Wakati Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, akifikiri kuongeza idadi ya askari wa usalama barabarani, mamlaka ndani ya Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inao askari hao wa kutosha.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Marison Mwakyoma, anayeshughulika na suala la usalama barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amesema kitengo hicho kwenye eneo lake hakina uhaba wa askari.

ASP Mwakyoma amesema mahitaji ya askari wa usalama barabarani huzingatia shughuli za kiuchumi, usafirishaji pamoja na ongezeko la watu. Ametoa mfano wa ongezeko la viwanda, kwamba watu wengi watakwenda kufanya kazi, hivyo suala la msongamano halitaepukika, hivyo askari wa usalama barabarani kuhitajika zaidi.

“Idara yetu ya Usalama Barabarani haina upungufu wa askari wa usalama barabarani… tunao wengi, na kama kutakuwa na mahitaji, basi yatakuwa ni kidogo sana. Ongezeko la askari wa usalama barabarani hutegemea idara mbalimbali zinavyokua.

“Kuna sekta ambazo zikikua lazima askari waongezwe, kwa mfano sekta ya elimu, usafirshaji, uchumi na viwanda. Kutokana na sekta hizo kukua, hapo suala la kuongeza askari huja,” amesema ASP Mwakyoma.

ASP Mwakyoma amesema kwa kawaida Idara ya Usalama Barabarani ni kubwa, zinapotokea nafasi kwa ajili ya kuongeza askari lazima wachukue wale wenye sifa. Wanapochaguliwa hupelekwa kozi kwa ajili ya kuwaongezea weledi.

Kamanda huyo, mbali na kuthibitisha kwamba Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inao askari wa usalama barabarani wa kutosha, hakuweza kutoa idadi yake.

“Askari huchaguliwa kwa sifa zake, wengine huchukuliwa kutoka kambini na wanapopata nafasi hizo tunawapeleka kozi ili wakapate weledi, kwa sasa askari wa usalama barabarani ni wengi japo idadi yao siifahamu,” amesema ASP Mwakyoma.

ASP Mwakyoma ameliambia JAMHURI kwamba katika Idara ya Usalama Barabarani wanapambana na changamoto kadhaa, hivyo kulazimika kuanza kutoa elimu kwa askari kuhusu huduma kwa wateja, uvumilivu, lugha nzuri na kutoa elimu kabla ya kumkamata mtuhumiwa.

Amesema kwa sasa Idara ya Usalama Barabarani imeandaa kampeni ya kuzuia na kupambana na rushwa, askari wanapelekwa mafunzoni ili wakapate weledi jinsi ya kujilinda na changamoto za rushwa kazini.

Hata hivyo amesema askari wa usalama barabarani wamekuwa wakitoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abiria wa masafa marefu.

“Dereva anapoendesha gari ana tabia ya kujisahau, ndiyo maana serikali imeyafungia magari vinasa mwendo ili kuhakikisha wanawadhibiti madereva wanaovunja sheria,” amesema. 

By Jamhuri