SIMON+MSUVAWakati mshambuliaji chipukizi wa yanga mwenye kasi, Simon Msuva, akimaliza majaribio yake nchini Afrika Kusini, wadau mbalimbali wa soka wamempongeza kwa kuthubutu.
Ingawa uongozi wa Klabu ya Yanga ulisema kuwa unakusudia kumuadhibu mchezaji huyo na klabu aliyokwenda kufanya majaribio, lakini baadhi ya wadau wanasema amechukua uamuzi sahihi.
Baadhi ya wadau wanauunga mkono uongozi wa Yanga, uliosema kuwa utamuadhibu Msuva kwa kutoroka na kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga unakiri kuwa Msuva aliomba ruhusu, lakini akanyimwa ndiyo maana akaamua kutoroka siku chache baada ya kurejea nchini akitokea Tunisia, ambako aliichezea Yanga katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho na kutolewa na Etoile Du Sahel ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-1.
Miongoni mwa wadau hao ni Kocha maarufu nchini, Kenny Mwaisabula, maarufu kwa jina la Mzazi, na nguli wa zamani wa Yanga, Sekilojo Johnson Chambua, ambao wamesema Msuva amefanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi, kwa sababu tayari ameshaona kigezo.
Mzazi alisema kigezo cha Msuva na wachezaji wengine wanaopata nafasi ya kwenda nje ni mafanikio ya wenzao Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, wanaokipiga TP Mazembe ya DR Congo, pamoja na kukosa mafanikio kwa nyota waliozichezea nafasi hizo.
“Mzazi, wachezaji wa sasa wakizichezea nafasi hizi tutawashangaa kwa sababu tayari wana kigezo, wawatizame kina Samata na Ulimwengu kabla ya kugeuza jicho na kuwaangalia wachezaji wa zamani waliozichezea bahati hizi walipozipata, wapo wengi kama kina Edibily Lunyamila, Sekilojo Chambua, Athumani China na wengine wengi sana,” anasema Mzazi.
Anasema vijana wa sasa wanatakiwa kutumia mwanya wa unafuu wa kuwapo kwa teknolojia kujitengenezea mipango ya kimaisha kupitia soka, licha ya kukosekana mawakala wala mameneja wanaoweza kuwatafutia timu zenye maslahi na mikataba mizuri ya kazi, lakini wapambane hivyo hivyo kupitia kuonekana kwao kwenye runinga kujiuza.
Akizungumzia hilo, Chambua anasema kama atapata nafasi ya kuzungumza na wachezaji hao atawataka wasizipoteze nafasi hizo kwa sababu maisha ya soka ni mafupi.
“Bwana, hawa wachezaji wetu wala wasidanganyike kudhani kwamba nafasi hizo zitakuja mara mbili, pale wanapozipata tu wazichangamkie haraka,” anasema Chambua.
Anasema kuwa hivi sasa viongozi wa klabu na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wana mwamko, hivyo kutakuwa na unafuu wa kufanikisha mipango ya kwenda nje ukilinganisha na enzi zao.
“Unajua kuna tofauti na viongozi wa sasa na wale wa enzi zetu, kipindi kile viongozi walipoletewa ofa walizikalia kwa hiyo hatukuwa na cha kufanya, waliishia kutusihi tusiondoke na kutupa ahadi nyingi ambazo pia hawakuzitekeleza,” anasema.
Chambua aliongeza kusema kuwa tofauti na kazi za utaalamu, soka lina umri wake ukipita basi, kwa hiyo, anampongeza na kumfahamisha Msuva na wanasoka wengine kwamba wanapaswa kujua hilo na kuzitumia nafasi zinazojitokeza.
“Soka lina muda mfupi sana, kwa hiyo unapaswa kuutumia muda huo vizuri, hii siyo kama sheria, we angalia mtu kama mzee wetu Said Hamad El Maamry ana miaka zaidi ya 70 lakini bado anafanya kazi yake ya kitaalamu ya sheria, utamuona mara Mahakama Kuu mara Mahakama ya Rufani mara Kisutu lakini soka sana sana utacheza hadi miaka 35 baada ya hapo huwezi,” anasema.
Mbali ya hapo, pia wadau mbali mbali wameutaka uongozi wa Yanga kutomuadhibu mchezaji huyo aliyewafungia mabao 17 yaliyosaidia kuwapa Ubingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, ukiwa ni wa 25 kwa klabu hiyo.
Msuva ambaye awali inadaiwa amekwenda kufanya majaribio Orlando Pirates na baadaye taarifa zikasema ni klabu nyingine pia ya Ligi Kuu Afrika Kusini, anatarajiwa kurejea nchi wakati wowote kuanzia leo na atabaki akisubiria majibu ya majaribio, ingawa watu wake wa karibu wanasema aling’ara na ana matarajio makubwa ya kufuzu.

By Jamhuri