url-1Makandarasi ni shida

 

SEHEMU YA PILI

 

KANDARASI ZA UJENZI

408. Wizara ya Ujenzi ni miongoni mwa Wizara zinazotumia fedha nyingi za Serikali. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 1994/95 bajeti ya Wizara ya Ujenzi ilikuwa sawa na 4.32% ya bajeti ya Serikali na 20.25% ya bajeti ya maendeleo ya Wizara na Idara za Serikali. 

Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 1995/96 bajeti ya Wizara ya Ujenzi ilikuwa sawa na 7.53% ya bajeti ya Serikali na 17.44% ya bajeti ya maendeleo ya Wizara na Idara za Serikali.

409. Lakini tukizingatia kwamba miradi ya ujenzi ipo pia katika bajeti za mikoa na wizara nyingine zikiwemo za Elimu na Ulinzi ambazo zina Bodi za Zabuni zinazojitegemea, Wizara ya Afya, Mawasiliano, Madini na Nishati, Viwanda na Biashara na Maji, ambazo zina mahitaji makubwa ya ujenzi wa hospitali, reli, bandari, majengo, viwanda, mabwawa na miradi mingi ya maji mijini na vijijini, ni dhahiri kwamba sekta ya ujenzi inachukua sehemu kubwa sana ya bajeti ya taifa ya maendeleo.

Hivyo ni muhimu kwamba tunapofikiria maeneo yanayoliingizia taifa hasara kubwa kutokana na rushwa, sekta ya ujenzi lazima ipewe kipaumbele.

410. Miradi ya ujenzi huwa kwa kawaida inahusisha pande tatu za mteja yaani mwenye mradi (client), mshauri (project consultant) na mkandarasi (contractor). Washauri wa mradi ndio hutafsiri wazo lililobuniwa na mteja (ambaye kwa upande wa Serikali ni Idara au Wizara mbalimbali) na kuliweka wazo hilo katika michoro (usanifu) ambayo huwa dira ya ujenzi. 

Washauri pia hukadiria gharama za ujenzi unaohusika, kusimamia ujenzi wa makandarasi, kusimamia ujenzi na kudhibiti gharama. Makandarasi ndio wenye jukumu na wajibu wa kutafsiri michoro kwa vitendo na kutekeleza ujenzi wa kilichokusudiwa – jengo, barabara, daraja, reli, bandari, bwawa na kadhalika.

411. Wajibu wa msingi wa mteja ni kuhakikisha kuwa masilahi yake yanatekelezwa; kwamba usanifu ni tafsiri sahihi ya wazo lake na ujenzi ni tafsiri sahihi ya usanifu pamoja na kutekelezwa kazi katika wakati unaofaa na kwa gharama nafuu. Katika utekelezaji wajibu wake huo, mteja anahitajika kutumia vigezo sahihi vitakavyomwezesha kuteua mshauri anayefaa na hatimaye mkandarasi mwenye uwezo.

 

UTEUZI WA WASHAURI WA MIRADI YA UJENZI NCHINI

412. Zipo taratibu zinazotumika katika kufikia maamuzi yanayohusu uteuzi wa washauri wa miradi ya ujenzi hapa nchini. Maamuzi juu ya taratibu ipi itumike mara nyingi hutokana na masharti ya nchi au shirika kimataifa linalohusika na kutoa fedha za miradi unaotafutiwa mshauri.

413. Mashirika ya kimataifa ambayo yanahusiana na miradi ya ujenzi nchini, hususan ya barabara, ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB). Kila moja ya mashirika haya inazo taratibu zake zinazosimamia uteuzi wa washauri kwa ajili ya kusimamia miradi wanayoitolea fedha.

414. Kwa hiyo, tukiacha kanuni za jumla za Serikali zinazoelezea namna ya kumpata mzabuni anayefaa kutoa huduma fulani – iwe ni ya ushauri, ujenzi au ugavi – miradi inayofadhiliwa na mashirika ya kimataifa hufuata moja ya njia zifuatazo:

Taratibu za uajiri wa washauri kwa misingi ya maelekezo ya “General Regulations for the procurement of works, services and supplies under the integrated roads project.”

415. Uajiri wa ushauri wa miradi huzingatia umuhimu wa kuwa na mshauri. Zipo njia mbili ambazo zinatumika. Ya kwanza ni ya mazungumzo ya moja kwa moja na mhusika. Ya pili ni ya uteuzi unaotokana na ushindani. Uteuzi wa kutokana na mazungumzo huhitaji kuzingatiwa kwa uwezo uliothibitika, ujuzi na uaminifu wa anayeteuliwa. Mazingira yafuatayo ndiyo kigezo cha uteuzi wa mshauri mradi kwa njia ya mazungumzo:

(a) Iwapo kazi inayotafutiwa mshauri ni sehemu ya mradi unaoendelea;

(b) Iwapo idadi ya washauri katika fani inayohusika ni ndogo kiasi cha kuukosesha maana uteuzi  wa ushindani;

(c) Iwapo huduma hiyo ya ushauri inahitajika haraka na kwamba ikicheleweshwa itaweza kuiletea Serikali hasara.

416. Uteuzi wenye kuzingatia ushindani hufuata utaratibu wa kutayarisha orodha fupi inayotokana na uteuzi wa awali (short listing). Walioorodheshwa hukaribishwa kuzabuni. Orodha inaweza kutayarishwa kwa maelekezo ya wafadhili wa mradi unaohusika au kwa kupitia matangazo katika vyombo vya habari. Orodha isipungue washauri watatu na wasizidi sita.

Washauri hao hukaribishwa rasmi kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu jinsi watakavyoendesha na kusimamia ushauri wa miradi katika moja ya namna zifuatazo:

(a) Uwasilishi wa bahasha mbili zinazojitegemea, moja ikiwa na mapendekezo ya kiufundi na nyingine kifedha. Uchambuzi na tathmini ya utaratibu huu ni kuanza na ufunguzi wa mapendekezo ya kiufundi na kufuatiwa na makubaliano ya gharama.

(b) Uwasilishi wa mapendekezo ya kiufundi bila ya mapendekezo ya kifedha. Uchambuzi wa tathmini ya mapendekezo hayo ya kiufundi hufanywa na hivyo kuwezesha kupatikana mshindi wa zoezi hilo. Hatimaye mshindi huarifiwa apeleke mapendekezo yake ya kifedha yatakayofanyiwa majadiliano hadi makubaliano.

(b) Uwasilishi wa mapendekezo ya kiufundi na kifedha kwa pamoja ndani ya bahasha moja. Utaratibu huu ni kwa ajili ya miradi ambayo haina masuala nyeti na magumu ya kitaalamu na kiufundi. Ndani ya utaratibu huu tathmini ya kina hufanyiwa mapendekezo ya kiufundi kwanza na zinazopata asilimia 75 au zaidi katika 100 hufanyiwa tathmini ya kina ya mapendekezo ya kifedha. Majadiliano hufanywa na mzabuni mwenye gharama ya chini kuliko wenzake ili kufikiwa maafikiano.

Utaratibu wa uajiri wa washauri wa miradi inayofadhiliwa na mashirika ya kimataifa:

418. Taratibu zinazofuatwa na mashirika ya kitaifa katika uteuzi wa washauri wa miradi ni hizi zifuatazo:

(a) Miradi yenye ufadhili wa  Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB)

Mapendekezo ya kiufundi (Technical Proposals) yamepangiwa asilimia 80 na mapendekezo ya kifedha (Financial Proposals) asilimia 20. Mapendekezo haya hupokelewa yakiwa katika bahasha mbili zinazojitegemea. Kanuni za ADB zinaagiza ufunguaji wa “Technical Proposal” kwanza kabla ya “Financial”.

Zabuni zote zinazopata asilimia 72 hadi 80 katika uchambuzi wa mapendekezo ya kiufundi ndizo ambazo hati zao za mapendekezo ya kifedha hufunguliwa kwa ajili ya tathmini ya kina. Mshindi huwa yule ambaye gharama zake kutokana na tathmini ya kina ya mapendekezo ya kifedha, zitadhihirika kuwa ndogo kuliko nyingine.

 

(b) Miradi yenye ufadhili wa Benki ya Dunia

Mapendekezo ya kiufundi yana asilimia kamili 80 na mapendekezo ya kifedha asilimia kamili 20. Kanuni za Benki ya Dunia zinaelekeza kwamba zabuni zote zifunguliwe na kutathminiwa na alama zake kujumlisha mapendekezo ya kifedha na ambayo ndiyo bei ya chini kuliko zote hupewa alama zote 20.

Mapendekezo  ya kifedha ya wazabuni wengine hulinganishwa na yule wa chini kwa kugawanya gharama za mzabuni (Fn) kwa gharama za yule mzabuni wa chini (FO) na kuzidisha kwa ishirini (yaani Fn/Fo x 20). Utaratibu huu ni rahisi kutumiwa vibaya kwa kuonyesha upendeleo katika tathmini kwa vile mapendekezo yote ya kifedha huwa yanajulikana.

(c ) Miradi yenye ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU)

Kanuni za uchambuzi na tathmini ya zabuni zinaelekeza kwamba tathmini ya mapendekezo ya kiufundi yaainishwe katika makundi manne kutegemea alama wanazopata, yaani (i) nzuri sana (84-100%); (ii) nzuri (80 -84%); (iii) wastani (70-79%); na mbaya (chini ya 70%). Ndipo mapendekezo ya kifedha ya wale wa kundi la kwanza hufunguliwa na kutathiminiwa. 

Mzabuni anayeonyesha gharama za chini kuliko wote anapewa zabuni alimradi gharama hizo ziwe sawa au chini ya makadirio yaliyowekwa (within the budget). Utaratibu huu pia kama ule wa ADB ni mzuri zaidi kwa vile unazingatia pia makadirio ya gharama.

 

TARATIBU ZA UPATIKANAJI WA MAKANDARASI KWA AJILI YA MIRADI YA UJENZI

419. Washauri wa miradi (project consultants) wanaoajiriwa na Serikali wamekuwa wakitumia miongozo inayotokana na taratibu tofauti ili kuwawezesha kuwapata makandarasi kwa ajili ya miradi ya ujenzi. Taratibu hizo mbalimbali ni pamoja na za “Royal Institute of British Architects” (RIBA), “International Federation of Consulting Engineers” (FIDIC).

Taratibu za Uzabuni za Mashirika ya Umma – kila shirika likiwa na taratibu zake – “Code of Procedure for Tendering for Civil and Building Works in Tanzania” ambazo zimeandaliwa  na Baraza la Taifa la Ujenzi (National Construction Council – NCC) na kadhalika. Kwa jumla, hapa nchini hatuna mfumo mmoja wa uteuzi wa makandarasi.

420. Aidha, kwa miradi yenye ufadhili kutoka nje, miongozo hiyo inategemea mfadhili.  Kila shirika kubwa la kimataifa lina taratibu zake maalumu. Kwa mfano,  zipo taratibu za Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB). Hivyo hivyo kwa miradi ya ujenzi inayofadhiliwa na nchi moja moja, taratibu zinazotokana na nchi inayohusika mara nyingi ndizo zimekuwa zikitumika.

421. Kwa kuzingatia upungufu wa kutokuwepo kwa utaratibu wa pamoja wa kushughulikia uajiri wa makandarasi hapa nchini, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) lilikamilisha mwaka 1990 matayarisho ya hati ya taratibu za uzabuni kwa ajili ya kusimamia upatikanaji wa makandarasi wa miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.

Ili kumwezesha msomaji wa taarifa hii kupata fununu kuhusu taratibu za uzabuni, hati hiyo ya Baraza la Taifa la Ujenzi inachukuliwa hapa kuwa kigezo na inapendekezwa itumike kuelezea taratibu za uzabuni.

422. Madhumuni ya msingi ya taratibu zinazowekwa kusimamia uzabuni ni kumwezesha mwajiri kuteua makandarasi miongoni mwa waliopo na waliojitokeza katika mazingira ya ushindani ambaye ataweza kutimiza malengo yaliyokusudiwa kwa viwango sahihi vya kazi, katika muda mwafaka, kwa gharama nafuu na kwa kuzingatia misingi kwamba usawa wa uzabuni haukiukwi.

Kwa hiyo taratibu za uzabuni zinalenga katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka na kuzingatiwa kwa uharaka na unafuu wa gharama katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi. Hatua zinazopaswa kufuatwa ni hizi zifuatazo:

 

Uteuzi wa awali (Prequalification)

(a) Madhumuni:

Hatua hii ina dhamira ya kuorodhesha kampuni kadhaa ambazo yoyote miongoni mwao inaweza kupewa dhamana ya utekelezaji wa mradi. Kitendo cha uteuzi wa awali hurahisisha uchaguzi wa mwisho wa mkandarasi utakaozingatia zabuni yenye gharama ndogo iliyotathminiwa (lowest evaluated tender).

 

(b)  Matayarisho ya Mradi

Mradi hutangazwa katika magazeti ya kitaaluma na yenye kuuza nakala nyingi. Matangazo hayo yanalenga katika kuwataarifu makandarasi kutuma maombi kwa madhumuni ya kufanyiwa uteuzi wa awali. Zoezi hili hufanywa mwezi mmoja kabla ya kuitishwa tenda. Tangazo hutoa tamko lenye vipengele kadhaa vikiwemo:

(i) Aina na ukubwa wa kazi na mahali mradi ulipo. Taarifa hii ni kwa ajili ya kumwezesha mzabuni kupata hisia ya gharama ya kuutekeleza mradi;

(ii) Aina ya mkataba unaodhamiriwa;

(iii) Jina la mwajiri na la mshauri wa mradi;

(iv) Tarehe ya mwisho na mahali zabuni zitakapowasilishwa;

(v) Wafadhili wa mradi kama ni tofauti na mwajiri;

(vi) Aina ya upendeleo unaotarajiwa kuwepo kama upo;

 

(vii) Vigezo vingine vyoyote kama vile sifa za mkandarasi anayehitajika;

 

(viii) Tarehe ambayo ujenzi unatarajiwa kuanza.

 

Aidha, makandarasi wanahitajika kueleza sifa walizonazo na zinazowiana na mradi unaotangazwa. Mathalani, wanahitajika kuorodhesha miradi ambayo wameitekeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita – ikiainisha majina ya waajiri, washauri, ukubwa wa miradi, tarehe ya kuanza na kumaliza miradi hiyo na matatizo waliyopambana nayo.

Aidha, wanahitajika pia kuonyesha miradi ambayo wanaitekeleza kwa wakati uliopo pamoja na majina ya waajiri wao, ukubwa wa miradi, hatua ambayo utekelezaji umefikia, kama kuna ucheleweshaji na sababu za kuchelewa huko. Wanatakiwa pia kuonyesha umbile la kampuni, idadi na aina za watumishi, aina na idadi ya vifaa, ujazo wa biashara kwa kila mwaka kwa miaka mitatu iliyopita, hali ya ukwasi, jina la benki zao na vyeti vya kuandikishwa kama makandarasi.

(b) Uchujaji wa Makandarasi (Short Listing)

Orodha fupi ya makandarasi kutoka miongoni mwa waliojitokeza kuomba uteuzi wa awali hutayarishwa kwa kuzingatia sifa zenye uwiano na mradi pamoja na vigezo vifuatavyo:

(i) Uwezo wa kiufundi (wataalamu na vifaa) na utawala;

(ii) Ujuzi na uzoefu wa utendaji;

(iii) Uzoefu wa mazingira ya mradi;

(iv) Uwezo wa kifedha.

Makandarasi walioteuliwa na kuwemo katika orodha hii fupi hukaribishwa rasmi kutuma zabuni kwa ajili ya kufikiriwa kupewa mradi, na wale ambao hawakufanikiwa kuwepo katika orodha wanaarifiwa juu ya kutofanikiwa kwao.

Hati maalumu ya uzabuni hupelekwa kwa waliothibitishwa kuwa wazabuni. Hati hii inajumuisha:

(i) Barua rasmi ya kukaribisha zabuni;

(ii) Maelekezo ya uzabuni;

(iii) Masharti ya mkataba utakaoingiwa;

(iv) Fomu za uzabuni;

(v) Usanifu wa mradi (specifications);

(vi) Mahitaji ya vifaa na viwango vya bei (Bill of Quantities and/or schedule of rates);

(vii) Michoro;

(viii) Maelezo mahususi kuhusu mradi (Information Data);

(ix) Maelezo ya nyongeza kama yapo.

 

Muda wa kutosha hupewa wazabuni ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao kikamilifu kabla ya kuwasilisha.

 

Uteuzi wa Makandarasi

(a) Kupokelewa na kufunguliwa zabuni

 

Ni wajibu wa wazabuni kuhakikisha kwamba zabuni zao zinapokelewa ndani ya wakati uliotajwa katika hati za zabuni, zabuni zote zinazofikishwa baada ya wakati ulioainishwa huwa hazipokelewi.

Ufunguzi wa zabuni hufanywa katika hadhara inayojumuisha waombaji wote, mshauri wa mradi, mwajiri au mwakilishi wake, n.k. Wakati wa ufunguzi taarifa zifuatazo huwekewa kumbukumbu kwa kila zabuni na kuwekewa saini na Mwenyekiti na Katibu wa Bodi ya Zabuni inayohusika: 

 

(i) Jina la mzabuni;

(ii) Gharama za zabuni;

(iii) Masharti yaliyowekwa na mzabuni, (qualifications) n.k.

 

(b) Uchambuzi wa Tathmini ya kina za Zabuni (Evaluation of Tenders)

Ingawa hairuhusiwi mzabuni kubadilisha chochote ndani ya hati ya zabuni baada ya kufunguliwa, lakini wakati wa kutathmini zabuni, mshauri wa mradi anaruhusiwa kutafuta taarifa za ufafanuzi kuhusu kipengele chochote kilichomo katika zabuni. 

Taarifa itakayotolewa na mzabuni au maelezo yatakayotokana na ufafanuzi uliohitajika na mshauri wa mradi, hayapaswi kuathiri, kwa vyovyote vile lengo la ushindani baina ya makandarasi waliowasilisha zabuni. Uchambuzi wa awali unalenga katika kuhakikisha kuwa zabuni zote zimefuata masharti ya msingi yaliyoelezwa katika zabuni.

Madhumuni ya kufanya tathmini ya kina ya zabuni ni kuthibitisha gharama za mradi kwa mwajiri kwa kila zabuni na kuwezesha kuteua zabuni ambayo baada ya tathmini ya kina itadhihirika kuwa ya bei nafuu zaidi na kwamba inalingana na makusudio ya zabuni kama yalivyoainishwa katika hati za zabuni (tender documents).

Uchambuzi na tathmini ya kina ya zabuni ina vipengele vitatu vifuatavyo:

(i) Tathmini ya Kifundi

Tathmini hii inazingatia uwiano wa viwango vilivyowekwa na michoro, makosa ya majumuisho ya tarakimu, uhakiki wa bei, taratibu sahihi za ujenzi, mipangilio ya kazi, muda wa kukamilisha kazi, ufanisi wa mitambo n.k.;

(ii) Tathmini ya Masuala ya Kifedha na Gharama

Tathmini hii inahusisha mambo yafuatayo: gharama za mradi, mtiririko wa fedha na thamani ya fedha hiyo kwa wakati uliopo (discounted cash flow and net present value), mpangilio wa malipo na namna ya kuyagharamia, aina ya sarafu, mipango ya kinga na tahadhari (bonds, guarantees and insurance), malipo ya awali na kiasi kinachotakiwa kubaki na mwajiri (down payment/retention) n.k.

(iii) Tathmini ya jumla kuhusiana na mkataba na masuala ya kiutawala

Tathmini hii inahusu uhakiki wa uwiano na maelekezo yaliyomo katika zabuni, usahihi wa zabuni, uthabiti wa utawala, usafiri wa meli, taratibu za forodha na usafirishaji kwa jumla, saa za kazi mipango ya usalama, afya na masilahi ya wafanyakazi, masharti maalum, n.k.

Kama kuna masharti maalum yoyote yasiyokubalika na mwajiri, mzabuni sharti aarifiwe na kutakiwa akubali kuyaondoa kwa maandishi bila kuleta mabadiliko ya gharama zilizomo kwenye zabuni. Aidha, iwapo yapo masharti mengine, mwajiri kwa kupitia mshauri wa mradi anaweza kumwita mzabuni anayehusika kwa majadiliano. 

Masharti hayo hayana budi yajadiliwe kwa kina ili kumwezesha mshauri kulinganisha athari katika tathmini. Katika kufanyia uchambuzi masharti ya zabuni, ni muhimu kuzingatia faida na hasara za masharti hayo kabla na baada ya mradi huo kukamilika. Usichukuliwe katika tathmini ushauri wowote ambao mahitaji yake ni makubwa kuliko mahitaji yaliyoainishwa katika hati za zabuni.

Zabuni itakayoonekana kuwa yenye gharama nafuu kiuchumi (most economical) baada ya uchambuzi wa tathmini hii ya kina ndiyo ambayo itakuwa yenye manufaa zaidi kupita zote na inayopaswa kukubaliwa na mwajiri.

 

(b) Uteuzi wa Mkandarasi

Uteuzi wa mkandarasi huzingatia zabuni iliyoonekana kuwa na gharama nafuu zaidi kuliko zote kama ilivyobainika wakati wa uchambuzi wa tathmini ya kina (the lowest evaluated tender). Majadiliano yenye lengo la kufikia hatua ya kutiliana sahihi mkataba hufanywa kwa kuzingatia:

(i) Wasiwasi uliobainika wakati wa tathmini (risks assessed during evaluation);

(ii) Masharti yaliyopendekezwa kwa majadiliano;

(iii) Viwango vya malipo vinavyoonekana kukosa uwiano na gharama halisi;

(iv) Kazi ambazo ziko nje ya utaratibu wa kawaida;

(v) Viwango vya gharama za kinga na tahadhari;

(vi) Mtiririko wa matumizi iwapo unatofautiana na ule uliopangwa na mwajiri.

Mwajiri au mshauri wa mradi haruhusiwi kuweka katika hatua hii masharti mapya nje ya yale yaliyokuwemo katika hati za zabuni.

 Baada ya maafikiano kufikiwa, mwajiri anawajibika kuwekeana sahihi mkataba na mzabuni anayehusika. Aidha, endapo hawakukubaliana na mzabuni ambaye zabuni yake imetathiniwa kuwa ndiyo yenye gharama nafuu, mwajiri anaweza kukataa zabuni  hiyo na kumwomba mzabuni wa pili kwa unafuu afike kwa majadiliano.

Baada ya kufikia makubaliano na mzabuni aliyeshinda, wazabuni walioshindwa wanapaswa kuarifiwa kila mmoja juu ya matokeo ya zabuni na bei iliyofikiwa. Aidha, kwa sababu za kitaaluma kuhusu haki za unakili (copyright), wazabuni walioshindwa wanapaswa kuarifiwa pia kwamba warejeshe kwa mwajiri michoro yote ambayo haikuambatanishwa na zabuni ziliporejeshwa.

 

Taarifa kwa Baraza la Ujenzi la Taifa

423. Moja ya majukumu ya kisheria ya Baraza la Ujenzi la Taifa ni kutunga na kufuatilia utekelezaji wa miongozo na taratibu za uzabuni kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba haki inatendeka, kazi zinafanyika haraka na kwa gharama nafuu. 

Ili kuwezesha udhibiti wa jukumu hili, kila mshauri wa mradi nchini ana wajibu wa kulipelekea Baraza nakala ya taarifa ya uchambuzi na tathimni ya kina ya zabuni zote pamoja na maamuzi ya mwisho ya uteuzi wa mkandarasi.

Aidha, mwajiri anashauriwa kuwasiliana na Baraza kwa ajili ya ushauri iwapo anatofautiana na tathmini na maelekezo ya mshauri wa mradi kuhusu zabuni yenye gharama nafuu kupita zote.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anazungumziaje rushwa katika ujenzi? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

3039 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!