Kwa muda wa mwezi mmoja tumechapisha habari zinazohusiana na ukusanyaji wa kodi. Tunatambua na tunapenda kupongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyotekeleza kwa ufasaha maelekezo ya Rais John Pombe Magufuli ya kutaka kodi ikusanywe bila kuangaliana usoni.

Alipokutana na wafanyabiashara mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alisema anawasihi wafanyabiashara kulipa kodi kwa nia ya kuiwezesha Serikali kugharimia maendeleo. TRA imebana maeneo mbalimbali hasa eneo la Bandari ambako kwa mara ya kwanza tumeshuhudia wafanyabiashara kama Said Salim Bakhresa wakibanwa na kulipa kodi.

Makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 900 na kufikia trilioni 1.3, mwezi Novemba na trilioni 1.4 mwezi Desemba. Kiwango hiki ni kikubwa kupata kukusanywa katika nchi hii. Hata hivyo, sisi tunaamini bado kiasi kinachokusanywa kinaweza kuongezeka mara mbili au zaidi iwapo tu watu wote wanaostahili kulipa kodi watalipa kodi badala ya kutegemea mishahara ya wafanyakazi tu.

Uchunguzi tuliofanya unaonesha kuwa kuna upotevu mkubwa katika kodi ya mauzo. Zaidi ya asilimia 90 ya bidhaa zinazouzwa hapa nchini wahusika hawapewi risiti. Hata wanaotoa risiti, wapo wanaoandika risiti inayoitwa ya kutembeza mzigo kwa maana kwamba mtu ananunua mzigo wa Sh 1,500,000 lakini anaandikiwa risiti ya Sh 15,000.

Mwaka 1998, nchi jirani ya Kenya ilibuni mbinu tunayoweza kuiazima. Serikali ilisambaza askari polisi nje ya maduka jijini Nairobi na maeneo mbalimbali ya nchi. Askari hawa walikuwa hawakamati raia, bali walikuwa wakimkagua kila aliyenunua bidhaa yoyote. Iwapo mtu alinunua bidhaa bila kupewa risiti, askari walimlazimisha kurudi dukani kuchukua risiti.

Askari walikuwa wanakagua thamani ya mzigo pia. Iwapo mtu ananunua bidhaa akaandikiwa risiti yenye thamani ndogo, basi mteja alikuwa anarejeshwa dukani kuandikiwa risiti yenye thamani halisi. Mwezi wa kwanza Rais Magufuli alipoingia madarakani, vituo vingi vya mafuta vilifunga mashine za kutoa risiti mara tu mteja anapomaliza kuwekewa mafuta kwenye gari. Hivi sasa wamerejesha kauli kuwa mtandao wa TRA hausomi.

Sisi tunaishauri Serikali iazime busara hii ya Kenya hata kwa kuanza na angalau wilaya moja tu ya Ilala katika eneo la Kariakoo, kisha baada ya mwezi mmoja au miwili Serikali ijipime na kubaini imeongeza makusanyo kiasi gani na ufanisi ukiwapo utaratibu huu usambazwe nchi nzima. Tukitarajia wafanyabiashara wajihimu wenyewe na kutoa risiti kwa usahihi bila shuruti, TRA na Taifa tutasubiri mno.

Tunasema kama Kenya inaweza kuendesha uchumi wake kwa asilimia 95 ya kodi za ndani bila kutegemea wafadhili, sisi tumelaaniwa na nani hadi maisha yetu yategemee wafadhili wanaotupa misaada yenye masharti? Kwa kuwa Rais Magufuli ameonesha nia ya kulitumikia Taifa hili, basi tuunge mkono juhudi zake, tuhamasishane kodi ikusanywe tuboreshe huduma za jamii kama maji, usafiri, barabara, elimu, afya na nyinginezo. Tujaribu mbinu hii, inawezekana.

By Jamhuri