Katika toleo la leo tumechapisha taarifa zenye kuonyesha kuwa hali ya kifedha ya Balozi za Tanzania nje ya nchi ni mbaya. Habari hizi zinaonyesha kuwa Balozi karibu zote zinakabiliwa na madeni, zimekatiwa huduma za simu, maji, umeme na mifumo ya kupoza hewa imechakaa. Ubalozi kama wa Urusi, tumechapisha taarifa za kusikitisha.

 

Kwamba dongo la kwenye paa lenye uzito wa karibu tani moja limeangukia kwenye ofisi ya Balozi wa Tanzania nchini Urusi na kwamba hadi sasa nondo zimejitokeza nje. Lakini pia tumechapisha taarifa za nyumba zilizoko hoi zinazovuja kwenye Balozi za Beijing – China, London – Uingereza, Washington – Marekani na kwingineko.

 

Pia yapo maombi ya kununua nyumba katika Balozi za New York, Moscow, Johannesburg na kwingineko. Imeelezwa kuwa mabalozi wetu wanaendesha magari mikweche, ilihali hapa nchini hadi wakuu wa idara tu, wanaendesha magari yenye thamani kubwa na ya kisasa. Kuna upungufu wa watumishi kwenye Balozi unaohatarisha utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi (2004).

 

Ubalozi kama wa Ufaransa ni aibu tupu. Kwamba gharama ya pango kwa mwaka ni karibu Sh milioni 720 wakati ipo fursa ya kununua nyumba ya wastani wa Sh bilioni 1.2 ikafanya kazi hii. Si hilo tu, Tanzania inatumia anwani ya posta ya Uganda kufanya mawasiliano yake yote ya kibalozi. Tumeshindwa hata anwani? Lipo jengo tuliloahidiwa kuuziwa na New Zealand, lakini kwa bahati mbaya hatujibu maombi yao.

 

Mbaya zaidi hata watumishi kwenye Ubalozi wetu wa Ufaransa wengine si Watanzania. Mkalimani ni Mkenya. Huko Washington kuna nyumba ya Serikali inayosubiri kupangishwa itoe kodi ya dola 400,000 lakini kilichokwamisha ni Serikali kutoa ruhusa tu. Imeripotiwa kuwa Msumbiji gari aina ya Town Hiace inayotumiwa na ubalozi inazimika barabarani na kuwashwa kwa kusukumwa.

 

Waziri wa Mambo ya Nje katika bajeti ya mwaka huu, ameeleza kuwa bajeti iliyopita amepata wastani wa asilimia 44 tu ya fedha alizoidhinishiwa bungeni. Membe analalamikia pia utaratibu unaotumika wa kulipisha wageni viza wakati wameishafika kwenye viwanja vya ndege hapa nchini. Anasema mbali na kulikosesha mapato taifa, ni hatari kwa usalama wa nchi.

 

Kwa nchi kama Italia na Ujerumani, imeelezwa wapo mabalozi wa heshima wanaotoza viza bila kutumia stika, badala yake wanagonga mihuri na hivyo kuikosesha Serikali mapato makubwa. Malalamiko ni mengi yanayohitaji ufumbuzi wa haraka. Kubwa likiwa ni la kuboresha mawasiliano wizarani kwa kujibu hoja za mabalozi walioko nje ya nchi.

 

Alichokisema Membe, kuwa wizara yake imepewa asilimia 44 tu ya bajeti iliyotengewa kinatisha. Inawezekana tatizo la namna hii lipo katika kila wizara, hivyo mambo mengi yamesimama hapa nchini. Tunasema si busara kwa mabalozi wetu kuendelea kuhangaika ughaibuni. Katika hili tunasema Serikali itimize wajibu wake kuliepushia taifa letu aibu hii. Mabalozi watumiwe fedha za kutosha.

 

 

By Jamhuri