Kiongozi mwingine wa tatu wa dini ambaye ni vizuri kumsoma katika falsafa na kauli zake mbele ya Mwenyezi Mungu, ni Mwenyekiti Kamara Kasupa.

Mwinjilisti Kamara Kasupa katika gazeti moja, toleo Na. 520 la tarehe 16-20/10/2012, anauelezea udini kuwa ni “Ubaguzi unaoendeshwa katika misingi ya kidini, una kawaida nyingine mbaya, nayo ni ubinafsi wa kubinafsishwa katika misingi ya kidini, una kawaida nyingine mbaya nayo ni ubinafsi wa kubinafsisha kila kitu.”

 

Mwinjilisti Kasupa anabainisha maelezo hayo kwa kusema, “Dhana ya kundi hili ni kwamba Watanzania wengine si muhimu sana kustahili kutendewa haki hata wakidhulumiwa kwa kuwa si Waislamu, basi acha wadhulumiwe.”

 

Kiongozi wa nne wa dini ambaye ni vizuri tumsome ni Naibu Katibu wa Umoja wa Wanazuoni nchini, Sheikh Mohamed Issa. Aprili 24, 2012, alitoa hotuba iliyohusu siasa na dini, na katiba kwa Waumini wa Kiislamu kwenye Msikiti wa Khaq, mjini Morogoro.

 

Sheikh Issa alisema udini ni kupendelea dini yako kiasi cha kuwadhulumu watu wa dini nyingine, na bila kujali taratibu. Huo ndiyo udini.

 

Aliendelea, “Udini si wewe kujihusisha na dini yako. Kujihusisha na dini yako kila mtu anatakiwa. Lakini udini ni kupendelea dini yako na kuwadhibiti watu wa dini nyingine wasije wakapata mafao, mafanikio na maendeleo kama ya dini yako. Huo ndiyo udini.”

 

Kutokana na masomo yote hayo manne ya viongozi wa dini, unapata picha kuwa udini ni dhuluma, ubinafsi na upendeleo dhidi ya haki, ambayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa aliowaumba.

 

Iwapo umekuwa ukifuatilia mada hii ya udini, utaweza kukumbuka au kufahamu sababu, chanzo na maana ya udini tunaouzungumzia leo, udini ambao uliletwa na wakoloni wakiwa na malengo ya kuwafarakanisha Waafrika.

 

Nirudie kusema kwamba mtu mdini ni yule mwenye kuipenda dini yake sana, kufuata taratibu za dini yake sana na kufanya matendo ya ubinafsi, upendeleo na dhuluma.

 

Nasisitiza kwamba mtu kuwa mdini si kosa, ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa mtu yeyote. Mtu kuwa na udini ni kosa, ndiko kunako lalamikiwa. Matokeo ya udini ni chuki, mfarakano na hata kutokea ugomvi na mauaji.

 

Nadhubutu kusema kihistoria; palikuwapo na wamisionari hapa nchini. Wamisionari ninaoongelea hapa ni wale wote walioleta na kuendesha dini za kigeni. (Uislamu na Ukristo). Wamisionari wanaofahamika sana ni wale wa madhehebu ya dini ya Kikristo kutoka Ulaya.

 

Malalamiko yanayotolewa na Watanzania yanabeba dhana mbili. Ya kwanza ni mfumo Kristo au mfumo Katoliki, mfumo ambao unalalamikiwa na kambi ya pili (Waislamu).

 

Dhana ya pili ni mfumo wa mihadhara ya Kiislamu au kashfa dhidi ya dini nyingine. Mfumo huo unalalamikiwa na kambi ya kwanza (Wakristo). Hebu tuangalie mfumo mmoja mmoja ili kujiridhisha ni kweli mfumo mmoja unaonea mfumo mwingine?


MFUMO KRISTO

Ni sahihi kuwa taasisi za madhehebu zilikuwa ni chombo muhimu sana cha kufanikisha siasa ya wakoloni na malengo yao mbalimbali. Madhehebu ya Kikristo ndiyo yaliyoingiza na kuendesha elimu ya siasa nchini. Shule zilifunguliwa katika sehemu ambako wamisionari waliweka vituo vyao au karibu na makanisa, ambayo yalijengwa karibu na Ikulu za machifu au wajumbe.

 

Elimu iliyotolewa ilitarajiwa kuwapa waumini wa Kikristo ujuzi wa kusoma, kuandika na kuhesabu. Shabaha kuu ya elimu hii ilikuwa kuwapa waumini wenye uwezo wa kusoma na kukariri maandishi ya Injili na Bibilia.

 

Pili, wamisionari walihitaji baadhi ya wanafunzi wao kuwasaidia katika kazi za ofisini kama makarani, watunza bustani, wachuuzi madukani na hasa walimu wa dini. Walimu hao walikuwa na kazi za kuzalisha, kusimamia fujo kanisani na kuwaandaa waumini katika sehemu ambazo wamisionari wenyewe waliogopa kufika.

 

Elimu hiyo pia ilikuwa ni chombo cha kunasia roho, fikira na nguvu za jamii mbalimbali za Kiafrika na watoto wa waumini wa madhehebu yaliyohusika tu, waliweza kuruhusiwa kuandikishwa kama wanafunzi shuleni.

 

Watoto wa waumini wa madhehebu mengine waliweza kupokelewa kwa masharti maalumu. Walipaswa kuahidi kubadili madhehebu yao na kuwa waumini wa madhehebu yaliyoendesha shule husika. Hali hii iliendelea hadi Uhuru.

 

Itaendelea

 

0717 113542 au 0787 113542

By Jamhuri