Salaam za Maige kwa ‘waliomfitini’

*Aahidi kuendeleza mapambano bungeni

 

Hivi karibuni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alirejea jimboni na kupokewa na wapigakura wake na kisha akawaeleza kilichomfanya ang’olewe kwenye nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Ifuatayo ni hotuba yake kwa wapigakura.

 

Ndugu zangu na rafiki zangu, kwanza niwape pole kwa mshituko mlioupata kwa haya yaliyojitokeza. Naomba msisikitike sana . Kila jambo alilopanga Mola hutokea kadri ya mapenzi yake. (Safari) “Route” ya maisha ya mwanadamu hupangwa na Mola mara tu anapompulizia pumzi ya uhai. Hili lilipangwa hata kabla sijatokea duniani miaka 42 iliyopita.

 

 

 

Mungu hakushindwa kumwokoa mwanawe Yesu asisulubiwe, tena kwa kuonewa! Hasha, tungeupataje ukombozi bila hilo kutokea? Wakati mwingine Mungu hutoa nafasi kwa mambo magumu kuwafika waja wake, si kwamba hawapendi, bali ili unabii utimie. Ilifika wakati hata Yesu akaona kama Mungu kamuacha! Hasa sisi kwa hili tunaweza kudhani Mungu katuacha! Hasha, ni njia ya kuufikia ukombozi wa kweli.

 

Pili, kwa kifupi sana , niwafahamishe kuwa yaliyotokea ni ushahidi kwamba (wizara) Maliasili ni ngumu. Kukabiliala na wabaya ni kazi ngumu. Wapo waliojipanga, ukiwavamia ovyo ovyo unaondoka wewe. Ndivyo ilivyotokea.

 

Niwahakikishie, wazalendo wamepoteza mpambanaji. Nimepambana na wahalifu angani, majini, porini, mijini na vijijini, ndani na nje ya nchi. Nilitumia kila aina ya uwezo wangu kulizawadia taifa langu utumishi uliotukuka. Sikubakisha chembe ya (nguvu) “energy”.

 

Waziri gani aliyesimamia sheria na kuwapa vitalu Watanzania masikini wenye sifa na kuwaacha wazungu kama sheria ilivyoelekeza?

 

Waziri gani aliyewafikisha mahakamani watorosha twiga akina Kamrani na wenzake? Watu wametumia rekodi za matukio ya mwaka 2009/2010 kuficha matendo na uamuzi wa kishujaa wa Maige ya 2011. Yawezekana hawakutaka nipate sifa, lakini ipo siku nitaipata. Tena si siku nyingi. Niliwaomba wenzangu wamwogope Mungu. Bado nasisisitza hivyo, si Mungu wangu kama ilivyodhaniwa, bali Mungu wetu wa haki.

 

Waziri gani aliyefunga biashara ya wanyamahai?

Waziri gani aliyeonyesha mfano wa kuchukua hatua kwa watumishi pale alipoona hawatendi sawa? Maige hakusita kuchukua hatua.

 

Uamuzi huu ni magumu na umegusa watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa. Nilitegemea vita hii, na ninaamini tutashinda. Nilisema bungeni, Watanzania wapenda haki wanisikilize kwa makini. Muda haukuruhusu, ila nitarudi bungeni na nitasema.

 

Imesemwa (suala) “issue” ya nyumba. Nimefafanua na kutoa vielelezo. Kila mbunge aliyetaka amekopeshwa Sh milioni 290, wengine wameanzisha biashara na wengine wamenununua magari na wengine majumba. Wapo walioficha, na tupo tuliojiweka wazi! Mkopo wangu huo umekuwa (mchango wangu) “my contribution” na “balance” kulipwa na benki na nyumba kui-mortgage (kuiweka dhamana). Nimetoa nyaraka zote kwa wanahabari na vyombo vyote husika.

 

Nimesema mwenye shaka aende kwa Msajili wa Hati Wizara ya Ardhi, au kwa Kamishna wa Maadili, au CRDB Azikiwe na Dodoma nilikokopa au amtafute muuzaji. Kote huko utapata rekodi ya bei na mode of payment. Wapo wahuni, kwa masilahi ya kisiasa na chuki binafsi wametangaza bei tofauti na niliyonunulia. Mwanasheria wangu anashughulikia hilo .

 

Niwahakikishie, vita nimepigana, imani na dhamana nimeilinda. Muda wa kutuzwa na mwenye kumbukumbu sahihi, Mungu utafika. Naamini nimejiwekea akiba isiyooza mbiguni.

 

Yapo mengi yasiyo sahihi yaliyosemwa. Nitakuwa nafafanua kila nipatapo fursa na muda utazidi kutufunua. Kwa kifupi, kwa suala la vitalu, hakuna kampuni hata moja iliyopewa kitalu cha uwindaji bila kuomba, kukaguliwa na Kamati ya Ushauri na hatimaye kupewa alama.

Kampuni zisizokuwa na sifa ni zile zilizopata chini ya alama 50. Na kwa kampuni zilizokuwa kwenye biashara, “pass mark” ni alama 40 kwa mujibu wa kanuni ya 16(5) ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2010. Hakuna kampuni iliyopata chini ya alama 50 iliyopata kitalu. Hakuna kampuni ya kizalendo iliyopendekezwa na Kamati ya Ushauri ambayo haikupewa kitalu.

 

Kwa upande wa ripoti ya CAG, haikunigusa binafsi kwani ilikuwa inaishia Juni 2010 wakati mimi nilishika dhamana Novemba 2010.

 

Ka upande wa biashara ya wanyamahai, hakuna wanyama waliosafirishwa kinyume cha sheria wakati wangu (2011), na matukio ya utoroshaji tulipoyabaini, tulifungua mashitaka kwa watuhumiwa na kufunga biashara hiyo.

 

Naanza kazi ya kuwawakilisha wananchi wa Msalala. Nitawawakilisha kwa mujibu wa Katiba na ahadi zangu kwao hadi 2015 watakapopata fursa ya kuamua vinginevyo. Mara nyingi watenda mema hufanyiwa hiyana. Kama Wakristo, naomba msome Mwanzo 4:1-15.

 

Mwisho.

 

Mwanzo 4: 1-15 Inasomeka hivi:

 

“Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonoza za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, kwa nini una gadhabu? Na kwanini uso wako umekunjamana? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye (Twende uwandani). Ikawa walipokuwa uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua. BWANA akamwambia Kaini, yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapolima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia BWANA, adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. BWANA akamwambia, kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.”