchini.

iii)     Mamlaka ya Mahakama ichukue hatua za muda mfupi kufanya ukaguzi wa Mahakama kote nchini.

iv)     Mahakimu wapewe umuhimu katika ugawaji wa nyumba za Serikali. Aidha, mamlaka ya mahakama iruhusiwe kuwakodishia mahakimu nyumba.

v)      Majaji wa Mahakama Kuu waache tabia ya kusikiliza mashauri katika ofisi zao (chambers) badala yake watumie mahakama za wazi;

vi)     Mahakimu wapewe kipaumbele katika mikopo ya vyombo vya usafiri ili waweze kujitegemea katika usafiri wa kwenda na kutoka kazini;

vii)    Mamlaka ya Mahakama ihakikishe kwamba Mahakama zote zinapewa makaratasi ya kutosha na kuhakikisha kwamba kuna matumizi mazuri ya karatasi;

viii)   Mamlaka ya Mahakama ihakikishe kwamba mahakama zote zinapewa mashine za kupiga chapa na inapowezekana mashine za kompyuta. Wakati huo huo, idara ianzishe utaratibu ambapo mahakimu na majaji watachapa hukumu zao wenyewe badala ya kutegemea wachapa mashine. Hii itapunguza hukumu kuvuja kabla hazijasomwa.

ix)     Mamlaka ya Mahakama ichukue hatua dhidi ya mahakimu ambao watagundulika wakati wa ukaguzi kwamba huwa hawaandiki hukumu.

345. Tume imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai madalali, ambao ni maofisa wa Mahakama, hawafuati utaratibu wakati wa kukamata mali zinazoondosheka hasa mifugo. Kwanza mifugo inauzwa mara tu baada ya kukamatwa hata kama mtu anayekamatiwa mifugo ameonesha nia ya kukata rufani.

Utaratibu unataka siku 15 kwanza zipite kabla mifugo hiyo haijauzwa. Pili, watu ambao hawahusiki na kesi wanakamatiwa mifugo yao au mali ili kulipia wadaawa walio na uhusiano na mahakimu. Jambo hili ni kinyume cha sheria.

Tatu, mifugo hiyo au mali inauzwa kwa bei ndogo sana kiasi kwamba haikidhi deni na wenye deni hutafuta mali nyingine za mdaawa. Huu ni ukiukaji wa masharti ya kazi ya udalali yanayotaka haki ya mdaiwa isihujumiwe.

346. Madalali ni maofisa wa Mahakama ambao wanaisaidia Mahakama kukamata na kuhifadhi mali ambayo Mahakama imetoa amri ya kukamatwa. Madalali wanalipwa kwa mujibu wa kanuni zinazotawala kazi yao. Malipo hayo ni lazima yathibitishwe na Mahakama.

Tume ilipokea malalamiko kwamba hata kampuni zinateuliwa kama madalali. Dalali ni lazima awe mtu ambaye anawajibika yeye mwenyewe kama ofisa wa Mahakama. Aidha, kuna tuhuma kwamba wapo watu waliotoa rushwa ili wateuliwe kuwa madalali wa mahakama.

 

347. Tume inapendekeza kwamba:

(i)  Mamlaka ya Mahakama ichukue hatua za kiutawala kuweka bayana utaratibu wa kufuata kukamata mali ambayo mahakama imeagiza ikamatwe;

(i)   Mamlaka ya Mahakama ifafanue kiutawala utaratibu wa kufuata  kutekeleza hukumu zinazotoka nje ya wilaya na umuhimu wa kuwahusisha viongozi wa serikali kama vile Mkuu wa Wilaya.

(ii)    Uteuzi wa madalali usifanywe holela. Mamlaka ya mahakama ipitie tena orodha ya madalali wa mahakama na kufuatilia kazi zao. Wale watakaobainika kutokuwa waaminifu wafutwe.

(iii)   Mamlaka ya mahakama ihakikishe kwamba madalali hawakiuki Kanuni na taratibu zinazohusu ukamataji wa mali na muda ambao mali hiyo inaweza kuuzwa;

(iv)    Uteuzi wa madalali ufanywe kwa njia ya uzabuni na uchujaji wa waombaji uvihusishe vyombo vingine vya dola badala ya kuwa siri ya mahakama yenyewe.

348. Dhamana ni haki ya mtuhumiwa yeyote ambaye anaweza kuhakikisha kwamba atahudhuria kwenye kesi dhidi yake. Sheria imeainisha makosa ambayo dhamana haitolewi kirahisi. Kesi za mauaji ni moja ya makosa hayo. Tume imebaini kwamba mahakimu wengine wanashirikiana na polisi wasio waadilifu kuwanyima watuhumiwa wanaostahili dhamana na badala yake kuwaweka rumande hadi wanapotoa rushwa.

Matokeo ya yote haya ni msongamano wa mahabusu katika magereza na ongezeko kubwa la gharama ya Serikali kuwahifadhi mahabusu. Aidha, watuhumiwa katika mauaji wanapewa dhamana na Mahakama za mahakimu baada ya kutoa rushwa ingawa mahakama hizo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya mahakimu wanaovunja sheria kwa vitendo hivyo.

 

349. Tume inapendekeza kama ifuatavyo:

i)      Mamlaka ya Mahakama ichukue hatua kuhakikisha kwamba mahakama zinazingatia misingi ya utoaji dhamama na mazingira ambayo mtuhumiwa anaweza kunyimwa dhamana. Aidha, mahakama za mwanzo na wilaya zielimishwe kuhusu mipaka ya uwezo wao katika kesi au tuhuma za mauaji na makosa mengine makubwa ambayo hazina mamlaka nayo.

ii)     Uchambuzi wa haraka ufanywe na Idara ya Mahakama na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili mahabusu wanaostahili kupewa dhamana na wale ambao hawana kesi zinazowakabili waachiwe mara moja. Kuwepo na utaratibu wa kudumu kuzuia mlundikano wa mahabusu usio wa lazima.

iii)     Majaji, mawaziri, wabunge, mahakimu ambao kwa mujibu wa sheria ni walinzi wa amani (Justices of Peace) wahimizwe kutembelea magereza na kufanya ukaguzi wa kuwatambua mahabusu wasiostahili kukaa gerezani, na afya za wafungwa na mahabusi;

iv)     Uchunguzi wa makini ufanywe na Serikali ili kubaini wale wanaohusika na msongamano wa mahabusu na wafukuzwe kazi.

 

350. Mamlaka ya majaji kudhibiti nidhamu ya mawakili:

Sheria inampa Jaji mamlaka ya kumsimamisha kazi au kumfuta kwenye orodha ya mawakili, wakili yeyote. Mamlaka hayo yanatokana na marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya mawakili mwaka 1990. Utaratibu huu uko nje ya utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya mawakili.

Kama Jaji hana mamlaka ya kumsimamisha Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo anapotenda kosa au anapokuwa analalamikiwa ni vipi wawe na uwezo huo kwa mawakili ambao pia ni maofisa wa mahakama wenye utaratibu maalumu wa nidhamu?

 

Pendekezo:

Tume inapendekeza utaratibu wa nidhamu ya mawakili ushughulikiwe katika mfumo mmoja badala ya kuwapa majaji mamlaka tofauti na utaratibu huo na sheria Na. 12/1990 iliyoleta marekebisho hayo ifutwe.

351. Kanuni na taratibu zinazotumika kuendesha mashauri mahakamani zinachangia katika kuchelewesha mashauri mahakamani na kutoa mianya ya rushwa. Utaratibu mwingine haumo kwenye sheria, lakini unatumika. Kwa mfano shauri linaposajiliwa, anayedaiwa hupelekewa hati na hutakiwa kujibu hoja zilizo kwenye madai hayo ndani ya siku 21.

Baada ya hapo kesi  hutajwa tena na inaweza kuendelea kutajwa kama majibu ya mdaiwa hayajibiwi na mdai. Kuna ulegevu mkubwa katika eneo hili na utaratibu huu wa “mentions” unachelewesha uendeshaji wa kesi. Wakati mwingine kesi moja inaweza kuendelea kutajwa bila kusikilizwa kwa muda mrefu. Hali hii inawaletea usumbufu wadaawa ambao uamuzi wa mahakama katika suala lililo mbele ya mahakama ni muhimu kwao.

 

Mapendekezo:

Tume inapendekeza kwamba:

i)      Utaratibu wa kutaja mashauri (mentions) usimamiwe vizuri na mashauri yasikilizwe siku yanapopangiwa;

ii)     Mahakama ziache ulegevu wa kuachia watu wasiojibu madai yanayowakilishwa mbele ya mahakama bila sababu za msingi kutolewa:

iii)     Uchambuzi ufanywe na Msajili pale ambapo shauri linapoletwa kusajiliwa ili aone kama kuna msingi wa madai kabla shauri halijapelekwa kwa Jaji. Kama hakuna msingi akatae kulisajili shauri hilo; utaratibu huu hutumika huko Uingereza na unapunguza mlundikano wa mashauri mahakamani; wasajili wa Mahakama wawe waangalifu katika kuchambua madai kuliko ilivyo sasa.

352. Kanuni za Mahakama ya Rufani na sheria inayoongoza mashauri ya rufaa kutoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Rufani zinahitaji mwomba rufaa kuomba ruhusa ya mahakama (Leave) au kuthibitisha kwamba kuna suala la sheria linalohitaji uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kabla ya siku 14 hazijapita tangu hukumu kutolewa.

Shabaha ya ruhusa hii ni kuhakikisha kwamba Mahakama ya Rufani haipati rufaa ambazo hazina msingi. Ruhusa inaweza kuombwa kwa mdomo baada ya hukumu kusomwa au kwa  maandishi baada ya hapo. Aidha, waomba rufaa wanatakiwa kuambatanisha nakala ya hukumu na amri iliyomo kwenye hukunu hiyo.

Kutoambatanisha “decree” na hukumu kunaifanya rufaa itupiliwe mbali. ‘Decree’ ni sehemu ya uamuzi katika hukumu ambayo ndiyo msingi wa hukumu yenyewe. Anayesoma hukumu atafahamu “decree” ya mahakama ni nini.

 

Tume inapendekeza kwamba:

i)  Kanuni hii ya kutaka ruhusa itolewe na Mahakama Kuu iondolewe na hivyo hivyo kanuni ya 43 na 44 za kuendesha mashauri katika Mahakama ya Rufani ambazo zinahitaji ruhusa na Mahakama Kuu kuthibitisha kwamba kuna hoja sheria inayohitaji uamuzi wa Mahakama ya Rufaa:

ii) Kanuni inayotaka mwomba rufaa kuambatanisha hukumu na amri iliyomo kwenye hukumu hiyo iondolewe. Jaji yeyote anayesoma hukumu atafahamu uamuzi bayana wa mahakama iliyotoa hukumu hiyo.

iii)    Kanuni za Mahakama ya Rufani zirekebishwe haraka ili kuondoa kasoro ambazo zinawazuia watu kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

353.  Dhana ya “Uhuru wa Mahakama” ambayo inailinda mahakama kutoingiliwa na uongozi katika shughuli zake, au kuwatia hofu mahakimu na majaji wakati wanapokuwa wanalitolea uamuzi shauri…… [sehemu ya nakala ya ripoti tuliyonayo imekatika katika eneo hili na Mhariri analazimika kuchapisha vifungu vinavyoendelea].

…wa umma kwa mujibu ya sheria ya maadili. Viongozi hawa wanapaswa kutangaza mali zao na kuwasilisha matangazo yao kwa Kamishna wa Maadili. Chombo kinachohusika kitatumia matangazo haya kufanya uhakiki wa mali za mahakimu na majaji kwa lengo la kufahamu mapato yaliyoleta mali hizo na kuchukua hatua pale inapokuwa lazima. [Ripoti imekatika tena]

357. Hatua za kuwafukuza au kuwaachisha kazi na kuhakiki mali za mahakimu na majaji pekee hazitoshi kukomesha vitendo vya rushwa katika idara. Kama tulivyokwisha pendekeza huko nyuma, ajira ya mahakimu na majaji inatakiwa kuwa ya makini.

Kada ya mahakimu ambao ndiyo chanzo cha kupata majaji tayari inatuhumiwa sana. Kuna sababu za kufanya upekuzi wa kada hii kabla ya kuwateua kuwa majaji. Mahakimu wanaojulikana kwa uadilifu wao ndio wateuliwe kuwa majaji. Hata baada ya uteuzi huo, upekuzi (vetting) wa majaji uwe ni jambo la kudumu.

358. Utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya mahakama unapaswa uangaliwe upya. Malalamiko ya wananchi yanachukuliwa kwa mkato kama ni majungu hata kabla hayajachunguzwa. Aidha, uongozi wa mahakama hauchukui hatua kwa mahakimu waandamizi ambao wanapelekewa malalamiko na mamlaka hiyo kama tulivyoona kwenye mfano ulio kwenye vielelezo “A” –   “D”.

Hakimu anapoagizwa kufuatilia malalamiko anaweza asifanye lolote na hakuna hatua zitakazochukuliwa dhidi yake. Bodi za mahakama katika wilaya na mikoa na zenyewe hazifahamiki kwa wananchi. Vikao na maamuzi ya bodi hizi hawajui wajibu wao na hawafanyi wanayopaswa kufanya.

Hatua za kuimarisha bodi hizi zinapaswa kuchukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwateua makatibu wa bodi kama tulivyoshauri huko nyuma. Aidha, utaratibu wa kuwatumia mahakimu kuwachunguza mahakimu wanaotuhumiwa unaleta hisia za upendeleo na udanganyifu kwamba taarifa za uchunguzi zinazoandikwa zinamsaidia hakimu mtuhumiwa.

359. Tume inapendekeza mahakama iwe ni moja ya idara ambapo hatua mahsusi za kuondoa kero za wananchi zitaanza kutekelezwa. Hatua hizo ni pamoja na:

i)      Kupanga upya safu ya uongozi katika mtitiriko wa idara nzima ya mahakama ili kuimarisha mapambano dhidi ya walarushwa ndani ya idara na wakati huo huo kulinda kwa nguvu dhana ya uhuru wa mahakama. Mgawano wa madaraka wa vyombo vya dola na utawala wa sheria;

ii) Kuipatia mahakama bajeti ya kutosha ya kukagua mahakama zote na kuchukua hatua za haraka dhidi ya mahakimu na majaji watakaobainika kujihusisha katika rushwa;

iii) Kuipa uwezo idara kupata nyenzo za kufanyia kazi na kuongeza marupurupu ya mahakimu, majaji na watumishi wengine.

360. Mahakama ni mahali panapotakiwa paonekane safi. Heshima itakayoendana na matarajio ya wananchi kuhusu utakatifu wa mahakama itatokana na vitendo vya maofisa wa mahakama na jinsi wanavyochukulia utendaji wa haki.

Tume imeridhika hali hivi sasa ni mbaya sana. Wananchi wamepoteza imani kabisa katika mahakama. Hali hii ni ya hatari na Tume imetambua umuhimu wa kulishughulikia tatizo hili haraka iwezekanavyo.

361. Tume inaamini asilimia kubwa ya vitendo vya rushwa katika mahakama vinaweza kudhibitiwa na uongozi ili mradi uwepo usimamizi, uwazi na uwajibikaji. Kama uongozi wa mahakama utajipanga upya utaweza kudhibiti mmomonyoko wa maadili uliodhihirika. Tume inapendekeza safu ya uongozi wa mahakama ijipange upya na iwajibike katika kukabiliana na tatizo la rushwa.

 

VIELELEZO:

(Kuonesha mahakimu wasiotii maagizo ya Jaji)

 

“A”

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA JUDICIARY

DISTRICT REGISTRAR, HIGH COURT OF TANZANIA

P.O. BOX 1492, MWANZA

Ref. MR/DR/CN/CCNR/93/Vol.1/81 26/7/1993

Hakimu Mfawidhi, Mahakama ya Mwanzo,

Bukwaya, Musoma

 

Yah: Kukaza hukumu katika (PC) Civil Appeal No. 53/1988

Vincent Mongu …………………………. 

Appellant

Versus

Kuboja Makoba ………………………………..Respondent

 

Kichwa cha habari hapo juu chahusika.

Ndugu Kuboja Makoba katika shauri tajwa hapo juu, amekuwa akishinda toka Mahakama ya Mwanzo mpaka hapa Mahakama Kuu. Ingawa ndugu huyu alishinda katika mahakama zote hizo, lakini shamba ambalo ndilo asili ya shauri hili liko mikononi mwa Ndugu Vincent Mongu.

Kwa kuwa majalada yalishatumwa huko pamoja na nakala au hukumu unaagizwa kwamba utekelezaji wa hukumu ufanyike ili haki iweze kutendeka ipasavyo. Mara baada ya kukamilisha utekelezaji tafadhali tujulishe matokeo.

 

(Signed)

MSAJILI WA MAHAKAMA – MWANZA

Nakala: Hakimu Mkazi Mfawidhi,

Musoma.

Ndugu Kuboja Makoba,

c/o C.M. Makunja,

S.L.P. 621.

Musoma – Fuatilia utekelezaji huo.

 

“B”

 

JUDICIARY

 

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

HIGH COURT OF TANZANIA

P.O. BOX 1492

MWANZA

 

The Resident Magistrate I/C

Musoma R.M.S, Court,

Musoma

Ref. No. JC/72/Vol. 1.58 

1st August, 1994

 

RE: (PC) CIVIL APPEAL NO. 53 OF 1988

VINCENT MONGU V/S KUBOJA MAKOBA

 

In the above mentioned matter, the respondent, Kuboja Makoba, was the successful party. The appellant, Vincent Mongu unsuccessfully sought an appeal to the Court of Appeal.

The respondent has complained to me that the judgments of this court and both courts below have not been executed to date.

On receipt of this letter, please ensure that the shamba in dispute is handed to Kuboja Makoba, and let me know that this has been done.

 

B.D. CHIPETA

(Signed)

 

JUDGE IN-CHARGE

MWANZA

 

Copy to: Kuboja Makoba,

P.O. Box 621,

Musoma.

 

“C”

JUDICIARY

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

HIGH COURT OF TANZANIA

P.O. Box 1492

MWANZA

24th August, 1995

Ref. No. JC/72/Vol. 1/147

The Resident Magistrate In-Charge,

Msoma R.M.’s Court,

Musoma.

RE: (PC) CIVIL APPEAL NO. 53 OF 1988

VINCENT MONGU V/S KUBOJA MAKOBA

 

Please refer to my letter Ref. No. akv/72/Vol.1.58 of 1st August, 1994. Please let me know how you have dealt with this matter so far.

 

B. D. CHIPETA

(Signed)

JUDGE IN-CHARGE

MWANZA

 

Copy to: Kuboja Makoba,

P.O. Box 621,

Musoma.

 

“D”

 

JUDICIARY

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

THE HIGH COURT OF TANZANIA

P.O. BOX 1492

MWANZA

 

23 February, 1996

 

Ref. KC/72/Vol.1/179

 

Hakimu Mkazi Mfawidhi (M),

Mahakama ya Mkoa,

S.L.P. 63,

MUSOMA.

 

Yah: (PC) CIVIL APPEAL No. 53/88

 

Kuboja Makoba – Respondent

 

Tafadhali rejea barua yangu Na. JC/72/Vol.1/147 ya tarehe 24/8/95. Naomba unijulishe jinsi hukumu hiyo ilivyotekelezwa.

 

B. D. CHIPETA

(Signed)

 

Jaji Mfawidhi

MWANZA

 

Nakala: Mr. Kuboja Makoba,

c/o C.M. Makunja,

S.L.P. 1039,

Musoma.

Kabla ya hapo Msajili wa Mahakama Kuu alikuwa ameagiza kama inavyooneshwa kwenye kielelezo “A”.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anataja yapi kuhusu taasisi nyingine za Serikali na hatua zinazostahili kuchukuliwa? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

By Jamhuri