Samatta: Naanza kuwaelewa wenzangu

Mshambuliaji nyota wa Aston Villa, Mbwana Samatta, taratibu ameanza kuuzoea mfumo wa uchezaji wa timu yake mpya. Samatta pia ni nahodha wa Taifa Stars na ni mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Akizungumza hivi karibuni, Samatta aliiambia tovuti ya klabu yake kuwa hivi sasa ameanza kuwaelewa na kuwazoea wachezaji wenzake katika timu hiyo aliyojiunga nayo Januari katika dirisha dogo la usajili.

Tangu ajiunge, tayari Samatta amecheza mechi kadhaa na kuifungia timu hiyo bao moja ingawa bado haijashinda mechi nyingi.

Juzi Jumapili Samatta na wenzake wa Aston Villa walishuka katika dimba la Wembley kupambana na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi.

Aston Villa ilimnunua Samatta ili kuziba pengo la mshambuliaji, baada ya wale iliokuwa inawategemea kuumia.

Samatta ni mmoja wa wachezaji ambao wamejiunga na Ligi Kuu nchini Uingereza na kuanza kuonyesha makeke yake moja kwa moja tangu ajiunge nayo kutoka Genk ya Ubelgiji.

Alifanikiwa kufunga goli katika mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Bournemouth, na kuingia katika orodha ya wachezaji waliowahi kufunga katika mechi ya kwanza katika Ligi Kuu nchini Uingereza (EPL).

“Naanza kuwaelewa wachezaji wenzangu jinsi wanavyocheza,” Samatta aliiambia tovuti ya timu hiyo.

“Kwa hiyo ninaelewa kuwa (Anwar) El Ghazi ni mshambuliaji wa pembeni na kila mara amekuwa akijitahidi kupiga krosi, kwa hiyo kila mara ninajiweka tayari kuzisubiri krosi zake.

“Kwa upande mwingine ninaelewa kuwa Jack (Grealish) ni mzuri akiwa na mpira, ana akili sana. Wakati mwingine atataka mpasiane wawili na wakati mwingine atataka umpe nafasi ampige chenga beki, kwa hiyo ninajitahidi kuwaelewa ili tuwe na muunganiko mzuri,” anasema Samatta.

Aston Villa imekwisha kucheza mechi tano tangu Samatta ajiunge nayo – dhidi ya Leicester City, Bournemouth, Tottenham Hotspurs na Southampton. Juzi Jumapili alitarajiwa kucheza mechi yake ya tano walipokabiliana na Manchester City.

Samatta amesaini mkataba wa miaka minne na nusu chini ya Kocha Dean Smith akitokea Genk kwa ada ya paundi milioni 10.

Katika mechi yake ya kwanza aliisaidia timu yake kuifunga Leicester City 2-1 na kufanikiwa kutinga fainali iliyochezwa Jumapili.

Samatta ana kazi kubwa ya kufanya, kwani timu yake ipo katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita Aston Villa ilikuwa na pointi moja tu juu ya mstari wa timu zinazoweza kushuka daraja msimu huu.

Timu hiyo ilikuwa na pointi 25 kutoka katika mechi 25 ilizokuwa imecheza.

Rekodi zaidi

Juzi Jumapili Samatta aliandika historia nyingine kadhaa katika maisha yake na soka la Tanzania. Siku hiyo Samatta alikuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika fainali ya Kombe la Ligi nchini Uingereza. Hili ni moja ya makombe yenye heshima sana nchini humo.

Pia, siku hiyo Samatta amekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Uwanja wa Wembley. Huu ni uwanja wenye hadhi ya juu kabisa nchini Uingereza na ni moja ya viwanja maarufu vya michezo duniani.