Jalada la kesi ya mauji ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, limefungwa.

Uamuzi huu umetolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga. Akwilina aliuawa kwa risasi Februari 16, mwaka huu wakati polisi walipotumia nguvu kuyadhibiti maandamano ya wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wana- Chadema walikuwa wakidai haki ya mawakala wao kupewa viapo kama ilivyofanywa kwa mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa vyama vingine vya siasa.

Nini anakisema DPP Mganga? Anasema amefuta kesi na kuwaachia polisi kwa sababu ‘ameshindwa’ kujua ni nani kati ya hao watuhumiwa aliyerusha risasi iliyomuua Akwilina.

Anasema kwenye maelezo ya kesi, hakuna mahali ambako muuaji ametajwa moja kwa moja! Anasema kwenye maandamano hayo hakuna aliyekaguliwa na kubainika kuwa alibeba silaha yoyote. Akaenda mbali zaidi kwa kusema hakuna mtu aliyewasilisha ushahidi unaomtaja aliyepiga risasi hivyo hata polisi waliokuwa wakizuia maandamano hakuna aliyetajwa kama mtuhumiwa.

Magazeti yamemnukuu Mganga akisema, “Katika maandamano ya watu zaidi ya 2000 unasemaje kama polisi ndio walipiga risasi, kama kuna maandamano ya nguvu polisi hawawezi kushitakiwa kwa mauaji au kesi za madai.”

Mwisho, kwenye maelezo yake, akasema hata mwili wa Akwilina haukuwa na risasi iliyobaki, hivyo ni ngumu kusema ilitoka kwa polisi!

Kabla ya kuendelea, ni vizuri wasomaji tukazingatia jambo moja muhimu- nalo ni kuwa Akwilina hakuwa mshiriki wa maandamano hayo! Hakuwapo kabisa. Haya yametibitishwa na polisi wenyewe kwamba binti huyo kutoka familia maskini hakuwa kwenye maandamano. Alikuwa abiria tu katika basi akienda Bagamoyo kwa shughuli zake za kimasomo. Hili hatuna budi kulitambua na kulikiri kabla ya kuingia kwenye mjadala.

Kwa maneno mengine ni kuwa maskini huyu hakuwa mshiriki wala mtuhumiwa wa kushiriki maandamano ambayo polisi wanasema yalikuwa haramu, lakini aliyesababisha kadhia yote hiyo yupo. Haguswi. Akwilina Alikuwa mpita njia tu.

Naomba Mungu anisamehe, lakini kama kweli kuna haki duniani, basi haya yaliyowapata wazazi wa Akwilina naomba yampate Mganga, halafu atakeyekuwa amekalia kiti cha DPP ampe majibu kama aliyowapa wazazi wa Akwilina! Huhitaji kuwa mwanasheria ndipo upate uchungu kwa majibu mepesi kama haya. Kaka yangu Mganga ni mwanasheria, naomba nimwulize, kesi ya jinai ina ukomo?

Watu wangapi wanaozea jela wakituhumiwa kesi za mauaji? Siungi mkono watu kuumia jela au mahabusu, hoja hapa ni kitu gani kimemfanya afikie hitimisho la haraka ilhali hata mwili wa Akwilina ukiwa bado haujaharibika kaburini?

Ninayo maswali machache kwa DPP. Mosi, anasema amefuta kesi na kuwaachia polisi kwa sababu ‘ameshindwa’ kujua ni nani kati ya hao watuhumiwa aliyerusha risasi iliyomuua Akwilina. Je, kazi ya kujua aliyemuua Akwilina inapaswa ifanywe na mamlaka gani nje ya mfumo wa kisheria? Je, waje wazazi wa Akwilina kumtaja aliyemuua mtoto wao? Vyombo vya sheria vyenye wasomi na wataalamu wa kada zote wanapotangaza kushindwa, wanapeleka salaamu gani kwa wananchi?

Pili, anasema; kwenye maelezo ya kesi, hakuna mahali ambako muuaji ametajwa moja kwa moja! Sawa, tukubali kuwa hatajwi. Je, ni wajibu wa nani kumtaja? Ni wa mfiwa au ni wa Jamhuri baada ya kufanya upelelezi?

Tatu,  DPP anahoji, “Katika maandamano ya watu zaidi ya 2000 unasemaje kama polisi ndio walipiga risasi, kama kuna maandamano ya nguvu polisi hawawezi kushitakiwa kwa mauaji au kesi za madai.”

Hapa kuna maswali: Je, kama hakubaliani na madai ya kwamba polisi ndio waliorusha risasi, kwanini afikie hitimisho la kuwatetea kuwa hawahusiki? Nani amemthibitishia, na yeye akaridhika pasi na shaka kuwa yale maandamano yalikuwa ya nguvu? Wapi amepata ujasiri wa kuamini nguvu iliyotumiwa na polisi ilistahili kuwa kwa kiwango walichoonyesha? Haya, tukubali kuwa maandamano yalikuwa ya nguvu; je, Akwilina alikuwa mshiriki wa maandamano hayo? Je, ni haki gani za mtu anayeumizwa kwenye kadhia asiyohusika nayo?

Nne, DPP anasema mwili wa Akwilina haukuwa na risasi iliyobaki [mwilini], hivyo ni ngumu kusema ilitoka kwa polisi! Kauli ya ajabu sana! Hadi leo miaka 57 ya Uhuru watalaamu wetu wa vyombo vya ulinzi na usalama hawawezi kutambua aina ya silaha iliyotumika kwenye mauaji kwa kuuchunguza mwili wa majeruhi au marehemu? Je, wataalamu wetu hawawezi kujua risasi gani imetumika hadi wapate masalia ya risasi?

Nayauliza maswali haya kwa sababu ilivyo ni kuwa mjadala wa kifo cha Akwilina umeshafungwa na mamlaka halali ya nchi, japo umefungwa kwa wepesi mno. Wapo wanaoumia wanapokumbuka maneno ya babake Akwilina aliposema, “Kifo cha mtoto wetu kimemaliza matumaini yote ya kuumaliza umaskini.” Naam, huyu mtoto ndiye aliyekuwa kama risasi yao ya mwisho. Waliuza kila walichoweza kuhakikisha wanamsomesha ili baadaye aweze kuwalea. Waliwekeza fedha na matumaini yao kwa mtoto ambaye baadaye ameuawa na waliokuwa na dhamana ya kumlinda. Bila shaka kauli ya DPP imewafanya waanze kulia upya.

DPP anasema hata polisi aliyerusha risasi hajulikani! Anataka kutuaminisha kuwa polisi wanapokabidhiwa bunduki na risasi huwa hawatakiwi kusaini popote? Je, anataka tuamini kuwa ule utaratibu wa risasi kuhesabiwa polisi wanaporejea kituoni ulishafutwa? Kama sivyo, polisi wote walirejea wakiwa na risasi timilifu? Je, siku hizi polisi wana mamlaka ya kurusha risasi bila kuamriwa na mkuu wao?

Waswahili walisema “asiyekuwa na wake ana Mungu”. Kauli ya DPP inathibitisha wazi kwamba, si tu wazazi wa Akwilina, bali wanyongewengi kuipata haki ni majaliwa. Hawana wao, isipokuwa Mungu tu. Lakini asisahahu kuwa “dau la mnyonge haliendi joshi”.

Majibu kwenye hitimisho la mauaji ya Akwilina yanaibua chuki ya wananchi wanyonge dhidi ya vyombo vya utoaji haki, na hasa hasa Serikali. Majibu mepesi kwa uonevu mkubwa kama huu kwa wazazi wa Akwilina yanawafanya wananchi waichukie Serikali kama walioua hawakutumwa kufanya hivyo. Majibu ya aina hii yanawafanya baadhi ya wananchi waamini kuwa kuna mtandao wa dhuluma miongoni mwa vyombo vya utoaji haki nchini. Hata kama hakuna mtandao wa aina hiyo, kwa majibu na matendo ya viongozi wetu wa vyombo vya utoaji haki ni vigumu mno kufuta nadharia hizo vichwani mwao.

Vyombo vya utoaji haki vinapopuuza au vinaposhindwa kutenda haki matokeo yake ndiyo yale tunayoyasikia kila mara ya “wananchi wenye hasira”. Unaweza kujiuliza, hizo hasira hutoka wapi endapo wananchi wanakuwa na imani na Polisi, DPP, Mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki?

Uhai wa mtu hauwezi kuzidiwa au kulinganishwa kwa thamani na kitu chochote kile. Wala hakuwezi kuwapo maelezo ya maana ya kutuliza roho za wafiwa zaidi ya kuwafanya waamini kwa kuona haki imetendeka.

Mauaji ya mtu asiye na hatia yanatia simanzi mno. Mtu asiyehusika kwenye vurugu anapouawa, halafu akakosa watetezi ni maudhi na laana kwa nchi. Sijasikia kelele za wananchi wakilalamika kwa kuona polisi wameua watuhumiwa wa ujambazi wenye silaha. Hawalalamiki kwa sababu wanajua polisi hana namna nyingine ya kukabiliana na mtu au watu wa aina hiyo isipokuwa kwa kutumia silaha. Lakini inapotokea akauawa mtu asiyekuwa hata na uwezo wa kurusha jiwe, hapo jamii hukata tamaa. Mbaya zaidi ni pale kiongozi kama DPP anapotangaza sababu dhaifu zinazomtuma kufuta mashitaka.

Bado najiuliza, angekuwa binti yake DPP ndiye kapigwa risasi angeyapokea kwa shangwe majibu ya aina ile aliyowapa wazazi wa Akwilina? Je, Akwilina angekuwa mtoto wa ofisa mwenye uwezo mkubwa serikalini au katika jamii angetendewa kwa namna hii?

Haya, tukubali kwamba hakuna polisi aliyehusika moja kwa moja katika mauaji hayo! Tukubali! Je, bado si busara kutoa kifuta machozi cha maana kwa wazazi wa Akwilina? Yanapatikana mafungu ya kuwalipa wengine, kwanini isiwe hivyo kwa wazazi ambao mtoto wao ameuawa kwa risasi ya nchi?

Mwito wangu kwa viongozi wenye majibu ya aina ya DPP ni kuwa kabla ya kuzungumza na kutoa mahitimisho mepesi kwa masuala yanayohusu uhai wa raia wema wa nchi hii, ni vema wakakaa upande wa wanaotendewa. Wapate ujasiri wa kujiuliza, “Je, ningekuwa mimi ndiye najibiwa hivi ningejisikiaje?”

Poleni wazazi wa Akwilina. Wahenga walisema, “Kuku wa mkata hatagi, na angetaga haangui, na akiangua halei, na akilea hutwaliwa na mwewe.” Ndivyo ilivyotokea kwa mwanenu. Mimba ilitungwa, akazaliwa Akwilina, mkamlea kwa shida licha ya umaskini wenu, lakini kabla ya kufaidi matunda ametwaliwa. Mungu wa haki atakisikia kilio chenu.

Bado naamini majibu mepesi aliyotoa DPP ni kwa sababu hayajamfika haya yaliyowafika wazazi wa Akwilina. Siku yakimfika hatafuta kesi kirahisi namna hii. Mungu anisamehe maana nami ni mzazi. Kila nikijaribu kuivaa hali waliyonayo wazazi wa Akwilina naumia mno.

1261 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!