Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi Yaja

Serikali ipo katika mchakato wa kuwashirikisha wadau ili kufikia azma ya kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kulinda taarifa binafsi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Maria Sesabo, amesema.

Sesabo amesema hayo mjini Dodoma wiki iliyopita, wakati wadau wa mawasiliano wakipewa ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa wizara hiyo, kuhusu mapendekezo ya kutungwa sheria hiyo.

Kwa mujibu wa Sesabo, mchakato wa sheria hiyo itakayotumika Tanzania Bara na Zanzibar, ulianza mwaka 2009 na unatarajiwa kukamilika mwaka ujao.

Baadhi ya taarifa binafsi zinachukuliwa na taasisi za Serikali na za binafsi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo kutengeneza vitambulisho vya Taifa, alama za macho na vidole…zisipohifadhiwa vizuri zinaweza kutumiwa vibaya na wasiokuwa waadilifu,” amesema Sesabo.

Pamoja na wadau kutoa maoni yao kupitia mkutano huo, Sesabo amesema wizara hiyo kupitia kitengo cha Mawasiliano, inaendelea kupokea maoni kwa maandishi, yatakayotumika kuboresha muswada huo.

 

Ushuhuda

Mmoja wa wadau, Modesta Ernest (siyo jina halisi), ametoa ushuhuda kuhusu umuhimu wa kuwapo mifumo mizuri, inayohakikisha usalama wa taarifa binafsi zinazochukuliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Amelieleza JAMHURI kuwa mwaka 2013, watu wasiofahamika walifuta taarifa zake binafsi za kumiliki ardhi kwenye kumbukumbu za kieletroniki za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Amesema alipofika katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Kitengo cha Leseni za Makazi, ikabainika kuwa taarifa zote zinazomhusu hazikuwapo kwenye kumbukumbu za kompyuta, ingawa alikuwa na nyaraka halisi.

Amesema alifuatilia wizarani ambako alifikisha malalamiko yake kwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, anayemtaja kwa jina moja la Dk. Mayunga (wakati huo), ambaye ufuatiliaji wake ulibaini kutokuwapo kwa taarifa zake isipokuwa namba ya kiwanja inayoonesha kuwa eneo husika limeishamilikishwa kwa mtu mwingine.

Baada ya ukaguzi wa nyaraka alizokuwa nazo na kujiridhisha ni mali ya wizara hiyo, zilizotolewa Julai 2006 zikimilikisha ardhi yenye namba iliyosalia kwenye kumbukumbu ya kielektroniki ya wizara, taratibu zikazingatiwa kurejesha taarifa hizo.

Afisa wa Sheria wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Eunice Masigati, amesema sheria ya kulinda taarifa binafsi italinda faragha ya kila mtu.

Amesema faragha ni haki ya kikatiba kwa kadiri inavyoainishwa kwenye ibara ya 16(1) na 16(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na marekebisho yake.

Amesema mapendekezo hayo yanapendekeza kuundwa kwa chombo cha kisheria kitakachoweka utaratibu wa namna taarifa binafsi zinavyotakiwa kupatikana, kuchakatwa, kuhifadhiwa, kusambazwa na kusimamiwa.

 

Kwanini sheria hiyo sasa

Mhandisi Stephen Wangwe kutoka wizara hiyo, amesema ingawa haki ya faragha imekuwapo tangu mwaka 1948, hivi sasa hizi taarifa binafsi zinawekwa kidijitali, hivyo kusababisha ugumu katika udhibiti wake.

Wangwe amesema kuna ongezeka la mbinu za kuingilia taarifa binafsi hususan za kidijitali na hata kubadili lengo la matumizi yake, hivyo kusababisha madhara kwa hadhi na usalama wa wenye taarifa husika.

Taarifa binafsi ni lazima zikusanywe, zichakatwe na zihifadhiwe au kusambazwa kwa mujibu wa sheria na taratibu…mambo ya kuzingatiwa ni pamoja na kupata idhini ya mhusika na taarifa ihusianishwe na mipaka ya mkusanyaji kwa mujibu wa taratibu na sheria,” amesema.

Amesema kwa sasa Tanzania ina Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na Sheria ya Mitandao na kwamba Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi itakapokamilika, itakuwa sheria ya tatu katika eneo hilo.

Kwa kuwa nchi yetu siyo kisiwa kinachojitegemea, na ukizingatia kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano inatumika nchini, ni wakati mwafaka sasa kutunga sheria ya kulinda taarifa binafsi – ndani na nje ya nchi – ili kuzuia matumizi mabaya na kumlinda mhusika wa taarifa,” amesema Mhandisi Wangwe.