Habari kuu tuliyoichapisha katika toleo la leo inahusu mgogoro kati ya wazazi na wamiliki wa shule za Al-Muntazir. Shule hizi ambazo ni za awali, msingi na sekondari zinamilikiwa na Khoja Shia Ithnasheri Jamaat ya Dar es Salaam. Shule hizi zimejiwekea utaratibu wa kuongeza ada bila kufuata mwongozo unaotolewa na Serikali.

JAMHURI, limezungumza na wazazi zaidi ya 50 wenye kupinga utaratibu huu wa uongozi wa shule kuamka asubuhi ukaongeza ada utakavyo. Wazazi hawa wamefuata ngazi zote kutoka uongozi wa wilaya, kwa Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na Ikulu kwa Katibu Mkuu Kiongozi, bila kupata ufumbuzi.

Malalamiko ya wazazi hawa, yamekuwa ni kupinga ongezeko la ada lisilotabirika, kutozwa faini ya Sh 100,000 kila ada inapochelewa siku saba na kutoa mafundisho kwenye mitaala yanayokinzania na maadili ya kiimani na Kitanzania. Ada ya mwaka huu wameipandisha hadi Sh 2,480,000 kutoka Sh 1,980,000 ya mwaka jana.

Wizara imewaandikia barua wamiliki wa shule hizi kuzuia ongezeko la ada kwa mwaka 2016, utozaji wa faini na mitaala inayokiuka maadili, lakini wazazi wanasema uongozi umeendelea kukaidi. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, badala ya kuwasaidia wazazi hawa, anatumia nafasi yake kuwamwagia matusi na kudai wana kiherehere.

Makonda anasema wazazi hawajafuata ngazi stahiki, wakati uhalisia wamefuata kila ngazi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imeshiriki kuwaonya wamiliki wa shule hizi. Tumefarijika kuona Waziri mwenye dhamana na suala la Elimu, Prof. Ndalichako ameahidi kuwa ataunda Timu ya Wataalam kwenda kuchunguza mgogoro huu.

Kilichotushtua sisi ni ugumu wa mioyo ya wamiliki wa shule hizi. Ukiangalia idadi ya mawasiliano kati ya Serikali na shule hizi, kama wamiliki hawaoni kuwa Serikali ‘wameiweka mfukoni’ wasingethubutu kuendelea kutenda hayo watendayo. Tunaamini Waziri Prof. Ndalichako amefanya vyema kutosikiliza ushauri wa Makonda na kuamua kwenda kuwasikiliza wazazi hawa.

Sisi tumeshtushwa mno na tukio kwamba hata mitaala ya shule hii inapingana na maadili ya imani na Kitanzania. Tunaiomba Serikali kuwa hiyo timu itakayoundwa isiishie kwa shule za Al-Muntazir pekee. Tatizo la shule binafsi kuongeza ada kwa ukaidi wa ajabu lipo nchi nzima.

Tunapata hofu kubwa zaidi kuwa kama wamiliki wa shule hizi hawakaguliwi, huenda baadhi ya mafundisho wanayotoa ni hatari kwa ustawi wa taifa hili. Tunasisitiza wigo wa uchunguzi utanuliwe, na wanaokwenda kinyume wadhibitiwe. Mungu ibariki Tanzania.

2241 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!