Serikali yapongeza Tabora Marathon

Serikali mkoani Tabora imepongeza mashindano ya Tabora Marathon kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, na kuwa itakuwa bega kwa bega katika mashindano yajayo ya mwaka 2014.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Suleiman Kumchaya, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Fatma Mwassa, alitoa pongezi hizo kwenye kilele cha mbio hizo zilizomalizikia kwenye viwanja vya taasisi mjini hapa.

 

Kumchaya alisema amefarijika kuona vijana, wazee na watoto wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo. Hata hivyo, aliwashauri washiriki wote kuunda vikundi kwenye maeneo yao ili wanapopata muda wanafanya mazoezi ya riadha na hata mashindano yatakapokuja mwakani wanakuwa fiti kimwili.

 

Kumchaya aliwaasa viongozi wa Riadha Mkoa wa Tabora, (RITAM ) kwa kushirikiana na Kamati ya Tabora Marathon, kuanza maandalizi ya mbio za 2014, na baada ya kikao cha tathmini wahakikishe wanakutana naye ofisini kwake kuweka mambo sawa kwa mbio zijazo.

 

Katika hatua nyingine serikali imewapongeza wadau waliojitokeza katika michango yao, kuwa serikali itaandaa barua za kuwatambua wote kama shukrani kwao.

 

Wafadhili waliochangia kufanikisha mbio hizo ni Kampuni ya Mawsiliano  ya Vodacom Tanzania; Filbert Bayi Foundation; mwanariadha wa kike, Banuelia Brighton; Meneja Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Kanda ya Magharibi, Emmanuel Aidan; Kampuni ya Tumbaku (ATTT); Mkurugenzi wa Gonalla Phamacy, Godbless Mafole; Shirika la Posta; Benki ya NMB; Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Shirika la Nyumba (NHC), MVP na Platnum Credit.

 

Tabora Marathon 2013 ilishirikisha mbio za nusu marathon kilomita 21 kwa wanaume, kilomita 15 kwa wanawake na kilomita 5 kwa watoto na watu wazima.

 

Kwenye mbio za km 21,  Tabu Mwandu aliibuka mshindi wa kwanza kwa kutumia saa 1:10.35. Alizawadiwa kitita cha sh 100,000, kikombe na medali ya dhahabu; wa pili Dickson Mkami saa 1:13.18 na kujipatia sh 70,000 medali ya fedha huku nafasi ya tatu ikienda kwa Francis Jombe aliyetumia saa 1:14.36 na kuzawadiwa sh 60,000 na medali ya shaba.

 

Aidha, kilomita 15 wanawake, Grace Jackson alishinda akitumia dakika 55:33.06 na kuzawadiwa sh 100,000, medali ya dhahabu na kikombe; wa pili Maombi Elisha dakika 58:52.01 na kuzawadiwa sh 70,000 na medali ya fedha huku nafasi ya tatu ikienda kwa Naomi Samwel aliyetumia saa 1:00.05 aliyejipata sh 60,000 na medali ya shaba.

 

Washindi wa nne na tano kila upande walizawadiwa sh 20,000 kila mmoja huku wa sita hadi wa kumi wakijipatia sh 15,000 kila mmoja.

 

Kwa kilomita 5 wanaume, wa kwanza aliibuka Robert Mayala, wa pili ni Joseph Kimatile na kufuatiwa na Rashid Malugu waliopata medali za dhahabu, fedha na shaba.

 

Upande wa wanawake kilomita tano ni Getruda Musa, wa pili Sara Lyimo na Asha Seleman ambao nao walipata medali, huku mkimbiaji mwenye umri mkubwa Msese Said (65) akipata fedha sh 17,000 kutoka kwa akiwamo DC Kumchaya.