SIMBA SC itawakosa wachezaji wake watatu, mabeki Mganda Juuko Murshid, mzawa Erasto Nyoni na kiungo Mghana, James Kotei katika mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar leo Jumatatu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kutokana na kutumikia adhabu ya kadi za njano.
Lakini kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre anajivunia kurejea kwa, Jonas Gerald Mkude aliyepona maumivu ya kifundo chake cha mguu alichoumia wiki mbili zilizopita mazoezini mjini Dar es Salaam baada ya kugongana na mchezaji mwenzake, Muzamil Yassin.

Pamoja na kadi tatu za njano, lakini pia Kotei anayeweza kucheza na nafasi za ulinzi pia, alishindwa kuendelea na mchezo Jumanne wiki iliyopita Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, Simba SC ilishinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji FC baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Salim Mbonde.
Na Lechantre amesema kikosi chake kipo vizuri, hakuna majeruhi na huenda akamtumia Mkude leo.
Alisema anahitaji pointi tatu muhimu kwa michezo iliyobakia ikiwemo dhidi ya Mtibwa Sugar leo na dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Alhamisi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Hizi ni mechi muhimu sana kwetu, tunahitaji pointi sita kabla ya kucheza na Yanga. Umakini ni muhimu kwa wachezaji wangu katika kila idara. Tutawakosa wachezaji watatu lakini pia kuna watu watachukua nafasi zao,” alisema Lechantre.

By Jamhuri