Salaam za Kagasheki kwa majangili

*Angependa wakikutwa maporini ‘wamalizwe’ huko huko

*Maelfu ya wananchi wakubali adhabu ya kifo kwa wahusika

*Muswada kuipa makali sheria kuwasilishwa Bunge lijalo

Muda ni saa 2 na dakika kadhaa asubuhi. Mbele ya Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuna mamia ya watu wa rika, rangi na jinsi zote. Wana mabango yenye ujumbe maalumu.

Kuna gari aina ya Mercedes Benz linalokokota tela lililobeba sanamu kubwa ya mnyama aina ya ndovu (tembo).

Ubavuni mwa gari hili kuna ujumbe huu wa maandishi, “Sema! Pigia Kelele! Simamisha! Maliza ujangili sasa! Tembo mmoja huuawa kila baada ya dakika 15. Tembo 30 huuawa kila siku Tanzania. Hifadhi tembo wetu. Hifadhi misitu yetu. Hifadhi uchumi wetu. Hakuna tembo hakuna chakula, hakuna kazi. Tuokoe tembo wetu, na tuwe na nyakati njema zijazo tupate kuishi”.

 

Wanafunzi wa shule mbalimbali za awali, msingi na sekondari wamekusanyika hapa. Punde, anawasili Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.

 

Naam, shughuli iliyokutanisha hadhira yote hii ni maandamano yenye lengo la kuadhimisha Siku ya Wanyama Duniani. Ingawa lengo ni maandhimisho ya Siku ya Wanyama, mnyama anayelengwa zaidi hapa ni ndovu.

 

Maandamano yanaanza kuelekea katika viwanja vya AICC, eneo la Kijenge. Umbali kutoka hapa hadi sehemu ya kuhitimishia shughuli hii ni takribani kilometa tano.

Mbele kuna pikipiki ya polisi ikifuatwa na gari lenye matangazo ya kuhamasisha umuhimu wa kuwatunza ndovu kwa kigezo kwamba hakuna utalii bila mnyama huyo mkubwa duniani, anayeishi nchi kavu.

 

Maneno yanayorejewa kwenye matangazo haya ni, “Majangili wanajulikana, wadhibitiwe”; Okoa tembo wetu, okoa ajira, okoa kizazi kijacho, kila baada ya dakika 15 tembo mmoja anauawa, mimi na wewe tufanye sasa tuokoe tembo, tuokoe ajira zetu, tuokoe kizazi kijacho. Nini kifanyike sasa? Acha kabisa kuua tembo, acha kabisa biashara ya pembe za tembo, jamii tuungane, tutokomeze biashara ya tembo.”

 

Njiani waandamanaji wanaimba nyimbo mbalimbali za kulaani ujangili na majangili. Kwa nyakati tofauti wanaingiza vibwagizo vya: “Kagasheki tupe jibu”. ‘Majangili wanajulikana”. Tembo wetu wanauawa, majangili nao wauawe”.

Naam, muda ni saa 4:10. Maandamano yanaingia katika Viwanja vya AICC. Msimamizi wa shughuli hii anawaomba washiriki wote wasimame kwa dakika moja kukumbuka matukio makuu matatu. Mosi, ni tukio la watu waliouawa kwenye tukio la ugaidi jijini Nairobi; pili, ni tukio la watu wote ambao wameuawa na tembo; na tatu ni kuwakumbuka tembo wote wanaouawa na majangili!

 

Mtu wa kwanza kuzungumza hapa ni Mtafiti wa Ndovu, Dk. Alfred Kikoti. “Harakati hizi zilianza tangu mwaka 2007 kipindi ambacho mauaji ya tembo yalianza kushamiri. Tanzania ndiyo nchi pekee katika Afrika Mashariki yenye tembo wengi wa kuridhisha licha ya matatizo makubwa ya ujangili yaliyopo sasa.

 

“Ujangili si Tanzania pekee, ni tatizo la Afrika, Asia na dunia nzima, zamani tembo walikuwa dunia nzima lakini sasa wamebaki katika mabara mawili tu — Afrika na Asia. Tanzania tembo waliosalia ni 70,000 na Afrika kwa ujumla wake tembo waliosalia ni 450,000. Kwa kila dakika 15 kuna tembo anauawa. Hapa tulipo huko majangili yananyemelea kuua tembo.

 

“Tukitaka, tunaweza kabisa kuwafanya waendelee kuwapo. Kwa Tanzania au Afrika kukosa tembo itakuwa laana. Tukipoteza tembo itakuwa laana. Arusha inategemea utalii, tembo wakiondoka hakuna utalii. Tembo wakimalizika, atakayefuata kumalizika ni binadamu. Tutapata laana tembo wakitoweka, kizazi kijacho kitakwenda kwenye makaburi yetu bila nguo,” anasema Dk. Kikoti.

 

Anaeleza furaha yake kwa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na majangili.

“Sasa tunataka vumbi litimke, majangili wakubwa na wanaowafadhili lazima washughulikiwe. Hatutaki kuona Serikali ikilalamika. Kama nyumba inavuja dawa ni kuziba na siyo kulalamika. Serikali ioneshe ujasiri. Hatutaki urafiki na nchi inayoondoa wanyama wetu. Tuwe wakali tulinde ajira za watoto waliotembea leo.

 

“Matembezi yasiwe tukio, bali mwanzo wa kulinda tembo. Hii si kazi ya Kagasheki (Waziri wa Maliasili na Utalii), wala si kazi ya Serikali pekee; ni kazi yetu sote. Tunawajua wanaoua, tunawajua wanaouza pembe, wafanyakazi wa Maliasili ni wafanyakazi wa mali yetu, Watanzania tuseme ‘hapana’ kwa vitendo,” anasema.

 

Anaongeza kuwa Tanzania bado inaweza kuongeza idadi ya tembo kutokana na kuwa na mapori mengi na makubwa.

 

“Selous pekee inaweza kuwa na tembo laki moja. Tanzania ni ya kwanza kwa kuwa na mapori yenye ikolojia nzuri, ndiyo ya kwanza kwa kujituma, ndiyo ya kwanza yenye Sera ya Maliasili katika Afrika. Sera hiyo ndiyo iliyofanya kikajengwa Chuo cha Mweka hapa Tanzania. Mwalimu Nyerere alipoteza nguvu sana kuelezea umuhimu wa wanyamapori, tumuenzi kwa kuwalinda. Tuwalinde tembo kwa sababu tembo katika pori ni kama mwenye nyumba. Bila tembo hakuna utalii.”

 

 

TATO watoa mwito

Chama cha Waendesha Utalii Tanzania (TATO), kikiwakilishwa na Mwenyekiti wake, Willy Chambulo, kikaiomba Serikali ifanye yafuatayo: Mosi, ianzishe Operesheni Uhai Awamu ya Pili. Pili, biashara ya tembo na pembe za tembo izuiwe. Kwa upande wa kuua tembo, anapendekeza utalii wa uwindaji kwa wanyama hao uzuiwe japo kwa miaka miwili ili idadi yao iongezeke.

 

Tatu, TATO inaishauri Serikali ya Tanzania kupitia CITES, iibane China ili ipige marufuku biashara ya pembe za ndovu.

 

Kagasheki atangaza uamuzi mzito

Wakati wote wa maandamano, kibwagizo kilichotawala kutoka kwa waandamanaji kilisema, “Kagasheki Tupe Jibu”. Naam, sasa ukawa ndiyo wakati wa waziri huyo kuwaeleza Watanzania nini kinachofanywa na Serikali katika kukomesha mauaji ya tembo na ujangili kwa jumla. Kwa namna ya pekee, na akitambua kuwa kwa kauli hiyo atashambuliwa na wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, Balozi Kagasheki anaamua kutoa msimamo uliojikita kwenye nukuu inayotokana na Ilani iliyotolewa na Mwalimu Nyerere mnamo Septemba, 1961. Ilani hiyo ndiyo mwongozo unaotumiwa na Afrika nzima kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.

 

Ilani hiyo ya Arusha inasema,“Kudumu kwa maisha ya wanyama wa porini ni jambo linalohusu sana sisi wote katika Bara la Afrika. Viumbe hawa si maajabu na fahari ya nchi yetu tu, bali pia ni sehemu mojawapo ya uchumi wetu wa asili na starehe ya maisha yetu ya kesho.

“Kuchukua dhamana na ulinzi wa wanyama wa porini twathihitisha kwamba tutafanya kila tuwezavyo katika mamlaka yetu kuhakikisha kwamba watoto wetu wa keshokutwa wanaweza kufaidi utajiri na uhondo wa urithi huu.

“Utunzaji wa wanyamapori na misitu yake unahitaji ujuzi maalumu, watu waliofundishwa kadhalika na fedha, na kwa hivyo twataraji mataifa ya kigeni yatashirikiana nasi katika kazi hii muhimu ambayo kutokufaulu kwake, licha ya kuwa ni madhara katika Bara zima la Afrika, yatakuwa ni madhara katika ulimwengu wote.”

 

Julius K. Nyerere

7.9.1961

 

Balozi Kagasheki anasema, “Ndugu zangu, yanayofanyika katika mapori ni masikitiko, ni misiba…Haya maneno ya Mwalimu ni mazito. Tanzania ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya ndovu katika Afrika, hii ina maana ni ya pili katika dunia.

 

“Kinachojitokeza sasa kuna watu wenye tamaa zilizokithiri, wana mioyo ya kutojali kwamba kuna Serikali na sheria.

“Operesheni Uhai nilisema bungeni, lakini wapo waliosema ni ngonjera za Kagasheki. Waulize sasa, kazi imekwishaanza, mlio karibu nao mnajua, sitaki kwenda ndani zaidi.

 

“Operesheni ya safari hii itakuwa simulizi maana kuna watu hawajali. Wameleta sifa mbaya kwa Taifa. Nje jina limechafuka. Sasa basi, imetosha.

“Mheshimiwa Rais wiki iliyopita alikuwa Marekani, nilipata bahati ya kuwa naye, alitamka operesheni imeanza kwa njia tofauti tofauti. Haya ni manyunyu tu, yenyewe inakuja. Muziki wake mtausikia, ndilo hilo naweza kulisema…enough is enough.

 

“Tukiwa Marekani, Rais alishiriki vikao viwili vikubwa New York. Kimoja kilisimamiwa na Taasisi ya Bill Clinton. Viongozi mbalimbali walihudhuria, walizungumzia ujangili na nini kifanyike. Cha pili kiliitishwa na Rais wa Gabon kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani. Kilitoa maazimio na kuuonesha ulimwengu mzima tatizo la ujangili.

 

“Kilitoa mapendekezo; moja ni kumwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ateue msimamizi maalum wa masuala ya ujangili, na pili kuwe na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kuzungumzia ujangili duniani. Rais wetu akielezea ukubwa wa tatizo tulilonalo, aliahidi kuwa hadi atakapoondoka (madarakani) atakuwa amemaliza tatizo la ujangili,” anasema Kagasheki.

 

Waziri huyo akaongeza; “Wapelekewe salamu wasikie (majangili), tayari jeshi limo ndani, tumefika mahali tumesema tumechoka. Tuna majangili wengi, sheria zetu nazo ni dhaifu. Huwezi kamata mtu ana nyara ukamtoza faini ya mchezo. Sheria sasa inabadilishwa ili wapate adhabu nzito…Bunge lijalo sheria (muswada) inapelekwa.

 

“Kuhusu adhabu, ukiniuliza mimi sijali, nasema (askari) wakikutana na majangili wawamalize huko huko. Najua wapo watakaosema haki za binadamu, wanasheria wanaosema haki za binadamu wafunge midomo. Jangili akikupata atakumaliza wewe na tembo atammaliza. Hazi za kwanza ziwe kwa viumbe ambao hawawezi kujitetea… kwenda haraka kwa kesi hizi ni kuwamaliza huko huko, hapo utakuwa umemaliza kesi.”

Waziri Kagasheki anasema asilimia 30 ya ardhi yote ya Tanzania ni ya uhifadhi. “Tunataka uhifadhi endelevu, ukiutazama uwe na impact katika utalii.”

 

Siasa inavuruga uhifadhi

Kuhusu siasa kuingizwa kwenye uhifadhi, waziri huyo anasema, “Uhifadhi tunachanganya na siasa. Tukiendelea na utaratibu huu tutaua uhifadhi. Urais, ubunge tafuta lakini si kumaliza rasilimali zetu. Hatukubali…Hatuwezi kukubali jambo ambalo Mwalimu kalisimamia kihistoria, Mzee Mwinyi kaja hadi na Operesheni Uhai, Mzee Mkapa kalinda rasilimali hii; halafu wanyama wamalizwe katika awamu hii?

 

“Mheshimiwa Rais Kikwete anasema hawezi akawa Rais ambaye atahukumiwa na historia kwamba uhifadhi umefia mikononi mwake. Akishasema hivyo, sisi wasaidizi wake maana yake tufanye nini? Maana yake ni kazi tu. Waliotangulia wote walisimamia uhifadhi, uhifadhi tumeukuta, wangetia vurugu tusingeukuta. Tuhakikishe wanaokuja wanaupata. Haya ni mapambano makubwa na endelevu.

 

“Majangili tuwafichue, tuendelee kuwafichua. Hili la leo (maandamano) lisiwe la leo tu, liwe endelevu. Mwaka 2014 liwe kubwa zaidi. Leo miji mingine 15 mikubwa duniani wanaadhimisha siku hii ya wanyama. Namshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kusimamia vema suala hili.

 

“Ujumbe wangu ni ule alioutoa Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Rais Kikwete. Hatutasimama, shabaha ni kuhakikisha ndovu idadi yao inapanda. Sasa wanasema kuna ndovu 70,000 nchini, wengine wanasema waliosalia ni 30,000. Ipo haja ya kupata idadi halisi. Vyombo vya habari vitusaidie kwenye mapambano haya. Kwa sasa meno (pembe) yanakamatwa, lengo si kukamata, bali kuzuia tembo kuuawa. Nawahakikishia wananchi lengo hilo tutalipata.

 

“Kuna haja ya kubadili sheria. Hilo tunalifanya. Pili, ndani ya Serikali tunatazama — kuna ushirika majangili wanaupata kutoka ndani ya Serikali. Naomba sote tusimamie hili ili shabaha ya Mheshimiwa Rais Kikwete ya kutokomeza ujangili atakapokuwa anaondoka…suala la ujangili liwe limekwisha.”

 

Maandamano hayo yaliyofadhiliwa na asasi na watu mbalimbali, yalihitimishwa kwa kutoa vyeti kwa baadhi ya washiriki, hasa wanafunzi waliochora mabango yenye ujumbe mbalimbali.