Makocha wa timu za Yanga na Singida United wametunziana heshima baada ya timu zao kumaliza dakika 90 zikitoka sare ya 1-1 Kombe la Mapinduzi

Wachezaji wa Yanga wamelazimika kupambana hadi dakika ya mwisho na kufanikiwa kupata sare ya 1-1, dhidi ya Singida United ukiwa ni mchezo wa mwisho wa michuano ya Kombe la Mapinduzi uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar.

Matokeo hayo yanaifanya Singida United kuwa vinara wa kundi B, kwa kufikisha pointi 13 sawa na Yanga lakini yenyewe inawastani mzuri wa mabao ya kufunga tofauti na Yanga ambayo inamabao machache.

Singida United itacheza na Azam FC ilishika nafasi ya pili kwenye kundi A, Jumatano usiku wakati siku hiyo hiyo Yanga itamenyana na URA ya Uganda katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ambayo imepangwa kupigwa kuanzia majira ya saa 10:30 slasiri.

Katika mchezo wa leo Singida United ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa kwa kichwa na Danny Lyanga aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Kiggi Makasi dakika ya 72.

Yanga ilisawazisha bao hilo dakika ya 90 kufuatia kona iliyochingwa na Juma Mahadhi kuunganishwa kwa kichwa na Said Juma Makapu na kufanya ubao wa mabao kusomeka 1-1.

Katika kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu na Yanga ndiyo walioanza kufika kwenye lango la Singida United na dakika ya 15 Ibrahim Ajibu nusura aifungie timu yake bao la kuongoza kufuatia mpira wa faulo uliookolewa vizuri na kipa Ally Mustaph ‘Barthez’

Dakika ya 27 Kambale Salita alishindwa kumalizia wavuni pasi nzuri kutoka kwa Lyanga akiwa amebaki na kipa Youth Rostand alipiga nje na mpira kuwa golikiki.

Dakika nne baadaye Kambale tena alipata nafasi nzuri lakini shuti alilopiga lilidakwa kiufundi na kipa Rostand ambaye katika mchezo wa leo alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo.

 

By Jamhuri