Simba Sc Kucheza Kagame Bila Mastaa wake

SIMBA imamua kuwapumzisha wachezaji wake mastaa wa kikosi cha kwanza katika michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa mastaa ambao wameachwa katika mashindano hayo ni Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Jonas Mkude.

Michuano hiyo imepangwa kuanza kutimua vumbi Juni 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Simba imepangwa Kundi C, pamoja na watani wao Yanga, St George ya Ethiopia na Dakadaha FC ya Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata Simba imefikia hatua hiyo ya kuwapumzisha nyota hao baada ya kikao cha pamoja na viongozi wa kamati ya utendaji.

Mtoa taarifa alisema, lengo la kuwaondoa wachezaji hao ni kwa ajili ya kutoa muda wa kuwapumzisha nyota hao waliotumika sana kwenye msimu uliopita na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Aliwataja wachezaji hao waliowapumzisha ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Asante Kwasi na Nicolaus Gyan.

Wengine ni Shiza Kichuya, James Kotei, Jonas Mkude, Juuko Murshid huku nahodha wa timu hiyo John Bocco akiwepo kikosini baada ya kuomba acheze michuano hiyo kwa ajili ya kujiweka fiti ili msimu ujao arejee akiwa fiti.

“Bocco ni mchezaji pekee atakayecheza michuano hii ya Kagame kati ya wale wachezaji waliokuwa katika kikosi cha kwanza baada ya yeye mwenyewe kuomba kucheza kwa ajili ya kujiweka fiti.

 

“Hivyo, kama uongozi tumeona tukubali ombi lake alilolitoa kwa uongozi lakini hao wachezaji wengine wote waliokuwa katika kikosi cha kwanza msimu uliopita, tutawapumzisha.

“Lengo letu msimu ujao warejee katika ligi wakiwa fiti na pia kuhofia kujitokeza idadi kubwa ya majeraha, hivyo tumekumekubaliana kuwapumzisha huku tukiendelea na mipango mingine,” alisema mtoa taarifa huyo.

Simba imepanga kuwa na kikosi cha wachezaji walio fiti kwa ajili ya msimu ujao na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tayari imeshasajili nyota watatu wapya ambao ni mastraika Marcel Boniventure Kaheza kutoka Majimaji, Mohammed Rashid kutoka Prisons na Adam Salamba kutoka Lipuli.