Wkingunge-ngombale-mwiru-2-1iki niliyopita, mwandishi wa makala hii aliachambua chaguzi mbalimbali. Alifikia hatua ya kuchambua Uchaguzi wa Oktoba 31, 2005 ambako Tume ya Uchaguzi ilikuja na matokeo Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipata kura 5,276,827 yule mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alibahatisha kupata kura 2,271,491 huku Chama cha Wananchi (CUF) ikibaki na kura 695,667 tu chini kabisa ya zile alizopata mwaka ule 2005. Ndani ya Ukumbi wa Karimjee, anakumbuka kwamba viongozi wa Chadema hawakuhudhuria matangazo yale. Sasa endelea…

 

Kwa nini nachambua matokeo ya miaka hii ya nyuma mwaka huu? Sababu ni moja tu. Upinzani wanakuwaje na dhana ile ile ya kuibiwa kura, ya kutisha wananchi na ya kuanzisha hali ya kujitapa na ushindi? Ubabe wote huo wa nini? Waingereza wanasema “Why be so cocky before election?” Vipi kuwa vijogoo namna hiyo kabla ya chaguzi?  Nini kinawapagawisha hawa viongozi wa upinzani. Hilo mimi sintolifahamu.

 Hatimaye Dk. Slaa na chama chake, badala ya kukubali kushindwa (to concede defeat) ilivyozoelea nchi za Magharibi akaja na mwito kuwa “nchi hii haitatawalika.” Mtu kashindwa kwa tofauti ya kura 3,000,000 hakubali! Hapo ndipo demokrasia ya Afrika inapokuwa na mushkeli. Basi matokeo ya ile kaulimbiu yao kuwa nchi haitatawalika, tukaona misururu ya kususia vikao vya Bunge tangu siku Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete, anakwenda kulizindua Bunge jipya pale Dodoma.

Ususiaji ule uliendelezwa mpaka kwenye vikao vya Bunge Maalum la Katiba. Huko sasa likazaliwa wazo hili la Ukawa ambacho siyo chama ila ni muungano wa kienyeji usioeleweka wala kutambulika kisheria (it is a mere physical union scientifically with no recognition constitutionally).

Hata mwaka huu, katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 wapinzani tena wameghushi uzushi hatarishi ilimradi waonewe huruma (get sympathy from masses). Safari hii wamesema huko Njombe yamekamatwa masanduku kadhaa ya kura za CCM. Polisi wametuthibitishia hayo yalikuwa makasha yenye T-Shirts za CCM.

Huko Hanang nako wamezua eti mgombea ubunge Mary Nagu amekutwa na maboksi 10 ya kura za CCM tayari zimeshapigwa. Nako Polisi wamekanusha uvumi namna huo. Ni kwa nini upinzani wanakuwa wabunifu kwa uzushi na wanahodhi dhana ya kuibiwa tu? Huko Moshi Vijijini eti kuna masanduku ya kura yamebambwa katika gari la mgombea ubunge, Cyril Chami.

Yeye amekanusha kwa nguvu uzushi huo na kusema “Jamani mimi ni mzima wa afya, gari langu hilo hapo halikuchomwa moto na wananchi wanaodaiwa eti kuwa na hasira, na wala mimi sikulazwa “ICU” kama ambavyo uzushi umeenezwa kwenye mitandao ya kijamii. Nawaomba Watanzania na hasa watu wa Moshi Vijijini wapuuze uzushi huo ulioenezwa na watu wasio na nia njema. Hakuna sanduku la kura nililokamatwa nalo”.

Viongozi wa vyama namna hiyo ndiyo wanasababisha watu wawaogope na wapige kura za hasi (negative voting) kwa vyama vyao. Hapo ndipo CCM inaposhinda kiulaini. Wanalitafakari hili katika vikao vyao vya ndani (post-mortem after elections?)

Mungu kamwe hawabariki watu waovu na waongo. Sikiliza maneno haya:- “Nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonesha njia ambayo inawapasa kuienda na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu, ukawaweka juu yao wawe wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia kwa kumi” (Kitabu chake Kutoka Biblia kitabu cha sura18 mistari ile ya 20 – 21).

Ukitafakari huo mstari wa 21 utaona wazi Mungu ametupa viongozi wakuu (Rais). Tumeshafanya uamuzi wetu, tumewaacha wenye udhalimu na tumewaendea watu wachamungu na wenye kuchukia mapato ya udhalimu. Hayo ni maelekezo ya Mungu tangu kale. Tumeyafuata kwa ukamilifu katika Uchaguzi huu. (Soma Kut. 18:20 – 21).

Mimi nina kauzoefu kisaikolojia juu ya wananchi wa kawaida hawa. Niliwahi kuwa “Returning Officer” kule Songea katika uchaguzi wa urais mwaka ule 1962. Kati ya Mwalimu Julius Nyerere (TANU) na Zuberi Mtemvu (ANC). Nilisimamia maeneo ya Matiri, Liganga na Magagura, Songea Vijijini. Wapiga kura wazee walijazwa hofu kuwa ANC ni chama cha mtu katili sana ndiyo maana akawa na alama ya simba (mnyama hatari).

Basi kwa hofu waliyopakiwa kabla ya uchaguzi kila mzee asiyejua kusoma alikuja na kusema “Ne mbwitu lihimba ili nihagula mwehi bambo” kwa Kingoni wakimaanisha simtaki simba huyo nachagua mwezi! Kumbe simba ilikuwa alama ya ANC wakati mwezi ni alama ya TANU.

Vivyo hivyo wapigakura wa leo wanapoona fujo na vitisho vinavyofanywa na vijana wa vyama vya upinzani (waliopagawa kungojea kutawala) watu kimyakimya wanapigia kura CCM. Huko ni kupigia kura hasi (negative voting) kwa matendo ya wapinzani hasa huo ubabe wao.

Tumeona mafuriko ya watu katika kampeni za mwaka huu, si CCM wala si Chadema. Mwitikio umekuwa mkubwa mno. Hapa walikuwa wanapambana mafahali wawili wenye asili moja, malezi, yaleyale ya CCM na makuzi yaleyale. Tofauti ni mmoja mwana-CCM na mwingine ni kapi la CCM.

Pili mmoja mie nasema ni Yanga na mwingine ni Simba (bendera ya Chadema ni wekundu na weupe ukiachilia mbali kale karangi bluu pale pembeni). Tatu ni mpambano kati ya mpigania haki za maskini na wanyonge na mpigania mabepari wasiopenda umaskini (ndivyo alivyojitambulisha – kuwa yeye anachukia umaskini na atawatajirisha wote).

Kumekuwa na hili dai la “kulinda kura zao”. Jukumu hili kisheria ni la nani? Vipi Ukawa wang’ang’anie dhana hiyo huku wao walishiriki kupitisha  sheria ya uchaguzi bungeni? Walifikiri dhamana ya ulinzi wa kura ni ya kila chama? Nimefurahi kuona Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yenye majaji watatu imetoa tafsiri sahihi ya sheria hii na hivyo kuwafunga domo kaya lao Ukawa waliokuwa wakipotosha vijana wao eti lazima wakae vituoni kulinda kura!

Huu ni uchaguzi wa 15 katika nchi hii bado kuna watu hawajui sheria za uchaguzi? Jaji Kihiyo ametamka “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya mkutano siku ya uchaguzi kama kifungu Na. 104 (1) cha sheria sura 343 ya uchaguzi kinavyotaka.

Pili hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kukaa ndani ya wigo wa mita 200 wala nje ya mita 200 katika kituo cha kupigia kura wakati wa kuhesabu kura. Kama sheria inavyoelekeza, aidha kifungu Na. 72(2) kinaeleza kuwa mtu yeyote asiyehusika na hajatajwa katika kifungu kidogo cha kwanza hatakiwi kuwepo eneo la kituo.

Sasa yale maelekezo ya Mbowe, Mbatia na Mnyika yalikuwa na msingi upi? Huo ndiyo unaoitwa uchochezi wa makusudi na ni uvunjaji wa sheria za nchi. Lakini, tunashukuru ufafanuzi wa Mahakama Kuu na hapo Polisi watakuwa wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria tu.

Cha kushangaza kwangu mimi Chadema wanasema wanataka mabadiliko. Lakini hayo mabadiliko yataletwa na wazee waliochoka kama Ngombale-Mwiru na Lowassa? Umri wa Mzee Ngombale-Mwiru na umri wa mwasisi wa Chadema Mzee Edwin Mtei ni sawa sawa. Isitoshe hawa wawili ni rika moja. Walikuwa pamoja pale Tabora Upper School mwaka 1952). Leo Mzee Mtei amestaafu na kumwachia kijana wake Mbowe Chadema. Sasa vipi Mbowe amkumbatie Mzee Ngombale kusaidia kumnadi Mzee Lowassa? Hilo mimi sielewi. 

Mimi ninapomuona Mzee Ngombale-Mwiru akikebehi CCM na kujifanya anasaidia mabadiliko Chadema hapo ndipo sielewi hawa Chadema wanamuona kama kijana mwenzao?  Hicho ninakiita kichekesho cha mwaka!

Kama CCM wamekiuka Katiba aliyotunga na kuisimamia huyu Ngombale-Mwiru na Mngoni mmoja machachari akiitwa Gislar Mapunda, vipi leo anakashifu kazi yake mwenyewe? Yuko anayejikashifu mwenyewe? Enzi zake Ngombale-Mwiru alitunga Mwongozo wa TANU wa 1971 kule Handeni. Amekuwa anasimamia Ilani zote za Uchaguzi, hata hii ilani ya mwaka huu.

Anapokurupuka na kugeuka “about turn” anasukumwa na nini? Siyo imani ya chama cha Chadema au kupenda mabadiliko bali ni msukumo wa mshiko! 

Je, huko Chadema Katiba yao inasemaje? Kweli uteuzi wa Lowassa kutoka CCM na Juma Duni Haji kutoka CUF ulifuata Katiba? Kikao cha tarehe gani Baraza Kuu la Chadema lilimpambanisha Lowassa na mwanachama mwingine wa Chadema na zikapigwa kura ndipo akaibuka yeye kuwa ni pendekezo la Chadema? Ukawa kwa maana ya CUF, NCCR-Mageuzi, NLD walikaa kikao gani kumkubali kwa pamoja (unanimously)?

Tusidanganyane hapa! kama CCM walikiuka utaratibu kwa kumtema Lowassa pale Dodoma. Basi Chadema ndiyo hawana kabisa utaratibu wowote wa namna ya kuteua mgombea urais! Kwa uholela huo alipojitokeza Mzee Lowassa, wakamkumbatia mara na kumbebesha zigo hilo la kugombea urais. Chama kingekuwa na utaratibu mzuri sidhani kama wanachama wapya kutoka CCM wala CUF wangepokewa mara na kupewa nafasi za kugombea urais na mgombea mwenza nama ile.

Hata matumizi ya fedha za ruzuku tu huko Chadema yanatawaliwa kiimla. Hilo Mzee Ngombale-Mwiru wala Frederick Sumaye wanaona ni sawa? Basi ukiona chama hakifuati Katiba yake basi na wazee wanaokifuata chama nama hiyo hawana msimamo pia. Ni holela tu huko.

Katika taasisi namna hiyo viongozi wake wakipewa dhamana ya kutawala nchi kweli kutakuwa na sheria za kuendesha nchi? Mungu mkubwa anajua Watanzania wanataka utawala bora wa mtu mcha Mungu siyo wa wachumia tumbo. 

Viongozi wa vyama vya upinzani wajitafakari na kuepuka makosa yale yale ya kuhamaki, kuchochea vurugu, tabia ya shari na fujo na hata, kutunishiana misuli na vyomb vya dola. Badala yake vyama vijipange upya (re-organize).

Wakongwe wenye uchu wa madaraka wang’atuke ili vyama vichague uongozi mpya na vijana kwa hali ya kisasa. Kiongozi anang’ang’ania urais kila anapojaribu anabwagwa kwa nini asiachie ngazi? Chama siyo mtu mmoja tu wala siyo baba au mama mzazi. Hebu wapishwe wengine wenye mawazo endelevu waendeshe.

 

>>ITAENDELEA

1374 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!