Wiki iliyopita Rais John Pombe Magufuli, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM ametoa ahadi nzito kuwa atahakikisha Serikali inahamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho.

Kwa mara ya kwanza Serikali ilitangaza nia ya kuhamishia makao makuu yake Dodoma mwaka 1973. Hii ina  maana hadi mwaka huu imepita miaka 43 bila uamuzi huu kutekelezwa.

Nchi mbili za Afrika zilifanya azimio kama hili na zikalitekeleza mara moja. Nigeria, ilihamisha makao makuu yake kutoka Lagos kwenda Abuja Desemba 12, Mwaka 1991.

Nchi jirani ya Malawi, Mwaka 1975 walihamisha makao makuu yao kutoka Blantyre kwenda Lilongwe. Rais wa wakati huo kwao alikuwa Dk. Hastings Kamuzu Banda. Naye alitolea tamko hili kwenye mkutano wa Chama chake.

Hoja zilizotolewa kuhamisha makao makuu kutoka Blantyre kwenda Lilongwe na Lagos kwenda Abuja, ni mikoa husika kuwa katikati ya nchi na hivyo kurahisisha huduma kwa wananchi wao wanapotaka kwenda makao makuu ya nchi.

Hoja kama hiyo ndiyo ilikuwa msingi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuamua makao makuu yahamishwe kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma Mwaka 1973.

Dodoma ni katikati mwa Tanzania. Hadi sasa muhimili   uliohamia Dodoma ni Bunge. Utawala (Serikali) imekwamia Dar es Salaam. Hata hivyo, bado Bunge nalo lina ofisi ndogo Dar es Salaam inayoendeshwa kwa gharama kubwa kutokana na Serikali wanayoishauri na kuisimamia kuendelea kuwa Dar es Salaam.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alijaribu kutekeleza uamuzi huu kwa kuhamishia Dodoma Wizara ya Kilimo, Ushirika na Chakula, ila baada ya muda kimya kimya hii Wizara nayo ikarejea Dar es Salaam.

Ukiacha kigezo cha kuwa katikati ya nchi, Serikali inatumia gharama kubwa kuendesha ofisi mbili mbili karibu kwa kila Idara.

Tunaamini uamuzi uliofikiwa na Rais Magufuli utasaidia kupunguza gharama za kuendesha Serikali na miundombinu ya nchi hii itajengwa kwa uhakika zaidi kwani viongozi watakuwa kwenye kitovu cha nchi na hivyo kuwarahisishia kazi ya kuwafikia wananchi.

Tunasema hongera Rais Magufuli kwa uamuzi huu na tunaamini zamu hii utafanya utekelezaji wa uamuzi huu kwa vitendo. Mungu ibariki Tanzania.

1759 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!