Wakati mawaziri walipobinywa kujiuzulu sikushangaa nilipomsikia mmoja wao, aking’aka mbele ya waandishi wa habari. Waziri huyo wa zamani alisema: “Nijiuzulu ili iwaje? Mimi siwezi kujiuzulu…” Pamoja na kujitetea kote na kurusha lawama kwa wasaidizi wake lakini panga la Rais halikumhurumia.

Vyombo vya habari na wananchi wengine walitafsiri kung’aka huko kwa waziri kama uchu wa madaraka. Kiukweli hali iliyompata waziri huyo (na wengine ambao walipigwa panga) sio dalili ya kung’ang’ania wala uchu wa madaraka. Kuna jambo tunatakiwa tuwasiliane na wataalamu watusaidie.

 

 

Mtaalamu maarufu wa masuala ya saikolojia H. Maslow amepata kuchambua hulka na mpangilio wa mahitaji ya mwanadamu yanavyoathiri saikolojia yake. Maslow alipangilia mahitaji ya binadamu katika ngazi mbalimbali. Ngazi ya kwanza ni mahitaji ya msingi (chakula, malazi mavazi) huku ngazi zingine zinazofuata zikiwa ni kiu ya upendo, usalama, kujitambua na kujipambanua (self actualization).

Binadamu akishashiba akawa na mahali pa kuishi kisaikolojia anaelekeza akili yake katika kupenda. Mtu anapozidi kufanikiwa ndipo hofu ya usalama wake inaongezeka na baada ya hapo ataanza kujitambua (self esteem). Kutoka hapo atataka kujipambanua ili aoneshe kipaji chake, umaarufu wake, uwezo wake na vivyo hivyo atataka kuheshimiwa zaidi, kutambulika zaidi na atataka kuona jamii inayomzunguka ikimkumbuka kila mara.

Tunaambiwa kuwa kisaikolojia upandaji wa ngazi hizi ni wa moja kwa moja (irreversible). Yaani mtu akitoka kujitambua na kwenda kujipambanua akili yake hairudi nyuma, inaendelea kuamini na kuishi katika ngazi mpya. Lakini kikawaida (physically) binadamu hupanda na kushuka katika ngazi hizi.

Mtu anaweza kuwa na chakula cha kutosha, nyumba nzuri ya kuishi lakini inatokea anapoteza kila kitu na kujikuta hana chakula, hana pa kuishi na amekuwa omba omba. Mtu leo anaweza kuwa maarufu sana lakini baada ya muda anaporomoka umaarufu wake na anapotea kabisa. Kushuka kwa ngazi hizi za mahitaji ya kibinadamu kunaweza kusababishwa na mtu mwenyewe, mazingira ama watu wengine.

Kitaalamu maisha ya binadamu yanaongozwa na ufahamu (saikolojia), ndio maana kila kitu kinachofanywa na binadamu huanzia katika fikra zake. Kwa maana hii utabaini kuwa binadamu anaposhuka ngazi katika hali ya kawaida huwa kunatokea hali ya kuchanganyikiwa ama kuweweseka kwa sababu ufahamu (saikolojia) inakuwa kwenye ngazi ya juu wakati mwili (hali halisi) imeshuka kwenye ngazi ya chini.

Ndio maana utasikia mtu fulani amejinyonga kutokana na kufilisika, utasikia mtu amekimbia mji kutokana na madeni kumzidi ama mtu anaamua kujinyonga kwa kuachwa na mpenzi. Yote hii ni kwa sababu ya kuchanganyikiwa kunakotokana na tafsiri zinazipishana kati ya ufahamu na hali halisi.

Kutokana na hayo, hebu tumwangalie mbunge ambaye anateuliwa kuwa waziri. Mara tu anapoapishwa anapewa gari la thamani lenye namba maalumu, anapewa nyumba ya hadhi ya uwaziri, anakabidhiwa kusimamia maelfu ya wafanyakazi wanaomtii na kumnyenyekea na kila anakopita anapewa ukaribisho wa aina yake. Baadhi ya wataalamu wa saikolojia wanasema, mtu anapofika katika hatua kama hii huwa ametwaa “uungu” hivyo akili yake inazoea kuabudiwa.

Mara waziri huyu anajikuta anatakiwa kujiuzulu ama kuwajibishwa. “Uungu” unaondolewa na anajikuta akishuka ngazi kutoka kujimbanua kwenda chini zaidi. Akili lazima ikatae! Mara nyingi binadamu huwa tunaogopa tafsiri za ufahamu wetu kuliko hata hali halisi ilivyo katika mazingira yanayotuzunguka.

Angalia mfano huu; mtu ambaye alizoea kutembelea gari binafsi (private car) halafu akayumba kiuchumi na kujikuta anauza gari hilo; utamhurumia anavyohangaika. Mtu huyu akitembea barabarani kwa miguu ama akipanda daladala anahisi kama kila mtu anamwangalia yeye na kumsema.

Lakini wakati mwingine unaweza kuona watu wengi anaowahofia kuwa wanamsema hawakuwa hata na habari kama aliwahi kumiliki gari la kutembelea. Vivyo hivyo kwa huyu waziri ambaye anajikuta panga limempitia. Kila anakokwenda anahisi watu wanamnyooshea vidole, haoni tena kupokewa kama zamani, hana tena namba maalumu kwenye gari lake na hata simu za wadau zinazonyenyekea na kuita “mheshimiwa-mheshimiwa” anakuwa hazipati tena.

Kwa kuwa watu wanapochaguliwa kuwa mawaziri wanajua kuwa ipo siku watauacha uwaziri; iwe kwa kujiuzulu, kufukuzwa ama kumaliza muda wao; basi huwa wanajihami mapema. Hakuna aliye tayari kuona akishuka ngazi kimaisha. Hivyo mawaziri wengi hujikuta wakihangaika kuanzisha kampuni ambazo siku wakiondoka madarakani basi angalau ziwabebe ‘kiu-uwaziri’.

Nyumba ambayo atahangaika kuijenga ni ile ambayo siku akienda kuishi isilete ladha tofauti na ile ya ‘u-waziri’. Magari atakayonunua ni yale ambayo yataendana na mapigo ya ‘uwaziri’. Hata marafiki atakaoambatana nao atataka wawe ni wale ambao hata baada ya kuondoka madarakani watakuwa wakisemezana nae ‘kiuwaziri’.

Hili ni suala la mwito wa kisaikolojia na wala sio uchu wa madaraka. Je, waziri ama kiongozi mwingine anakabilinaje na mwito huu wa kisaikolojia? Hilo ni swali ambalo linahitaji makala nyingine.

Sasa tufanye tafakuri hapa. Je, waziri ama kiongozi mwingine aliyepo madarakani anawezaje kuandaa maisha yatakayofanana na hadhi yake baada ya kustaafu, kufukuzwa ama kuwajibishwa? Je, mshahara, marupurupu na kiinua mgongo chake kina ubavu wa kununua shangingi-V8 na kujenga mahekalu?

‘Anyway’ hili shangingi-V8 anaweza kununua, lakini je, kwa kutumia mshahara, marupurupu na kiinua mgongo ataweza kuihudumia kwa safari kama za uwaziri ama uofisa? Na kama ataweza ni kwa muda gani katika uhai wake asipokuwa na uwaziri ama uofisa? Je, ni kitu gani kitaendelea kumuweka karibu (baada ya kufukuzwa, kuwajibishwa, kujiuzulu ama kustaafu) na marafiki ambao yupo nao sasa kwa sababu ya uwaziri ama uofisa?

Mathalani; kwa mujibu wa taratibu za nchi yetu Marais na Mawaziri wakuu huendelea kutunzwa na serikali hadi kufa kwao. Pamoja na hilo wastaafu hawaambatani na misafara yenye misururu ya magari kama wakiwa madarakani. Hawafanyi uamuzi kama wakiwa madarakani, bila shaka hata ‘attention’ hawapati kama wanapokuwepo madarakani. Je, hili tunalitazamaje tunapoyatafakari maisha ya viongozi (kisaikolojia na kijamii) baada ya kustaafu kwao?

Maswali haya (ambayo tunayafanyia tafakuri) kikawaida hupita katika fahamu na akili za mawaziri, viongozi, maofisa na watumishi wengine wengi (japo yaweza kuwa si wote). “Automatically” baada ya kujiuliza maswali haya waziri ama ofisa hujikuta ameanza kuandaa maisha baada ya kufukuzwa, kujiuzulu, kuwajibishwa ama kustaafu.

Kiuhalisia hakuna waziri, ofisa ama mtumishi yeyote mwenye jeuri ya kuandaa maisha baada ya kuondoka kazini; yatakayofanana ama kukaribiana na hadhi ya cheo chake; kwa kutumia mshahara na marupurupu pekee. Hata ukichanganya na kiinua mgongo, bado sio rahisi kujenga mahekalu, kununua mashangingi na kuzunguka nayo sambamba na kuwa na marafiki wa hadhi ile ile ya cheo.

Kwa kuwa mishahara na viinua migongo havitoshi kutimiza ndoto za “maisha baada ya cheo kuchukuliwa”, mawaziri, maofisa na watumishi hawa huamua kuchukua njia mbalimbali.

Wengine huamua kuiba kwa kwenda mbele, wengine husaini mikataba ya kilaghai (10% commission), wengine huiba muda wa serikali lakini wapo wengi tu ambao huchukua njia halali za kuongeza kipato kupitia biashara, kampuni na kuanzisha miradi.

Kama nilivyotangulia kusema katika makala zilizotangulia katika mfululizo huu; Watanzania hatuamini katika mafanikio ya viongozi. Kiongozi akifanya biashara, akimiliki kampuni ama akifungua mradi ni nongwa.

Najua wazi kuwa tuna mkanganyiko katika sheria na kanuni zetu kuhusu uongozi na ujasiriamali (biashara) na hapa ndipo mahali ambapo mzimu unaowanyoa viongozi wetu ulipojificha.

Tuonane wiki ijayo 

0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com

 

 

1423 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!