Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha magonjwa ya mifupa (MOI) kinatarajia kufungua maabara kubwa ya kisasa kwa ajili ya upasuaji wa mishipa ya ubongo.

Kitaalamu maabara hiyo inafahamika kama ANGIO-SUITE, itakayogharimu Sh bilioni 7.9.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Respicious Boniface, amesema kuwa wanatarajia kufungua maabara hiyo kubwa na ya kisasa hapa nchini.

Gharama za kulipia mashine hiyo tayari zimeshalipwa na serikali na wanatarajia mwishoni mwa mwaka huu mtambo huo utakuwa tayari kufanya kazi.

Boniface amefafanua kuwa gharama hizo ni pamoja na ujenzi wa chumba maalumu cha kuhifadhia mtambo huo na vifaa vyake.

Kujengwa kwa mashine hiyo kutasaidia kuondoa kabisa rufaa za wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 98 kutokana na  shida za vichwa, migongo na magoti, kwani gharama za hapa nchini zitakuwa zipo chini.

Amesisitiza kuwa ni vema wananchi wakajiunga katika bima ya afya ili iwe rahisi kupata huduma ya afya bila kusuasua na kuondoa mzigo kwa serikali.

Ameongeza kuwa idadi kubwa ya Watanzania ni maskini, hivyo kila wanapokwenda kutibiwa katika hospitali hiyo, wengi wanataka kupewa msamaha, hivyo serikali kuingia gharama kubwa kuwalipia.

Amesema gharama za kuendesha hospitali ni kubwa na inategemea michango ya watu wanaotibiwa binafsi na wale wenye bima ya afya, kwa hiyo ingekuwa vema wananchi wangejiunga huko ili kupunguza mzigo kwa serikali.

Amesema hospitali hiyo inatumia gharama kubwa sana kununua vifaa wanavyotumia kwa ajili ya wagonjwa. Alitolea mfano wa kifaa cha kubadilishia nyonga ni Sh milioni 6.5 na ukichanganya na gharama zingine, inafika Sh milioni 10 hadi 11.

Mkurugenzi huyo ameipongeza serikali kwa kutekeleza ahadi yake kwa wakati. Amesema serikali imeendelea kuboresha vifaa tiba katika hospitali hiyo.

Amesema kuwa kutokana na ubora wa vifaa, hospitali hiyo (MOI) ilimpokea Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Juda Thadaeus Ruwa’ichi na kumfanyia tiba kutokana na miundombinu mizuri ya hospitali hiyo.

Dk. Boniface amesema kwamba serikali itakuwa imeokoa pesa nyingi kutokana na matibabu ya wagonjwa.  Amebainisha kuwa mgonjwa wa kichwa anahitajika kutoa Sh milioni 10 akihudumiwa hapa nchini na akifanyiwa nje ya nchi atahitajika kulipa kiasi cha Sh milioni 60.

Mgonjwa wa goti matibabu yake hapa nchini ni Sh milioni 9, huduma kama hiyo nje ya nchi ni Sh milioni 40.

Aidha, amesema mgonjwa wa upasuaji wa nyonga atalazimika kulipa Sh milioni 12  hapa nchini na Sh milioni 40 kama atapata huduma hiyo nje ya nchi.

Amesema kutakuwa na unafuu katika matumizi ya serikali kutibu wagonjwa nje ya nchi, kwani ilikuwa ikitoa fedha nyingi.

By Jamhuri