Naanza maelezo yangu kwa kusema yafuatayo: Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake; siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo; nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

Kweli haipendwi na binadamu yeyote mwenye sifa ya uovu au dhuluma, au unafiki. Kwa sababu kweli inatoa maana halisi na sahihi kutokana na neno lililozungumzwa, kusemwa au kutendwa na binadamu huyo.

 

Nakuomba msomaji wa makala haya uwe mtulivu na makini. Utafakari mada ya udini ninayoiweka mbele yako, ni nyeti. Inatoa maana halisi ya udini na chanzo chake hapa nchini.

 

Naomba radhi kwa Watanzania kusema si busara hivi sasa kuendelea kupambia, kulaumu na kuzungumza matokeo ya udini, badala ya kuanza kutazama na kuzungumza chanzo na sababu ya kuwapo kwa udini. Pili nini kifanyike kuondoa udini.

 

Wakati umefika Watanzania lazima tuyazoeshe masikio yetu kuyasikia tusiyoyapenda kusikia na bongo zetu zijenge tabia ya kupokea yaliyosikika na kuyatafakari bila mashaka. Hilo ndilo tibabu laNaanza maelezo yangu kwa kusema yafuatayo: Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake; siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo; nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

 

Kweli haipendwi na binadamu yeyote mwenye sifa ya uovu au dhuluma, au unafiki. Kwa sababu kweli inatoa maana halisi na sahihi kutokana na neno lililozungumzwa, kusemwa au kutendwa na binadamu huyo.

 

Nakuomba msomaji wa makala haya uwe mtulivu na makini. Utafakari mada ya udini ninayoiweka mbele yako, ni nyeti. Inatoa maana halisi ya udini na chanzo chake hapa nchini.

 

Naomba radhi kwa Watanzania kusema si busara hivi sasa kuendelea kupambia, kulaumu na kuzungumza matokeo ya udini, badala ya kuanza kutazama na kuzungumza chanzo na sababu ya kuwapo kwa udini. Pili nini kifanyike kuondoa udini.

 

Wakati umefika Watanzania lazima tuyazoeshe masikio yetu kuyasikia tusiyoyapenda kusikia na bongo zetu zijenge tabia ya kupokea yaliyosikika na kuyatafakari bila mashaka. Hilo ndilo tibabu la matatizo yatupatayo likiwemo hilo la udini. Vinginevyo tutaendelea kulaumiana na kudharauliana na mwishowe ni kupigana, kuuana na hata kuikimbia nchi yetu na kuwa wakimbikiz. Kisa ni kuukataa ukweli.

 

Ni muda mrefu umepita sasa, tangu neno udini lipewe mawanda ndani ya vinywa vya Watanzania na kufanya hewa ya nchi ya Tanzania kujaa harufu ya udini. Udini ni neno jepesi kulitamka lakini ni zito kulibeba na ni hatari kulilea. Kwa sababu linajenga chuki, uhasama na uadui wa kudumu ndani ya dini moja au nyinginezo mbalimbali katika jamii.

 

Si nia yangu kulaumu bali ni kuweka kadhia kutokana na matukio ya udini yaliyojiri sehemu mbalimbali. Kule Uingereza na Ireland ya Kaskazini watu waliuana kwa bunduki kwa sababu ya udini. Wote ni dini moja ya Ukristo, isipokuwa walio wengi Waprotestanti –Anglikana – wanadai Ireland Kaskazini ibaki kuwa upande wa United Kingdom (Uingereza).

 

Wakatoliki wao wanataka Ireland Kaskazini iwe ni sehemu ya ‘Irish Republic’, huo ni ubinafsi.

 

Watu wa Iran na Iraq wote ni Waislamu. Lakini walipigana takriban miaka minane (1980-1988) wakigombea mipaka ya nchi hizo, eti msingi wake ni Sunni na Shiah zikiwa madhehebu ya dini ya Kiislamu.

 

Nchini Lebanon Waislamu na Wakristo wa nchi moja walipigana kwa chokochoko za udini zilizoanza 1970 kati ya Wakristo kuikataa PLO na Waislamu kuikubali PLO (Palestine Libaration Organization), hatimaye kuangukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1975.

 

Kule Sudan, Waislamu wa Sudan na Wakristo wa Sudan Kusini walipambana vikali kwa sababu ya mgawo wa rasilimali za nchi na sheria za dini zinazozingatia dini ya upande mmoja (Shariah). Rwanda watu wote wa dini moja na madhehebu ya aina moja ya Ukristo, Katoliki walichinjana na kuuana sababu za tabaka za hali na ukabila wenye asili ya udini.

 

Wasomali nao nchi moja na dini moja – Waislamu. Walinyukana bila hadhari kwa misingi hiyo hiyo ya upendeleo ndani ya dini moja. Matukio mengi mengineyo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokea duniani tunayafahamu yenye vyanzo vya udini. Ndiyo maana Watanzania tulio wengi tunapinga na kulaani udini nchini usipewe nafasi ya kuranda.

 

Haitoshi hata chembe kudhani kwamba kupiga mayowe kutaondoa udini. La hasha! La hasha mara lukuki. Nakataa Dar es Salaam Jazz Band kati ya nyimbo zake, wimbo mmojawapo una maneno yafuatayo: ‘Mtoto wacha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe.’

Watanzania nawasihi tuache kupiga mayowe na wala tusingoje tuone wenyewe! Kwa sababu madhara hayo ya kuona yana idhilali. Iwe nchini mwetu, au nchi za wenzetu, kama tulivyoona hapo awali, kitovu au chanzo cha udini ni ‘unafiki dhidi ya haki.’

Mtu mnafiki ana dalili tatu. Kwanza akisema husema uongo, pili anapoahidi hatimizi, tatu anapoaminiwa hufanya hiyana au inda. Hii ina maana kuwa anasema kinyume cha anavyotenda, hatimizi kile alichosema na ni mdanganyifu – mwongo.

Haki ni stahiki ambayo mtu anastahili kuwa nayo. Haki haitoki kwa binadamu. Haki inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Anachofanya binadamu ni kuweka maelewano, makubaliano na mapatano katika haki, kutoa malipo, mgawo au ada chini ya utaratibu wa sheria na kanuni ndani ya jamii.

 

Udini ni kitendo anachofanya mtu wa dini moja kuipenda dini yake sana hata kumpa mtu haki isiyokuwa yake mtu wa dini yake, na kumnyima au kumdhulumu haki hiyo mtu wa dini nyingine, kufanya upendeleo.

 

Tuhuma nyingi zinazotolewa na kuelekezwa serikalini, kwenye vyombo vya dini, viongozi wa dini na mtu mmojammoja, kuendekeza udini katika uamuzi wa kutoa haki, madaraka na ajira. La kushangaza baadhi ya watu katika jamii ya Tanzania wanajifanya kuifahamu au hawataki kufahamu madhara ya upendeleo wa udini.

 

Kila siku vyombo vya habari vinaimba ‘Udini’ na kutoa kauli kali kuhusu vitendo vya udini. Hali kadhalika, wapo viongozi wa dini, wao ndiyo waliojigawa katika makundi mawili. Kundi moja linashindwa au halitaki kukemea wanaotumia madaraka yao vibaya kwa muono wa dini, lakini linadai serikali ikomeshe udini. Kundi jingine linalaani kutamalaki kwa udini na kutaka serikali ikomeshe udini, lakini linapuuzwa na serikali na jamii.

 

Serikali inatakiwa kudhibiti udini ina makengeza katika dini. Jicho la kushoto linaona serikali haipaswi kuingilia mambo ya dini kwa sababu eti haina dini. Jicho la kulia linaona dini ni mojawapo ya ngao zake katika kuwadhibiti na kuwahukumu raia wake wenye kutenda maovu au kwenda kinyume cha sheria za dola.

 

Si hivyo tu, serikali inatuhumiwa kama mshirika mkubwa katika vitendo vya udini, na ni ngao ya kukinga malalamiko na madai dhidi ya udini. Yote hayo kwake serikali ni ndumakuwili.

 

Ifahamike kwamba suala la udini halikuanza hivi karibuni kama baadhi ya watu wanavyotaka kutuaminisha. Udini nchini mwetu ulianza tangu ukoloni ulipoingia na kuanzisha utawala wake. Naanzia hapo kwa sababu ndiyo chanzo cha udini na mtafaruku ulipo hivi sasa.

 

Mwaka 1885, wakati wakoloni wa Kijerumani walipoingia Afrika Mashariki na kuanza kupanua utawala wao kutoka pwani hadi bara, walikuta lugha ya Kiswahili ikitumiwa na wafanyabiashara wa pwani na bara. Pia lugha hiyo ilikuwa ikitumiwa na Wamisionari katika kueneza mafunzo ya Biblia.

 

Lakini wamisionari wa Kijerumani na wa madhehebu ya Kilutheri walipinga sana matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa sababu:

  • á Kiswahili ni lugha ya kitumwa iliyotumiwa na Waarabu katika kuendeleza utumwa.
  • á Kiswahili kinaambatana mno na dini ya Kiislamu, kwa hiyo kikiruhusiwa kutumika kitafanya kazi ya kueneza dini ya Kiislamu kwa urahisi na hivyo kuhatarisha maendeleo ya uenezi wa dini ya Kikristo hasa huko Bara.
  • á Wakristo hao walidai lugha za kikabila ndizo zitakazofaa kutumika katika mafunzo ya Biblia.
  • á Walutheri walidai pia serikali ilikuwa inawaajiri watumishi wenye ujuzi wa Kiswahili ambao wengi wao walikuwa Waislamu wa pwani, kwa hiyo serikali ilikuwa inaendesha upendeleo kwa dini ya Kiislamu na  kuiweka kando dini ya Kikristo.

Lakini madhehebu ya Kikatoliki na ya UMCA (Anglikana), yaliunga mkono uamuzi wa serikali wa kutambua lugha ya Kiswahili katika shughuli zake mbalimbali na kufundisha shuleni. Makanisa ya Kiroma na ya UMCA yalitumia Kiswahili kwa kuanzisha magazeti.

  • á UMCA walianzisha gazeti la Habari za Mwezi mwaka 1895.
  • á Wakatoliki walianzisha gazeti la Kiongozi mwaka 1905.
  • á Hatimaye Walutheri walikubali uamuzi wa serikali kutumia Kiswahili na wao kuanzisha gazeti la Pwani na Bara mwaka 1910.

Ulipoingia utawala wa Kiingereza mwaka 1919, nao ulileta elimu iliyokuwa ya ubaguzi wa rangi na dini. Shule nyingi ziliendeshwa na mashirika ya dini mbalimbali. Kwa sababu ambazo si za dini yalijenga tabia ya uhasama mkubwa baina ya vijana wa madhehebu haya na yale, au wa madhehebu yale yale.

 

Serikali yenyewe ilisomesha vijana kwa lengo au madhumuni maalum ya kuwapa kazi ambazo hazitahatarisha utawala wake. Vijana waliokuwa na nidhamu ya woga walipendwa na wale waliokuwa wadadisi walifukuzwa shule mapema. Elimu ilikuwa si kwa wote kwani ilikuwa ama ya gharama au vizingiti.

 

Waarabu walijikita zaidi katika kufundisha dini ya Kiislamu na kufanya biashara. Hivyo wenyeji wa pwani hadi bara waliipokea dini ya Kiislamu wakawa Waislamu. Hivyo ni vigumu Mwislamu kuacha dini yake ya kweli kwa mujibu wa kitabu chake, yaani Qur’an na kufuata dini nyingine. Hata hivyo, Waislamu wachache mno walikubali ubatizo (Ukristo) ili wapate elimu.

 

Wote tunakubali kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Kumnyima mtu au kundi moja ni sawa kumnyima mtu au kundi hilo maendeleo ya maisha yeke au yao katika uchumi madaraka, ajira na tija nyinginezo.

 

Tangu kupevuka kwa harakati za kudai Uhuru mwaka 1953 chini ya TAA (Tanganyika African Association) na kushamiri kwa harakati hizo chini ya TANU, mwaka 1954; suala la elimu lilipewa nafasi pekee katika mazungumzo na mipango ya kudai uhuru katika vikao mbalimbali. Waasisi wa TANU walio wengi walikuwa Waislamu walionyimwa elimu na Mkoloni kwa sababu tu ya udini lakini walitambua thamani ya elimu kutoka katika elimu yao ya dini ya Kiislamu.

 

Rais wa TANU, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikiri mara kadhaa kuwapo ubaguzi wa utoaji elimu katika mazingira ya kidini kwa wananchi, na hasa Waislamu waliodhulumiwa haki yao ya elimu na kupewa wenzao wasio Waislamu. Mwalimu aliahidi kuondoa kasoro hiyo TANU itakapotawala nchi.

 

Baada ya mkutano wa kwanza wa TANU tangu kuzaliwa na kumchagua Mwalimu Nyerere kuwa Rais wa kwanza; madhumuni ya TANU yalitangazwa. Moja ya madhumuni hayo ni kuhusu elimu. TANU ilisema lazima watoto wa wananchi wapate nafasi zaidi ya kusoma katika shule zote za msingi na sekondari.

 

Imani ya kupata elimu zaidi na bora ilijengeka pale TANU ilipofanya Mkutano Mkuu wa mwaka mjini Tabora mwaka 1958 na kupitisha Azimio la kuanzishwa Chuo Kikuu. Aidha, umuhimu wa elimu ya ufundi na elimu kwa wote pamoja na elimu ya watu wazima.

 

Lakini, ukweli ni kwamba matatizo ya kutumia dini yaliendelezwa tangu wakati wa kuunda TANU mwaka 1954 na baada ya Uhuru. Kwani aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU, Sheikh Sulemani Takadir katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika mjini Tabora mwaka 1958, alitoswa baada ya kutoa madai ya kutumika udini katika shule ya mchanganyiko ya Ugweno kwa kusema; “Nimepata barua kutoka shule ya Waislamu ya Ugweno kuwa nafasi zote zimechukuliwa na Wakristo na kwamba watoto wa Waislamu wanateswa.”

 

Kwa kauli hiyo alinyang’anywa kadi ya TANU ya uanachama na kufukuzwa chamani, kwa madai ya kutaka kutia sumu ya dini ya TANU.

 

Mwaka 1960 baadhi ya masheikh na walimu wa Kiislamu waliunda chama cha siasa cha All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Baada ya kuundwa chama hicho, Kamati kuu ya TANU iliunda tume yenye wajumbe mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu kupinga kuwapo kwa chama hicho kwa madai kuwa ni cha dini. Pili, kuwaelewesha Wakristo na Waislamu madhumuni ya TANU na ubaya wa kutumia vyama vya dini kuwagawa wananchi.

 

Tume hiyo ilipofika Kigoma iligundua karatasi zilizotayarishwa na mapadre kuwashawishi Wakristo, kwamba Waislamu hawakuwa na elimu na kuwataka Wakristo wote popote walipo waungane kuwanyima Waislamu nafasi za uongozi wa Taifa.

 

Katika Uchaguzi Mkuu wa Pili wa Tanganyika uliofanyika Julai 1960, katika Wilaya ya Mbulu mkoani Arusha, iliyokuwa ‘Mbulu Tribal Council’ iliazimiwa kwamba Chifu Amiri Dodo, mjumbe wa TANU, asipewe kura.

 

Naye Chifu Sarwatt alitoa agizo kwa wajumbe wake kuwa kura apewe mwanawe Herman Ngildi Sarwatt na baadhi ya wakuu wa madhehebu ya dini walikuwa wanahubiri kwamba Chifu Amiri Dodo ni Mwislamu, kwa hiyo wampigie kura Herman Ngildi Sarwatt ambaye ni Mkatoliki. Katika uchaguzi huo, TANU ilishindwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za udini na ukabila.

 

Baada ya kueleza yote hayo hebu tutafakari kauli zifuatazo, zilizowahi kutolewa na viongozi wafuatao:

I. “Tulikuwa hatujali kabisa dini ya mtu hata kidogo. Tulikuwa hatuchagui mtu kwa dini yake, kwani anakuja kusalisha hapa?” Kauli hii ilitolewa na Mwalimu Julius K. Nyerere.

II. “Katika hali halisi kuna ukiukaji wa haki na matumizi mabaya ya madaraka, ambapo tabia hii inaelekea kukubalika na kupewa hadhi ya utamaduni.” Hii ilitolewa na Padre Vic Missiaen.

 

Kwa leo katika sehemu hii ya kwanza ya udini, napiga magoti kwa serikali na kuiambia yafuatayo:

Nasema mapema kwa serikali suala la udini lipo na limetamalaki. Katika suala hili serikali iache purukushani. Ichukue hatua za haraka na kuzingatia busara katika kuliondoa kwani hata tume ya marekebisho ya Katiba imekiri hadharani kuwa udini upo.

Lakini pia serikali isijadili na kuhukumu matokeo ya udini, bali itafute kwa kina chanzo cha udini na maana halisi ya neno ‘Udini’. Wahenga walisema ‘mdharau mwiba mguu huota tende’.

0717 113 542 au 0787 113 542

 

By Jamhuri