Kesi inayomkabili mfanyabiashara, Khamis Said, maarufu Meshack (38), anayetuhumiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani, imepigwa tarehe hadi Oktoba 7, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa upelelezi. 

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon, amemweleza Hakimu Mkazi, Salum Ally, mbele ya mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo upo hatua za mwisho kukamilika.

 Wakili Wakyo ameomba shauri hilo liahirishwe hadi Oktoba 7, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, huku upelelezi ukiendelea.

Mshitakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kumuua mkewe, kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kuchukua majivu ya marehemu kwenda kuyafukia shambani mwake.

Meshack mara kadhaa amekuwa akifanya matukio ya ajabu mahakamani, ikiwano  kuomba simu yake ambayo anadai ina pesa za matumizi ya nyumbani kwake pamoja na ada ya mwanaye.

Aidha, amekuwa akificha sura yake kwa kujifunga kitambaa usoni ili asipigwe picha na wanahabari.

Mwanzoni mwa kesi hiyo aliwatishia waandishi wa habari kwamba angewafanyia kitu kibaya. Hata hivyo kipindi hiki ameonekama kuwa mtulivu anaposimamishwa kizimbani.

By Jamhuri