Na Deodatus Balile

Baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha habari za ubovu wa matrekta ya URSUS yanayouzwa kwa wakulima nchini kutoka Poland, Bunge limeibana serikali, ambayo nayo imezinduka na kuchukua hatua, JAMHURI linathibitisha.

Kampuni ya URSUS S. A. iliingia mkataba na Shirika la SUMA JKT siku nane kabla ya uchaguzi mkuu, yaani Oktoba 22, 2015 kwa nia ya kuzalisha na kuuza matrekta 2,400 kwa wakulima nchini Tanzania. URSUS S. A. ilianza kuleta nchini matrekta mwaka 2017, ambapo hadi sasa imekwisha kuingiza nchini matrekta 825, ambayo kwa asilimia kubwa yamebainika kuwa mabovu.

Matrekta yaliyoingizwa nchini kwa ujumla wake katika ripoti mbalimbali yamebainika kuwa na ubovu wa aina 20. Kati ya aina hizo za ubovu, aina 5 zinaonekana kuwa kila trekta lina ubovu huo, ambao ni betri mbovu, tairi za mbele kupata pancha, rimu za mbele kuvunjika, mfumo wa umeme dhaifu na mkao wa jembe la kulimia hauko sawa. Baadhi ya wakulima wamekataa kulipa mkopo wao katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa maelezo kuwa matrekta waliyokopeshwa fedha kununua ni mabovu.

Mkataba kati ya URSUS S. A. na SUMA JKT, Agosti 9, mwaka 2016 ulihamishiwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), ambao wamepokea matrekta hayo 825 na kuuza karibu matrekta 500 kwa wakulima.

Wakulima wengi wamelalamika kuwa matrekta hayo yanawasumbua kwa kiwango cha mengine kuvunjika kifua wakati yanalima na hayana vipuri (spare). Hii imethibitishwa na hatua ya NDC kusambaratisha matrekta 26 kwa nia ya kupata vipuri kwa matrekta mabovu.

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), chenye makao yake makuu jijini Arusha, ambacho kina wataalamu waliobobea katika zana za kilimo, kilichopewa jukumu la kuchunguza ubora wa matrekta ya URSUS kabla ya kuyauza kwa wakulima, sasa kimekiri kuwa matrekta hayo yana upungufu mkubwa.

Pamoja na upungufu huo, Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, ameliambia JAMHURI hivi karibuni kuwa serikali imekwishalipa asilimia 60 ya gharama za matrekta hayo, sawa na dola 33,000,000 kati ya dola milioni 55 za mkataba huo.

Fedha hizi zinatokana na mkopo wa masharti nafuu kwa Tanzania kutoka Poland kwa mkataba wa Septemba 28, 2015. Mkopo wote ni dola milioni 110, unaopaswa kulipwa ndani ya miaka 30, baada ya kipindi cha mpito cha miaka 5.

Bunge laibana Serikali

Baada ya Gazeti hili la JAMHURI kuchapisha habari hizi za uchunguzi na kuanika upungufu wa mkataba na ubovu wa matrekta haya ya URSUS, wiki mbili zilizopita Bunge liliwafukuza maofisa wa NDC waliofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara kueleza maendeleo ya mradi, na likataka kukutana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu, Prof. Joseph Buchweishaija na maofisa wengine waandamizi.

Jumatatu Agosti 26, 2019 Kamati ya Bunge chini ya uenyekiti wa Murad Saddiq, iliwabana mbavu waziri na katibu mkuu ambao waliliomba Bunge lisiunde Kamati Teule kuchunguza suala hili, badala yake waikabidhi mikononi mwa serikali hoja hiyo waishughulikie kwa masilahi mapana ya wakulima na maendeleo ya kilimo cha Tanzania kama ilivyokuwa nia ya msingi.

Bunge na serikali walikubaliana kimsingi kuwa matrekta hayo yana upunguvu mkubwa, ambao uliainishwa ubovu upatao aina 20 katika matrekta ya URSUS, suala ambalo wote walikubaliana kuwa linamdidimiza mkulima badala ya kumkomboa. Bunge kupitia kamati, liliridhia ombi la serikali ambayo nayo haikulaza damu ikaanza kulifanyia kazi suala hili mara moja.

 

Serikali yakutana na Balozi wa Poland

Baada ya kuwekwa kitimoto na Bunge, haraka haraka Jumanne Wizara ya Viwanda na Biashara ilimwandikia Balozi wa Poland nchini, Krzysztof Buzalski na kutaka kukutana naye kujadili ubovu wa matrekta ya URSUS, pamoja na hali ya mkataba.

Kikao kimefanyika ofisi za NDC jijini Dar es Salaam, siku ya Alhamisi, Agosti 29, ambapo serikali imemweleza Balozi Buzalski kutoridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa makubaliano yaliyomo ndani ya mkataba na suala la ubovu wa matrekta ya URSUS.

“Kwa kweli Waziri Bashungwa na Katibu Mkuu, Prof. Buchweishaija wamewasilisha kwa umahiri mkubwa hoja kuwa kiwanda cha kuunganisha matrekta kilipaswa kukamilika Juni, mwaka 2018 hadi sasa bado hakijakamilika. Matrekta betri ni mbovu, mfumo wa umeme ni dhaifu, tairi zinapata pancha, malipo yameishafanyika asilimia 60, URSUS wamewekwa chini ya mufilisi, matrekta hayana waranti, yaani kwa kweli walieleza kila kitu.

“Balozi aliwasilikiza kwa umakini mkubwa, na baada ya maelezo yao akasema ‘suala la waranti atahakikisha linarejeshwa kwa matrekta yote, ubovu uliopo utarekebishwa’ na akakubali hoja iliyotolewa na serikali kuwa matrekta 1,575 yaliyosalia yasiletwe nchini hadi yakaguliwe ubora wake yakiwa huko huko Poland.

“Balozi aliomba akabidhiwe orodha ya kila ubovu katika matrekta hayo na atahakikisha yanarekebishwa kwa nia ya kumwinua mkulima wa Tanzania, ambalo ndilo lilikuwa lengo la msingi la kuingiwa kwa mkataba huo,” kimesema chanzo chetu.

Waziri Bashungwa alipotafutwa na JAMHURI kuzungumzia kikao hicho, alimshukuru Mungu kwa kupata fursa ya kutetea masilahi ya nchi na hakutaka kuingia katika undani wa mazungumzo hayo.

Kwa upande wake, Prof. Buchweishajia, ameliambia JAMHURI: “Kwa kweli mmekwishatuonyesha tatizo lilipo. Sasa tunaomba mtupe nafasi tulifanyie kazi. Inachukua muda kupitia mikataba yote, kuangalia kama taratibu zimefuatwa au la, na nimeielekeza timu ya wanasheria wetu ilifanyie kazi na baada ya muda tutawafahamisha kinachoendelea.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Gabagambi amelithibitishia JAMHURI uwapo wa kikao hicho, na akaongeza: “Kikao kimoja hakiwezi kumaliza matatizo yote. Hiki kilikuwa kikao cha kwanza, na balozi amesafiri nje ya nchi, amepokea hayo tuliyowasilisha na ameahidi kuyatatua kwa manufaa ya wakulima. Ameahidi akirejea tutafanya kikao kingine na kingine, kurekebisha penye upungufu.”

JAMHURI pia limemuuliza Prof. Gabagambi taarifa kwamba alifanya kikao kizito na wafanyakazi wa NDC, akasimamisha watumishi wawili na baadaye kuwarejesha kazini, akaahidi kutumia vyombo vya dola kusaka wapi mwandishi wa habari hizi anapata taarifa na kwamba yeye akiingia ofisini “anaona au kukuta mambo yasiyo ya kawaida hivyo amekabidhi maisha yake kwa Yesu,” naye akasema: “Kazi ni ngumu, ila Yesu ananilinda. Hayo mengine uliyoambiwa sijafikia huko.”

Sehemu zenye matatizo katika mkataba

Matatizo katika mkataba wa URSUS S. A. na SUMA JKT yalianza mapema kupitia mkataba ulioingiwa Oktoba 22, mwaka 2015 zikiwa ni siku 8 kabla ya Uchaguzi Mkuu. Katika mkataba huo wenye kurasa mbili na vifungu vinne, ukiambatana na masharti ya jumla na masharti mahususi, kifungu cha 2 cha mkataba huo kiliorodhesha mikataba au maandiko manane yanayoambatana na mkataba huo, lakini kati ya hayo hawakuutaja mkataba mama, ambao ni mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Poland.

Kifungu cha 4 cha Masharti ya Jumla ya Mkataba (GCC), kimeweka mtego unaojidhihirisha kuwa kuna nia ovu au kutoaminiana kwa kukiuka masharti ya mkataba mama kati ya Tanzania na Poland. Kifungu hiki kinasema sheria za Tanzania ndizo zitatumika, lakini hapo hapo kinasema Masharti Mahususi ya Mkataba (SCC) yatachukua mkondo. Katika kifungu cha 5 cha SCC, mkataba unabadili mwelekeo na kusema ikiwa kuna mgogoro zitatumika sheria za Uingereza, hivyo kesi au usuluhishi sasa utafanyika Uingereza.

Kifungu hiki kinapaswa kuondolewa katika mkataba huu wakati wa majadiliano mapya yatakayofanyika, kwani mkataba mama ulioingiwa na Serikali ya Tanzania na Poland, kifungu cha 12 kinasema: “Tofauti zozote baina ya pande mbili zilizoingia mkataba juu ya tafsiri na utekelezaji wa mkataba huu zinapaswa kumalizwa kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya washirika wa mkataba huu.”

Kifungu cha 8 cha Masharti ya Jumla ya Mkataba nacho kinahitaji kurekebishwa kwani ndicho chimbuko la tatizo. Kifungu hiki kinampa mtengenezaji wa matrekta mamlaka na haki ya kukagua bidhaa zake (matrekta) alizozitengeneza yeye na kujipa cheti cha ubora, kwa kusema: “Mzabuni atapaswa kuwasilisha kwa mnunuzi [Tanzania] cheti cha ukaguzi alichokitoa yeye, ambacho kitapaswa kuambatanishwa na cheti/vyeti vya mtengenezaji kutoa hakikisho kuwa bidhaa (matrekta) zimetengenezwa kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa kwenye mkataba.” “Hii ni ngumu mtengenezaji kujikagua ubora wa bidhaa zake,” kinasema chanzo chetu.

Kifungu cha 10 cha SCC kinachorejea kifungu cha 12(1)(e) cha GCC nacho kinahitaji marekebisho, kwani kinaitaka Tanzania kukagua matrekta na kupeleka ripoti ndani ya siku 7 tangu yanapofika bandarini na baada ya hapo kukitokea ubovu wowote URSUS hawatawajibika. Wataalamu wanasema kwa wingi wa matrekta yanayoagizwa kiuhalisia ni vigumu kuyakagua na kupeleka ripoti ndani ya siku saba, huo ni mtego unaopaswa kuteguliwa.

Kifungu cha 13 cha SCC kinaporejea kifungu cha 17 juu ya waranti ya matrekta ambapo kifungu hiki kinatoa miezi 12 au saa 1,000 za trekta kufanya kazi, na kwamba haya mawili yanapaswa kutokea ndani ya miezi 18 tangu trekta ilipopakiwa melini. Hii ina maana matreka yote yaliyoletwa na URSUS nchini mwaka 2017, hata kama hayajauzwa hayana tena waranti, hivyo mkulima akiharibikiwa kifaa chochote anapaswa kuingia mfukoni na kujigharamia. Hili Balozi Buzalski amesema atahakikisha waranti inarejeshwa.

Suala jingine, ni kuwa malipo yalipaswa kufanyika baada ya miaka 5, tagu mkataba uliposainiwa kwa Prof. Gabagambi kusema Tanzania imekwishalipa asilimia 60 ya malipo, na si kuidhinisha mkopo kutoka Benki ya Gospndarstwa Krojowego ya Poland ambayo ndiyo inayotoa mkopo kwa nia ya Serikali ya Poland, hili nalo ni tatizo.

Mkopo huu ulitakiwa kuanza kulipwa Novemba 15, mwaka 2020, na ulipaswa kulipwa kwa muda wa miezi 60, kwa maana ya kulipa dola milioni 1.84 kila Mei 15 na nyingine dola milioni 1.84 kila Novemba 15 ya kila mwaka hadi ikamilike miaka 30.

Uamuzi wa Balozi wa Poland na Waziri wa Viwanda na Biashara kuamua kukaa kuzungumzia matatizo ya matrekta haya, umetajwa na wadau wa kilimo kuwa wenye manufaa na masilahi mapana kwa wakulima wa Tanzania.

1664 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons