Serikali imesema inachunguza taarifa za meli yenye bendera ya Tanzania iliyokamatwa nchini ugiriki ikiwa na vifaa vya kutengenezea vilipuzi ambavyo vilikuwa vikisafirishwa kwenda Libya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Susan kolimba alisema kuwa wanafuatilia kwa kina jambo hilo ili kupata ukweli wake.

“Kwa sasa ni kwamba jambo hilo tunalifuatilia ili kujua habari hizo kama zina ukweli na tutakapopata taarifa tutawajulisha, bado tunafuatilia,” alisema Dkt Kolimba.

Kauli hii imekuja kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa maofisa wa Ugiriki wanaofanya doria baharini wameizuia meli hiyo iliyokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania ikiwa imebeba vifaa vya kutengenezea vilipuzi, vilivyokuwa vikipelekwa nchini Libya jambo ambalo ni kinyume na sheria iliyowekwa ya kutosafirisha silaha kwenda Libya.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, maofisa hao wameeleza kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba kreti 29 zilizojaavifaa pamoja na kemikali zinazotumiwa kuunda vilipuzi.

Wizara ya Safari za Baharini ilisema meli hiyo ilisimamishwa ikiwa katika kisiwa cha Crete kusini mwa Ugiriki baada ya maofisa kupatiwa taarifa na ilisindikizwa hadi katika bandari ya kisiwa hicho na kufanyiwa ukaguzi.

Ilielezwa zaidi katika ripoti hiyo kuwa nahodha wa meli hiyo ambaye alifahamika kwa jina moja la Andromeda, alidai meli hiyo ilikuwa inasafiri kuelekea Djibouti lakini baadaye ikabainika kwamba ilikuwa inasafiri kuelekea mji wa bandarini wa Misrata nchini Libya.

Mabaharia wanane ambao ni raia wa India, Ukraine na Albania waliokuwa kwenye meli hiyo, walitarajiwa kufikishwa mbele ya mwendesha mashtaka jana.

 

By Jamhuri