Huenda Kassim Dewji ni miongoni mwa viongozi wachache wa Simba wakiwa sehemu ya watendaji wa ‘Simba mbili’ zilizofanya maajabu kuliko Simba ya Manara.

Jumamosi ya Novemba 26, 1993 wakati Desre Koume na Jean Ball ‘Boli Zozo’ wanainyima Simba ubingwa wa CAF kwa magoli yao ya dakika za 17 na 77 waliyoifungia Stella Abdjan, Dewji alikuwa katibu mwenezi (nafasi inayofanana na ya Manara kwa sasa).

Wakati Simba inatinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa (Klabu Bingwa ya Afrika) mwaka 2003 kwa kuivua ubingwa Zamaleki ya Misri, Dewji alikuwa katibu mkuu. Nafasi kubwa zaidi ya aliyonayo Manara. Lakini kwa vyovyote vile, umaarufu wa Haji Manara wa Simba iliyofika hatua ya makundi ni mkubwa kuliko umaarufu wa Kassim Dewji wa Simba ya kizazi cha dhahabu. Alama ya Haji Manara ndani ya Simba itachukua muda mrefu kufutika kuliko ya Dewji na wengine.

Ndiyo, inawezekana ukasema umaarufu wa Manara dhidi ya Dewji unachagizwa na nyakati za teknolojia alizonazo Haji. Lakini ni wakati huu huu wa Haji Manara tunawaona wasemaji wa timu nyingine wakishindwa. Kuna wasemaji wengi tu wa klabu kubwa wanaonekana kama wamelala. Nafikiri Haji mwenyewe ana mchango mkubwa katika hili kuliko nyakati na teknolojia.

Kuna uwezakano watu wengi wa ukanda wa Afrika Mashariki haumfahamu Josep Vives wa Barcelona lakini wanafahamu kuhusu Haji Manara. Unaweza hata kushangazwa na idadi ya ‘followers’ wa Instagram kati ya Vives wa Barcelona na Manara wa Simba. Wakati Vives ana ‘followers’ wasiozidi elfu mbili, Manara ana ‘followers’ zaidi ya milioni mbili.

Haitashangaza kuona Waafrika wengi wanalijua jina la Haji Manara kuliko Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Manchester City, Simon Heggie. Haji ana usemaji wa soka la uswahilini. Mpira wa miguu ni mchezo wa watoto wa kimaskini ambao wengi wanapatikana uswahilini.

Manara anaturudisha kwenye somo la aina /makundi ya watu. Kuna aina nne za makundi ya binadamu zinazoweza kugawanywa kwenye makundi madogo manne, hivyo kuleta makundi 16. Aina mojawapo ndani ya hizo 16 ni ‘debaters’. Hili ni kundi la watu wabunifu wa njia za kudumisha utulivu  kwenye mazingira ya kazi hata kwa kutengeneza uongo wenye faida.

Ni watu wenye uwezo mkubwa sana wa kuchambua mambo. Ni watu wasiojali wanaumiza kiasi gani hisia za wengine ili tu wanaonekana wanachosema ni sahihi. Hutaka kufanana na ‘logicians’ kwa tabia ya kutumia nguvu kubwa kuwalinda wanaowaamini.

Lipo kundi jingine linaitwa ‘adventures’. Ni aina ya watu wanaopenda kufaidi maisha kwa gharama yoyote ile. Wanapenda kueleweka. Kwao maisha ya wengine si muhimu sana ilimradi ya kwao yanakwenda vizuri.

Haji Sunday Ramadhani Manara ‘De la boss’ ni mchanganyiko  wa Debater na Adventure. Haji yupo tayari kugombana na yeyote kwa ajili ya Simba (rejea bifu lake na Shafii wakati ule wa ‘underdog’). Yupo tayari kuwanyima furaha wengine kwa sababu ya Simba.

Wakati Simba ‘inatafunwa’ na kashfa zilizoibuliwa na Kabwili. Wakati Simba inafunga magoli ya ‘utata’ katika mechi mfululizo, wakati ‘boss’ wa klabu hiyo anatishia kususa. Wakati Simba inaruhusu goli karibu kila mechi. Pamoja na yote hayo Manara ameendelea ‘kuilinda’ Simba kupitia mdomo wake na kuonekana ni klabu bora zaidi.

Ni wakati huu Yanga wana Morisson ‘anayetembea’ juu ya mpira, ni wakati huu Yanga wanashinda mechi mbili mfululizo kwa kiwango bora kabisa. Ni wakati huu Yanga wana Haruna Niyonzima. Ni wakati huu Yanga inatoa bonasi ya milioni kumi kwa wachezaji wake kwa kila mechi inayoshinda. Pamoja na yote haya, bado Yanga inaishi maisha ya kinyonge kwa sababu ya ‘mdomo’ wa Haji Manara.

Soka linataka watu wa aina yake. Ni ‘mswahili’ mno utafikiri hajazaliwa Ulaya. Mpira wa miguu ni mchezo unaopaswa kuzungumzwa sana.

Zahera na Maurnho moja ya uimara wao ni pamoja na midomo yao. Wakati mwingine midomo hutumika kama silaha kwenye mchezo huu. Kwenye mechi iliyopita ya watani wa jadi, Haji alizunguka kwenye vyombo vya habari akihitahadharisha Yanga kuhusu namna nzuri ya kucheza na Simba.

Nyakati za mazuri ya Yanga yangekuwa Simba, mitandao ya kijamii ingesimama. Morrison angekuwa mchezaji wa Simba, kutembea juu ya mpira ingekuwa habari kubwa hata kuikaribia ya ugonjwa wa Corona.

Haruna Niyonzima kama angesajiliwa Simba, kwenye mitandao ya kijamii pangechimbika. Huoni hilo likifanywa na wasemaji wengine. Nguvu ya Haji imeleta hofu kwenye midomo ya wasemaji wengi. Unaituliza Simba kwenye pressure. Leo hakuna shabiki wa Simba anayemkumbuka Patrick Aussems kwa sababu ya mdomo wa Manara.

Anakera huku anafurahisha, anaudhi huku analiwaza, anakasirisha wakati huohuo anachekesha. Anatania huku anasema kweli. Anakuchukiza lakini hukomi kutembelea akaunti yake. Kuna uwezakano 70% ya ‘followers’ wa akaunti zake za mitandao ya kijamii ni Yanga anaowakera.

[email protected]

0629500908.