Michuano ya ngumi Afrika inatarajiwa kufanyika Casablanca, Morocco, baadaye mwezi huu, wakati Tanzania imeteua mabondia 13 watakaoiwakilisha huko, baada ya kuonesha uwezo mzuri katika mashindano ya Taifa yaliyofanyika Dar es Salaam, hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makoye Mashaga, ana imani na wachezaji hao wanaokabiliwa pia na mashindano mengine mbalimbali yakiwamo ya Kanda ya Sita Afrika, Jumuiya ya Madola na ya Dunia.


Mabondia hao na uzito wao kwenye mabano ni Saidi Hofu na Hafidh Bamtullah (fly), Sunday Elias na Boniface Mlingwa (light fly), Emilian Patrick na Undule Lanson (bantam), Idi Pialali, Khamis Kitenge na Nasser Mafuru (super bantam).


Wengine ni Victor Njaidi na Hashim Saimon (welter), Seleman Kidunda na Mohammed Chibumbuli (light welter), Joseph Martin (middle), Amos Godwin na Leonard Machichi (light heavy), Haruna Swanga na Nuru Ibrahim (kilo 90) na Maxmilian Patrick anayetwangana ngumi katika uzito wa kilo 91+.


Hata hivyo, kuna hofu kuwa huenda kambi itakayopigwa na timu hiyo ya mabondia ikawa zimamoto kutokana na BFT kutokuwa na wadhamini, wafadhili binafsi, kampuni na vyanzo vyake yenyewe vya fedha, hali inayoweza kuifanya itetereke na kutofanya vizuri katika mashindano hayo.

 

Wakati wa mashindano ya Taifa jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, BFT haikuwahudumia ipasavyo mabondia hao. Kwa mfano, iliwazawadia washindi Sh 30,000, kiasi ambacho hakitoshi hata kwa nauli ya kuwarudisha mikoani kwao Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Rukwa, Katavi, Kigoma na kadhalika.


Pamoja na Mashaga kutamba kwamba uteuzi huo umefanyika kwa makini ili kupata timu bora itakayoiwakilisha vyema Tanzania, tatizo la ukata linaweza kuwapunguzia morali, hasa endapo Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo nayo itashindwa kuwasaidia.

 

Serikali mara nyingi imekuwa ikisimamia zaidi Timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars), lakini imeshindwa kufanya hivyo kwa timu za riadha, netiboli, tenisi, magongo, kuogelea, gofu, baisketi, mpira wa mikono, wavu na kadhalika.


Taswira hiyo inaonesha kuwa Serikali haijadhamiria kwa dhati kuhamasisha michezo mingine zaidi ya mpira wa miguu nchini.


Ikiwa Serikali haitaweka mchango wake kipindi hiki, BFT inaweza kushindwa hata kuwasafirisha mabondia hao kwenda Casablanca kutokana na ukosefu wa fedha, na hata ikibahatika kufika huko si ajabu ikawa jamvi la kujinyakulia ushindi kwa mabondia kutoka nchi nyingine.

5979 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!