Mada ya Mzee Zuzu wa Kijiji Kipatimo juu ya:

“Kuhamia Dodoma itawezekana kwa siasa zetu?”

Naandika kuhusu maoni yako uliyotoa katika Gazeti la Jamhuri (Augusti 2 – 8, 2016).

Umesema kwamba unakubaliana na dhana ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Kuu, Dodoma kutokana na sababu ya ‘kusogeza huduma karibu na wananchi’.

Dhana unayotumia si sahihi na ni ya upotoshaji na iliyo kinyume kabisa cha maelekezo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni vigumu sana kueleza jinsi gani Mkurya wa Rorya au Mmakua wa Newala au Muha wa Kigoma, Msegeju wa Tanga au Msukuma wa Bariadi atakavyosogezewa huduma karibu na nyumbani kwake pale tutakapohamishia makao makuu ya Serikali Kuu, Dodoma.

Kwa mujibu wa Katiba ya Taifa; vyombo pekee vilivyopewa madaraka ya kusogeza huduma karibu na wananchi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kamwe si Serikali Kuu (Ibara ya 146 (1). Serikali za Mitaa ndizo hutoa kidhati kwa wananchi mmoja mmoja na wote kwa ujumla huduma za zahanati, shule za chekechea, shule za msingi na sekondari, ujenzi wa masoko ya magulio vijijini, barabara za vijijini (village extension roads), majosho, huduma za uvuvi na urinaji na nyingine utakazoweza wewe mwenyewe kukumbuka.

Huduma za aina hii kamwe hazitasogezwa karibu na wawanchi kutokana na Serikali Kuu kuhamia Dodoma. Kazi pekee ya msingi ya Serikali Kuu mintarafu Serikali za Mitaa ni kuziwezesha mamlaka za serikali za mitaa kuwa na nguvu ya kisheria (Bye Laws, Regulations) na kifedha kuweza kumudu utoaji wa huduma hizo za msingi. Kwa sababu hiyo makao makuu ya Serikali Kuu yanaweza kuwa Mbozi, Tarime, Tabora, Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Moshi au Magu. Iwe popote pale ilipo Serikali Kuu itatunga kutoka huko sheria-rafiki kwa manufaa ya mamlaka za Serikali za Mitaa au kutoa RUZUKU wezeshaji kwa vyombo hivyo ili viweze kufanikisha na kumudu kazi zao.

Serikali Kuu ni chombo wezeshaji- siyo chenyewe kutoa huduma moja kwa moja kwa wananchi, isipokuwa huendesha miradi mikubwa mikubwa ya huduma za kitaifa.

Serikali Kuu ina jukumu kuu la msingi kuziendeshea mafunzo mamlaka za Serikali za Mitaa jinsi ya kutoa huduma zao kistahilivu. Hivyo, Serikali Kuu ni Mkufunzi na Mwalimu Mkuu wa kuzielekeza mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya kazi zao ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

Jukumu la pili la Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa ni kuziwezesha kifedha (ruzuku na majaliwa) na kuzitungia sheria – wezeshaji zinazostahili. Iwapo sasa tutaituma Serikali Kuu kwenda kufanya shughuli za kusogeza huduma kwa wananchi ni sawia na kuwataka walimu wa shule za watoto wetu “kuwafanyia mtihani” wanafunzi wao.

Mwalimu bora ni yule anayetumia muda na maarifa yake yote kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi wake. Walakini mwalimu anayewafanyia mtihani wanafunzi wake ni mwalimu mdanganyifu atakayetokomeza taifa zima kusikojulikana kwa kuwa atasababisha kuzalisha wanafunzi vilaka wafaulu mtihani wasiouweza.

Kushindwa kwa Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao ni sawia na kushindwa kwa “mkufunzi” kufundisha “wanafunzii” wake misingi stahiliki.

Jambo tunalotakiwa kufanya ni kwa Serikali Kuu kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzipatia vyanzo vipana vya kodi ya kichwa (mamlaka za wilaya) na kodi ya majengo (mamlaka za mijini) na kuzipatia RUZUKU pana pamoja na majaliwa ya kuendeshea shughuli zao.

Aidha, itatakiwa kutunga sheria – wezeshaji kwa manufaa ya Serikali za Mitaa na si kutunga sheria zinazopoka uwezo wa mamlaka za Serikali za Mitaa kifedha au kiutendaji.

Sababu kuu ya Serikali Kuu kuhamia Dodoma hutokana na uamuzi halali utokanao na ridhaa ya kiuendeshaji wa Serikali yenyewe pamoja na wanasiasa (Bunge). Na kwa sababu hiyo, Makao Makuu ya Serikali yanaweza kuchaguliwa kuwa mahali popote pale ndani ya mipaka ya nchi kadri itakavyoamuriwa na Serikali yenyewe pamoja na wanasiasa. Kwa mfano Wajerumani walichagua Tabora kuwa makao makuu yao wakati wa enzi yao. Baadaye walijaribu Bagamoyo, lakini hatimaye wakachagua Dar es Salaam mahali ambako Serikali ya wazalendo iliridhia kuendelea kupatumia kama makao makuu yake.

Ridhaa hiyo isichanganywe na dhana ya kupeleka huduma karibu na wananchi. Wananchi wako Mpanda, Mtwara, Tarime, Kigoma, Mafia, Mbozi, Mbulu, Simiyu, Tandahimba, Malindi, Chunya na penginepo.

Maeneo haya yote yako mbali na Dodoma. Hata tu pale Dodoma Wagogo waishio kuzunguka manispaa hiyo kama vile Zanka, Mundemu, Kigwe, Bihawana, Mwitikira, Mvumi, Fufu, Handali, Hombolo na penginepo kamwe hawatapatiwa huduma moja kwa moja kutoka Wizara za Makao Makuu ya Serikali, bali watawasilisha kero zao kwa Halmashauri za Wilaya ya Dodoma au ya Chilonwa pamoja na Manispaa ya Dodoma.

Kwa sababu hiyo inatakiwa kwamba sera zetu zielekeze pekee kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa ili “Zidumu na Kuimarishwa” ama kwa njia ya kutunga sheria-rafiki, kuzipatia vyanzo-vipana vya mapato yao ya ndani au kuzirudufishia RUZUKU na MAJALIWA itakayotumika kuzipatia halmashauri hizo mafunzo stahiliki.

Ni kwa njia hizo kwamba zitaweza kufanikisha utekelezaji wa jukumu lao la msingi la kupambana na umaskini na hivyo kupeleka huduma karibu na nyumbani kwa mwananchi mmoja mmoja na wote kwa ujumla ili kukuza maendeleo yao haraka kadri inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria za Serikali za Mitaa mwaka 1982.

Zidumu na Kuimarishwa Serikali za Mitaa!

 

Mwandishi wa makala hii, J. C. Kilembe ni mtumishi mstaafu wa Serikali za Mitaa. Anapatikana kupitia barua pepe: jckilembe@gmail.co

Simu: 0685214691.

973 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!