Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuandika makala hii kuhusu Kiwanda cha Sao Hill cha kuchakata magogo ili kupata mbao na bidhaa nyingine zitokanazo na miti au rasilimali misitu.

Kiwanda cha misitu – Sao Hill Industries Ltd – ni miongoni mwa viwanda vya mazao ya misitu vilivyokuwa vinamilikiwa na serikali kupitia Shirika la Viwanda vya Misitu lililokuwa likijulikana kama ‘Tanzania Wood Industries Corporation (TWICO) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kipo eneo la Shamba la Miti – SaoHill – linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Mufindi, Iringa. Kinapata malighafi kutoka kwenye shamba ambalo kwa miaka 10 (2008/2009 hadi 2017/2018) takriban hekta 40,000 zilipandwa miti.

Kwenye shamba hili vipo viwanda vidogo zaidi ya 400 vijulikanavyo kama ‘dingdong’. Vilevile vipo vyenye ukubwa wa kati na vilivyo vikubwa kama Kiwanda hiki cha Sao Hill Industries Ltd pamoja na Kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Mufindi Paper and Pulp Mill (MPM). Hiki kipo Mgololo karibu na Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Kama tujuavyo, serikali ilibadilisha sera zake kwa misingi kuwa ijiondoe kwenye biashara na kuachia sekta binafsi ndiyo ifanye hivyo. Kazi ya serikali ikabaki ya kusimamia utekelezaji wa sera na sheria; uperembaji na ufuatiliaji. Kwa hiyo viwanda vya misitu chini ya TWICO vikabinafsishwa.

Baada ya sera ya kubinafsisha mashirika na viwanda vya umma kupamba moto, ndipo Kampuni ya Green Resources kutoka Norway iliponunua na hatimaye kusimamia na kuendesha Kiwanda cha misitu cha Sao Hill. Januari, mwaka huu nilitembelea Kiwanda cha Sao Hill na kushuhudia kazi zinazofanywa hapo.

Kwanza, nitoe shukrani za dhati kwa Kampuni ya Green Resources Limited (GRL) ambayo ndiyo inamiliki kiwanda hiki, kupitia Mkurugenzi wake hapa Tanzania, Godlisten Minja, kwa kuniruhusu kutembelea kiwanda na kujionea shughuli zinazofanyika hapo.

Vilevile natambua watumishi wote na kazi nzuri inayofanyika kiwandani hapo. Kipekee namshukuru Victor Kimei, Meneja wa masuala ya Usalama ambaye alinipitisha kiwandani kuanzia sehemu ya kupokea magogo (log-yard) hadi maeneo mengine ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Kiwanda kina sehemu kuu mbili za uzalishaji wa mazao ya misitu. Kwanza, ni kwenye uchakataji magogo ambayo hutoa mbao za viwango mbalimbali na hatimye mbao hizo hutumika kwa mahitaji kadha wa kadha kama ujenzi, samani, milango na madirisha.

Pili, Kiwanda cha So Hill kinatengeneza nguzo za kusafirishia umeme au nyaya za simu au za shughuli nyingine,  vilevile na mahitaji mengine kama nguzo za kutengeneza uzio (fencing posts. Kwa miaka ya karibuni kiwanda pia kimeanzisha utengenezaji wa mkaa mbadala (briquettes) kutokana na mabaki ya magogo wakati mashine zinapochakata magogo kupata mbao.

Vilevile, yapo mabaki kutokana na mbao zinazotumika kutengeneza bidhaa nyingine ikiwa ni pamoja na vumbi wakati wa kuranda mbao ili kutengeneza bidhaa nyingine kama samani.

Kiwanda pia kinatumia vipande vya magogo visivyofaa kwa mbao na kuvichanachana hadi kuwa vipande vidogo (wood chips) ambavyo vinauzwa kwa Kiwanda cha kutengeneza karatasi cha MPM.

Zaidi ya hapo, kiwanda kina mitambo ya kuwekea mbao dawa (kulingana na mahitaji ya wateja) pamoja na nguzo za umeme (wood treatment plants). Ipo pia mashine maalumu ya kukausha mbao hadi kwa kiwango cha unyevu unaotakiwa ili kupata mbao za ubora wa hali ya juu.

Yapo manufaa kwa serikali na jamii inayozunguka kiwanda. Kwanza, kiwanda kinanunua miti (malighafi) kutoka shamba la miti, hivyo kulipa ushuru serikalini. Pia Serikali za Mitaa zinanufaika kupitia tozo ya asilimia tano ya ushuru (cess). Vijiji vinanufaika kutokana na ajira na huduma za kijamii (corporate services) zinazotolewa na kiwanda.

Kwa maelezo ya Meneja Rasilimali Watu, Jane Lyimo, kiwanda ni chanzo cha ajira kwa jamii iliyo karibu. Ajira ni za aina mbili: wafanyakazi wa kudumu na wale wa muda.

Kuna wafanyakazi wa kudumu 265 na wa muda ni kuanzia 200 hadi 1,000 kulingana na majira pamoja na hali ya kazi (nature of work). Hii ina maana kuwa ajira ni mapato kwa familia na watu wengi kuweza kumudu maisha kupitia kipato cha aliyeajiriwa.

Mathalani, watu 1,000 kama wana ajira na kila mmoja ana wategemezi sita kwenye familia yake hii ina maana wanufaika ni watu 6,000.

Pia Mifuko ya Jamii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali za Mitaa, Usalama Sehemu za Kazi (OSHA), na kadhalika, ni wanufaika kutokana na kodi, michango na tozo mbalimbali.

Kimsingi, viwanda vya misitu ni nguzo muhimu katika uchumi wa taifa letu na maendeleo ya jamii. Miti ikikomaa inatakiwa kuvunwa. Tukijaliwa kuwa na viwanda kama 50 vya aina hii hali ya uchumi wetu kupitia sekta ya misitu na nyuki itaboreka.

Viwanda kama cha Sao Hill vinahitaji malighafi ya kutosha na malighafi kuu ni miti. Kiwanda kinatumia aina mbili za miti: mikaratusi (Eucalyptus and Pine species) na aina zote mbili zinastawi kwenye maeneo mengi nchini. Nitoe mwito kwa Watanzania wenye ardhi ya kutosha watumie ardhi vizuri ikiwa ni pamoja na kuanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya kutoa malighafi kwa viwanda vya misitu.

Kwa kufanya hivyo tutaongeza fursa za ajira na kipato kwa aliyepanda miti, jamii na serikali. Takwimu zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa miti takriban meta za ujazo  milioni 19. Ili kuziba pengo hilo tunahitaji kupanda miti kwa wingi.

Tukijaliwa kupanda miti hekta 185,000 hadi 200,000 kila mwaka tutafikia hali ya matumizi endelevu ya rasilimali misitu yetu. Hivyo kuchochea ukuaji wa viwanda vya misitu na hatimaye kuongeza tija kwenye uchumi wa viwanda Tanzania.

Kwa hali hiyo, misitu itachangia kuinua kipato kwa mtu mmoja mmoja mijini na vijijini. Kwa maelezo niliyopata, soko la mbao linapanuka kila mwaka na uzalishaji wa mbao za kutosha bado ni kitendawili. Kwenye matoleo yajayo nitafafanua zaidi kuhusu hali hii na nini kinafanyika kiwandani Sao Hill. Penye nia pana njia. Tutafanya, ni muhimu tufanye na tutafanikiwa.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa simu: 0756 007 400.

By Jamhuri