Kampeni na uchaguzi vimeisha salama. Namshukuru Mungu kwa kutupatia hekima na busara zilizofanikisha kushiriki mchakato huu kwa amani na utulivu pamoja na changamoto zilizojitokeza.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, tumejifunza na kuona namna uchaguzi huu ulivyokuwa na ushindani mkubwa kuliko wakati wowote ule katika historia ya nchi yetu, wa kuleta mapinduzi ya haraka kwenye mfumo wetu wa demokrasia.

Ni lazima tukubali ya kuwa tujifunze kutofautiana zaidi kwa hoja za msingi, za namna tunavyofikiri tofauti juu ya njia mbalimbali zilizopo za kuleta maendeleo kwenye nchi yetu. Tutofautiane kiitikadi huku tukidumisha udugu wetu ambao ni hazina kuu ya Taifa letu.

Tunu ya Taifa letu ni udugu wetu, mshikamano wetu na amani yetu kwa ajili ya vizazi vyetu. Tayari nchi yetu imeshapata viongozi wanaopaswa kutimiza wajibu wao, huku wakitekeleza ahadi walizozitoa wakati wakisaka uongozi hapa na pale.

Tunalo jukumu la pamoja kuona ahadi zilizotolewa zinatekelezwa kwa wakati. Ili kuweza kufanikisha hili, ni lazima tukubali kuungana na kufanya kazi kwa pamoja. Tusahau yaliyopita tuliangalie Taifa letu kwanza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu wake hawawezi katu kutimiza wajibu wao kama hatutakuwa tayari kufanya kazi nao. Ni jukumu letu sote kuungana na kufanya kazi pamoja nao, kwa kuwaunga mkono katika kulikomboa Taifa letu na kuleta mabadiliko yaliyohubiriwa katika kipindi chote cha kampeni.

Dk. John Magufuli alihubiri mabadiliko ya kweli na katu hawezi kuyaleta peke yake bila kupewa ushirikiano. Samia Suluhu yeye binafsi alihubiri kumkomboa mwananchi wa kipato cha chini. Ni vyema tukawaunga mkono ili waweze kufikia malengo yao waliyoyaweka.

Wakati wa kampeni na kuuza maneno umekwisha, tupo katika kipindi cha kunena na kutenda, kipindi ambacho nchi imepata viongozi waliokwishaanza kuonesha dhamira ya kweli ya kumkomboa Mtanzania.

Nasi kwa pamoja tusimame tuwaombee Magufuli na Samia ili Mwenyezi Mungu awaongoze katika kulitumikia Taifa hili kwa hekima na utulivu.

Tunalo jukumu la pamoja kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na umoja katika kuboresha maisha yetu sote, huku tukipiga vita adui ujinga, umaskini na maradhi.

Natambua jukumu kubwa lililo mbele ya rais na wasaidizi wake, hivyo ni vyema tukampongeza kwa hivi alivyoanza kuonesha mwanga wa kile tunachotarajia kifanyike bila kutanguliza kejeli na vijembe ambavyo katu haviwezi kujenga.

Mabadiliko tunayoyahitaji na kuyahubiri tunaweza kuyapata iwapo tutaunganisha nguvu ya pamoja kipindi hiki na kuondokana na siasa za chuki na mtandao, zilizoasisiwa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na kuwa Dk. Magufuli hakuwa chaguo la kina fulani, tunalo jukumu la kumuunga mkono kwa hali na mali, katika kuliletea Taifa letu mabadiliko aliyoanza kuonesha hasa kwa kukomboa fedha zetu zilizo mikononi mwa wanyang’anyi wachache wakwepa kodi.

Tumpe muda wa kutimiza ahadi zake kwa maskini na walala njaa wasio na uhakika wa mlo mmoja kwa siku, huku akirudisha kile kikubwa kilichoporwa na manyang’au wachache. Kidole kimoja hakivunji chawa, anahitaji umoja wetu kutimiza ahadi zake kwetu.

Viongozi hawa wanapaswa kuombewa, nayasema haya kutokana na kasi wanayokwenda nayo. Wapo ambao hawatopendezwa na uamuzi wao, wapo watakaoumizwa na baadhi ya uamuzi, hivyo ni vyema tukatoa mchango wetu kwa pamoja kwa ajili ya nchi yetu.

Naamini Rais Magufuli hatabadilika, hatakuwa na nguvu ya soda kama ambavyo wengine wameanza kumbeza. Maana naamini anatambua wazi ushindi wake ulitokana na rekodi yake ya utendaji wake binafsi.

Watanzania wanahitaji viongozi wachapa kazi, na kuliletea Taifa matokeo chanya katika kipindi hiki ambacho kila mwananchi analalamikia umaskini uliotopea, huku baadhi ya ndugu zetu wakiishi maisha ya anasa.

Katika kuelekea mabadiliko ya kweli, ni vyema kila mmoja wetu akatimiza majukumu yake ipasavyo na si kusubiri mshtukizo wa Dk. Magufuli kama ilivyotokea katika baadhi ya ofisi za umma.

Dk. Magufuli na Samia peke yao hawawezi, wanahitaji  nguvu ya pamoja katika kufikia mabadiliko ya kweli kwa kila mmoja wetu. Tuwaunge mkono ili sote tuweze kunufaika na kile tunachokiandaa.

Tanzania ni nchi yetu sote, ni jukumu letu sote kuhakikisha inakuwa nchi ya maziwa na asali, kama kweli tunayo nia ya dhati ndani ya mioyo yetu.

2203 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!