Moja ya habari zilizobeba uzito wa juu katika gazeti hili ni ile inayomhusu raia wa Uswisi, Dk. George Hess, anayetuhumiwa kumiliki na kuuza ufukwe wa Amboni uliopo Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga kinyume cha sheria.

Dk. Hess ambaye anayeishi nchini Kenya, kupitia tovuti yake ya ambonibeach.com, amejitangazia ‘Jamhuri’ katika eneo hilo, huku Serikali ikionekana kutochukua hatua zinazostahili dhidi yake. Dk. Hess anapata ujasiri wa kujihusisha na vitendo hivyo, huku sheria zilizopo zikikataza wazi kuwa raia wa kigeni haruhusiwi kumiliki ardhi nchini.


Taswira hiyo inaweza kuwafanya wengi kuamini kwamba si Dk. Hess pekee, aliyepata mwanya wa kukiuka sheria kwa kujitwalia ardhi na rasilimali nyingine holela kana kwamba nchi haina wenyewe. Serikali na vyombo vyake vya dola vichukue hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na kumfuatilia Dk. Hess kubaini iwapo kweli ana uhalali wa kumiliki ufukwe na kuuza sehemu ya eneo hilo.

 

Watanzania wanataka kusikia na kuona raia huyo wa kigeni anamulikwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa itathibitika ametenda makosa hayo. Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa mfumo wa utawala wa kisheria, hivyo raia yeyote wa ndani na nje ya nchi hapaswi kufumbiwa macho pale anapothibitika kuvunja sheria na kutapanya mali za nchi.


Sisi JAMHURI tunadhani ni wakati mwafaka kwa Serikali kuanza uchunguzi wa kina dhidi ya Dk. Hess, kwani huenda anatenda makosa mengine zaidi ya hayo ya kumiliki na kuuza ardhi kinyume cha sheria. Matumaini ya wengi ni kwamba viongozi wa Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Uwekezaji na Uwezeshaji, pamoja na vyombo vya dola watafuatilia suala hilo na kuchukua hatua zinazostahili.


Hatuwezi kuacha nchi yetu ivamiwe na raia wa kigeni ambao – ama wanatumia rushwa au ulaghai – kuhujumu mali za umma huku wazawa wakiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini uliokithiri.


Sisi JAMHURI tunasema ni aibu kubwa ikiwa kweli Dk. Hess amepata mwanya wa kumiliki na kuuza ardhi nchini kinyume cha sheria. Tunasema adhibitiwe ili liwe fundisho kwa wengine wanaojiandaa kufanya makosa ya aina hiyo.


By Jamhuri