Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ni mali ya Watanzania kwa asilimia 65. Sehemu nyingine ya hisa ndiyo inayomilikiwa na wawekezaji.

Kwa miaka zaidi ya 10, TTCL imeachwa yatima. Hakuna waziri, naibu waziri wala Katibu Mkuu yeyote wa wizara yenye dhamana na mawasiliano, aliyeweza kukutana na wafanyakazi.

 

Menejimenti ya TTCL inajiendesha kadri ya utashi wake. Bodi imebaki kufaidi posho ya vikao inayofikia Sh milioni kwa kila mjumbe kwa kila kikao. Kuna wizi wa fedha wa mabilioni ya shilingi.

 

Kiongozi wa TTCL alipaswa kuwa ameshastaafu, lakini kwa namna ya kipekee ya kulindana katika nchi hii, ameongezwa mkataba huku vijana wenye ari, nguvu na dhamira za kulitumikia Taifa lao wakiachwa bila ajira.

 

Kwa wiki kadhaa sasa tumekuwa tukiandika juu ya mkataba tata ambao TTCL imeingia na kampuni moja ya ulinzi. Mkataba huo wenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 740 ni wa ujanja ujanja kwa kila namna. Imebainika kuwa kampuni haina walinzi wa kutosha wala silaha kama ilivyojitanabaisha kwenye mkataba huo uliosainiwa mwaka jana.


Kwa ufupi ni kwamba TTCL imeachwa iwe shamba la bibi ambalo kwa kawaida kila anayetaka kuchuma tunda huachwa achume bila kuulizwa!


Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa pamoja na kelele zote zinazopigwa kuhusu hujuma ndani ya kampuni hii ya umma, wahusika wametia pamba masikioni. Wabunge wamekuwa makini sana kuhoji Tanesco na mashirika mengine, lakini kwa TTCL ni kama na wao wanapata mgawo.


Tunatoa wito kwa Waziri mwenye dhamana kuzinduka na kuhoji yanayoendelea ndani ya TTCL. Tunatoa wito kwa wabunge kuhoji utendaji kazi wa kampuni hii. Tunamwomba Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ‘special auditing’ abaini siri kubwa za ulaji zilizojikita ndani ya kampuni hii.

 

Haya mambo yanapaswa kufanywa haraka kabla TTCL haijazikwa na walaji waliomo ndani. Kama imewezekana Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirik la Reli Tanzania (TRL) na kwingineko, tunaamini hata TTCL itawezekana.


By Jamhuri