*Yawataka Watanzania kupuuza uvumi mitandaoni

Baada ya kuwapo joto kali la maneno ya kidiplomasia kutoka kwa maafisa wa Serikali za Tanzania na Rwanda kutokana na habari kwamba Rais wa Rwanda, Paul Kagame amemtukana Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Serikali ya Rwanda sasa imetoa msimamo rasmi kukanusha tuhuma hizo.

Balozi wa Rwanda hapa Tanzania, Dk. Ben Rugangazi, ameliambia Jamhuri katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa habari zinazosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Rais Kagame, amemtukana Rais Jakaya Kikwete si za kweli.

 

“Tanzania na Rwanda ni nchi masikini. Tuna mambo mengi tunayopaswa kuzungumza kukuza uchumi wa nchi zetu mbili. Malumbano haya yenye lengo la kuleta vurugu na uhasama mkubwa, tusiyape nafasi.

 

“Rwanda iliishaonja madhara ya vurugu mwaka 1994, hivyo hatutaki kurudi huko. Rais Kagame si mtu wa vurugu kama wabaya wake wanavyotaka ionekane,” Dk. Rugangazi aliliambia Jamhuri.

 

Katika utumishi wa umma kwenye tasnia diplomasia kauli ya Balozi wa nchi yoyote duniani, kidiplomasia huwa ndio kauli ya nchi anayoiwakilisha na kimsingi ndio msimamo rasmi wa taifa lake.

 

Amesema habari hizo zinalenga kuharibu uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Rwanda, na hasa zinasambazwa na wabaya wa Rais Kagame wakilenga kumpunguzia marafiki na hatimaye kuathiri maendeleo ya Rwanda.

 

Balozi huyo anayeiwakilisha Rwanda nchini Tanzania na Ushelisheli, ameliambia JAMHURI kwamba Rais Kagame ni mwadilifu na si mtu wa kutukana watu kama inavyoripotiwa katika mitandao hiyo.

 

Amesema Rais Kagame anaheshimu mchango wa Watanzania kwa Rwanda na pia anamheshimu Rais Kikwete, hivyo haoni sababu ya kumtukana au kumdhihaki kupitia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

 

Dk. Rugangazi amesema watu wasioutakia mema uhusiano mzuri wa Tanzania na Rwanda wamekuwa wakitafsiri vibaya hotuba za Rais Kagame.

 

Amesema kuna baadhi ya nyombo vya habari na Kundi la Waasi la FDLR vinakuza jambo hilo ili kuharibu uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Rwanda, na kwamba Rais Kagame alipokuwa akizungumza katika Chuo cha Maofisa wa Jeshi la nchi hiyo hakumtukana au kumdhihaki Rais Kikwete, bali alipinga wazo la kukutana na Kundi la Waasi la FDLR ambao amewaita kuwa ni wauaji.

 

Mbali na hotuba ya chuo cha kijeshi, inadaiwa kuwa Rais Kagame Juni 30, mwaka huu alitoa hotuba nchini kwake katika mkutano uliojulikana kama Youth Connect kwa ufadhili mke wake, Janet Kagame ambapo alisisitiza kutozungumza na waasi kwa lugha kali.

 

Kwa mujibu wa hotuba hiyo ambayo imesambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii, Rais Kagame anadaiwa kusema: “Huyu mtu mliyemsikia akiwa upande wa Interahamwe na FDLR na akashauri majadiliano….majadiliano?”

 

Rais Kagame anadaiwa kusema kuwa hatakuwa tayari kujadili jambo hilo, isipokuwa atamsubiri Rais Kikwete sehemu mwafaka: “Sitapoteza muda wangu kumjibu Kikwete, inajulikana maana kuna mahali hataweza kuvuka…haiwezekani.”

 

Mbali ya Kagame, baadhi ya viongozi kadhaa wa Serikali ya Rwanda wanadaiwa kuwa wamekuwa wakimshambulia Rais Kikwete wakimpachika majina ya kejeli kama “Rais mhurumia magaidi, wauaji wa kimbari, mkorofi na mwenye dharau.”

 

Balozi Dk. Rugangazi amesema Rais Kagame hakumtaja Rais Kikwete bali hotuba yake ililenga kuwasema wafuasi wa kikundi cha waasi cha FDLR.

 

Amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuchochea maendeleo na kukuza uhusiano mwema kati ya Rwanda na Tanzania badala ya kuharibu uhusiano.

 

Amasema Rwanda kama Taifa ni waathirika wa uhasama uliochochewa na vyombo vya habari, kwani mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, kwa asilimia kubwa yalichochewa na vyombo, hivyo ahawapendi kujihusisha na kauli za uchochezi.

 

Amesema kuwa ni kosa kubwa kuharibu uhusiano uliojengwa kwa muda mrefu wa Tanzania na Rwanda, kwani kufanya hivyo ni sawa na kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi yaliyopo.

 

Dk. Rugangazi amewaasa Watanzania kupuuza uvumi huo na kuelekeza nguvu zao katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kwani nchi hizo bado ni maskini.

 

“Nchi hizi ni maskini, sasa wananchi wake wanatakiwa kuwa na uhusiano mzuri wakae kwa amani na kuzungumza kuhusu kuondoa umaskini na kupiga hatua kiuchumi.

 

“Leo hii kama Rwanda wakiwa matajiri lazima na wananchi wa Tanzania watafaidika na utajiri huo, kwani ni nchi ambazo zinaingiliana kibiashara. Sasa kama uhusiano utakuwa ni mbovu hakutakuwa na maendeleo si kwa Rwanda wala kwa Tanzania,” amesema Dk. Rugangazi.

 

Hata hivyo, Dk. Rugangazi amesisitiza kuwa nchi yake haitakaa meza moja kufanya mazungumzo na Kundi la FDLR kwa kuwa kundi hilo la waasi halina dhamira nzuri, bali linataka kufanya mauaji mengine ya kimbari dhidi ya wananchi wa Rwanda.

 

“Tofauti iliyopo baina ya Serikali na FDLR si ya kisiasa wala si ya ugomvi wa kawaida. Ni kwamba kuna watu hawataki wenzao waishi hapa duniani na wengine wanataka kuishi na kuendeleza Taifa lao.

 

“Tatizo la sisi na FDLR nalilinganisha na tatizo la Wayahudi na Manazi wa Ujerumani. Huwezi leo ukasema Wayahudi wakae na kupatana na Manazi maana hawana matatizo ya kuyajadili wakayamaliza.

 

“Wanazi wanataka Wayahudi wafutike kwenye uso wa dunia. Hiyo ndiyo sera waliyokuzwa nayo. FDLR ni wauaji na huo ndiyo mtazamo wetu,” amesema.

 

Amesema kwamba wapiganaji wa FDLR ambao wako tayari kukiri makosa yao na kutubu, watasamehewa na kujenga Rwanda.

 

Hadi sasa, tayari waasi zaidi ya waasi 51,000 wamerejea Rwanda wakitokea katika kundi la FDLR katika kipindi cha kati ya mwaka 1996 hadi sasa, na kwamba baadhi yao wameingizwa katika Jeshi la Rwanda, amesema.

 

Amesema ushahidi wa hilo ni kuwa hata Mkuu wa Magereza wa sasa nchini Rwanda alikuwa askari wa zamani wa FDLR.

 

“Wale ambao hatuwezi kuzungumza nao ni ambao wana mashtaka ya kujibu kutokana na makosa waliyoyafanya kwenye mauaji ya mwaka 1994. Wale ambao bado wanataka kufanya mauaji ya kimbari na hawataki kukiri makosa yao hatuwezi kuzungumza nao.

 

“Kuna watu ambao hadi Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kwamba wanatafutwa na kama unavyofahamu, Serikali ya Marekani imetoa hadi zawadi kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwao.

 

“Kama wanadhani wanaonewa, wajitokeze na waende kujibu mashtaka yao kwenye Mahakama ya Kimataifa kama wenzao waliopelekwa ICTR ya Arusha.

 

“Kama wakishtakiwa huko na wakakutwa hawana hatia na wakaonesha kuwa hawana nia wala mwelekeo wa kutaka kuangamiza Wanyarwanda, hapo tunaweza kuwa na mawazo mengine,” amesema.

1451 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!