Nimeanzisha utaratibu wa kuandika ujumbe wenye kuhamasisha mabadiliko ya kifikra kwa vijana wa nchi yetu. Sababu ikiwa ni imani yangu kubwa kwamba hizi ni zama zetu kuchukua majukumu ya kuongoza mageuzi kwenye kila eneo la maisha ya jamii yetu. Kwenye siasa. Kwenye sanaa. Kwenye biashara. Kwenye kilimo. Kwenye utafiti. Kila kona.

Katika moja ya maandiko yangu kwenye ukurasa wangu wa Twitter (@HKigwangalla ) niliandika ujumbe wenye lengo la kuwaamsha vijana wahitimu wa vyuo kufungua bongo zao na kutoka nje ya boksi ili wazitambue fursa na watumie vipaji vyao kubadili hali zao na za Taifa kwa ujumla. Ujumbe huu haukueleweka.

Jambo moja zuri na la uhakika ni kwamba ujumbe ule umefikisha lengo kwa wahusika. Umezua mjadala. Naamini hii ni hatua muhimu sana kwenye mawasiliano. Suala la ajira ni lazima tulijadili maana halikwepeki. Ajira ni maisha yetu.

Bahati mbaya sana ni kwamba tukisema ‘ajira’, kila mtu haraka haraka anawaza ajira ya benki, serikalini, kiwandani n.k. Tulipofikia hizi hazitoshi, na tunakoelekea kutakuwa na janga la kitaifa la watu kukosa mahala pa kujishikiza ili kupata kipato chao cha kujikimu. Ni lazima tuwe wabunifu, kama nchi, tujiandae.

Utafiti wa NBS wa mwaka 2014 unaonesha ni watu 2,141,351 tu (takriban 4.3%) wa Tanzania Bara walioajiriwa kwenye sekta rasmi. Na ongezeko la ajira rasmi kutoka mwaka 2013 mpaka 2014 lilikuwa ajira 282,382 tu. Na kwamba sekta isiyo rasmi inaajiri watu wengi zaidi kuliko sekta ya umma.

Pia, asilimia 61.1 ya vijana walio kwenye umri wa kati ya miaka 15 – 24 wameajiriwa kwenye sekta binafsi. Lazima tujiulize kwa mwaka tunazalisha wahitimu wangapi kwenye fani zote, na viwango vyote vya elimu, kuanzia Cheti mpaka Shahada? Pia tuna fungu kiasi gani la mishahara kiasi cha kutoa ajira kwa wote wanaohitimu? Mwajiri mkubwa ni sekta binafsi, ambaye ameajiri asilimia 67 ya wote wenye ajira nchini.

Mfano rahisi kwangu ni mfano wa wahitimu wa taaluma ya udaktari. Kwa mwaka wanahitimu takriban madaktari 1,300; uwezo wa kuajiri ni madaktari kati ya 300 – 500 (kwa sekta zote za umma, hiari na binafsi). Hawa wengine wanaenda wapi? Nini kifanyike? Majibu yake yapo kwenye ‘kujiajiri’ na kuzalisha fursa mpya za ajira.

Sekta ya umma hufika mahali ikakoma kuajiri kwa kipindi fulani, sababu haitanuki. Inabidi kukuza ajira kwenye sekta binafsi. Ni lazima tuongeze uzalishaji. Ni lazima tufanye kazi ili tuzalishe ajira. Ndiyo maana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli inahamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Kuna watu wanadhani Serikali itajenga viwanda ili wao wakapate ajira. Kuna wengine wanadhani suluhu ya kujenga uchumi wa viwanda basi ni kuwapa mitaji wasomi waliohitimu vyuo vikuu. La sivyo hawawezi kujiajiri. Kuna watu wanaamini kuwa ili wajikomboe kimaisha ni lazima Serikali iwabebe, iwaajiri au iwape mitaji. Mimi nadhani hizi ni fikra potofu miongoni mwa vijana wetu. Ndiyo maana nimeanza kuwahamasisha wafikirie ‘nje ya boksi’. Wafikirie kubuni miradi itakayotatua changamoto mbalimbali kwenye jamii, na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejiajiri na wataajiri wengine.

Kuna mambo mengi sana kwenye kufikia kuwa na kizazi cha watu wabunifu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine; kubwa ni kuwa na msingi kwenye mfumo wetu wa elimu, kwamba uwaandae vijana kufikiri kibunifu zaidi na kijasiriamali kuliko kufikiri kwa ‘soma kwa bidii shuleni, faulu, pata digrii, nenda kapate ajira nzuri’. Na pia kuwa na mifumo inayowezesha na kurahisisha vijana wetu wabunifu na wajasiriamali kutambuliwa, kuendelezwa, na kuungwa mkono kwenye kazi zao za kibunifu, ikiwamo kuwezeshwa. Kwa hali ilivyo sasa, naamini tunahitaji kuwa na vijana wajasiri, wabunifu na wenye kuchukua hatua za kubeba ‘risk’ za kila aina kuanzisha shughuli mbalimbali za kimageuzi kwenye biashara, kilimo, sanaa, jamii n.k. Ni lazima vijana wetu waote ‘ndoto’ kubwa za mafanikio, watamani mambo makubwa, watamani mafanikio, wavutiwe na mafanikio ya wenzao; wajitoe kufanyia kazi mawazo yao, wabadilishe hali zao – watoke kwenye kundi la kulalamika na kulaumu, waingie kwenye kundi la wenye kuchukua hatua za kuishi ndoto zao. Kundi la ambao wataendelea kulaumu, kulalamika na kumtafuta mchawi wa maisha yao litabaki na watu wengi kwa hakika – na hawa wataajiriwa na kundi (dogo) la wale watakaohamasika kuota vitu vikubwa na kuziishi ndoto zao.

Mimi niliishi ndoto yangu – kuja kuwa DAKTARI. MBUNGE. MJASIRIAMALI. Na leo nimepewa heshima ya kuwa Naibu Waziri kwenye Serikali. Njia yangu haikuwa rahisi. Nilizaliwa Hospitali ya Maweni Kigoma, baba yangu akiwa mtu msomi akifanya kazi benki ya NBC pale Kigoma, na mama yangu akiwa mwalimu wa shule ya msingi. Ingetarajiwa niwe na maisha mazuri utotoni na hata ukubwani. Sababu ningeandaliwa kila kitu na wazazi. Haikuwa hivyo. Baba na mama waliachana (sababu hazinihusu) nikiwa na miaka kati ya minne na mitano, niliishia kurudishwa kijijini kwao baba (Goweko, Tabora) nikiwa na miaka minne/mitano hivi. Nikachunga sana ndama na mbuzi, nikaugua surua n.k. Mdogo wangu alifariki dunia kwa ugonjwa wa kupungukiwa damu. Nikabaki peke yangu. Nilienda shule bila viatu, kwa kushona viraka n.k.

Maisha yangu yote ya utoto yalikuwa ya kuhangaika chini ya malezi ya bibi, babu, na mama yangu. Niliishi utoto wangu kwa kula mlo mmoja (wakati mwingine uji tu), tena wa chumvi. Fagio la chuma lilipitia ajira ya mama yangu, na alilazimika kufanya biashara ya mama ntilie ili kutupatia mahitaji yetu muhimu. Niliuza jerebi, samaki, vitumbua, mihogo na karanga mitaa ya Nzega. Vijana niliokua nao wapo na ni mashahidi wa hili. Nilipona kifo kwa njaa ya mwanzo wa miaka ya 1980.

High School, nilisoma ShyBush, ambako kulikuwa hakuna walimu wa kutosha. Niliporudi likizo, nililazimika kuazima notisi za rafiki zangu akina Joseph Pius Mwami (leo hii Mhandisi) na nilizinukuu usiku kucha bila kufumba macho, chumbani kwangu ambako kulikuwa hakuna umeme, nilisoma kwa kibatari.

Nimepata Digrii ya Udaktari. Ubingwa wa Afya ya Jamii, Uongozi na Usimamizi wa Biashara n.k. Nimeanzisha kampuni, zikakua mpaka kufikia kuzungusha zaidi ya Sh bilioni 7 kwa mwaka. Nimekuwa mbunge n.k. Yote haya si katika mafanikio makubwa ninayoweza kusema najivunia. The biggest success ever in my life has been to achieve ‘self-recognition’ (kujitambua!). Kujua nguvu na uwezo wangu, kujua nina kusudi gani maishani na kutenda yanayopaswa kutendwa.

Ukijitambua utafika mbali. Ukikuta milango imefungwa utapita hata dirishani. Ukijitambua hushindwi kitu. Kujitambua kwangu kumenifanya nione kila kitu kinawezekana, maana kama mimi na historia yangu, leo hii nimeweza kuwa daktari n.k, nini sasa kitanishinda?

Mimi baada ya kuhitimu masomo yangu ya digrii ya kwanza ya udaktari, nilianza internship (mafunzo kwa vitendo); wiki tatu kabla ya kumaliza nilisimamishwa kazi sababu ya mgomo wa madaktari wa mwaka 2005. Kila tulipoenda tulikuwa hatuajiriki! Niliamua kuanzisha kampuni (pamoja na rafiki zangu wawili – wote graduates). Niliachana kabisa na habari za kusaka ajira, nikaamua kuwa mjasiriamali, mtafiti na consultant wa kujitegemea (ndiyo nikapata mkataba wa kuwashauri WAMA kama mtaalamu wa mikakati, siyo kama mwajiriwa).

Kabla ya hapo nilikuwa naendesha biashara ya taksi (nilianza na moja na zilifika nne – kila moja ikiniletea wikiendi Sh 60,000), saluni ya kike moja pale chuoni Muhimbili (ikileta Sh 200,000 kila wikiendi), na nne ndogo ndogo za kiume kule mitaani (kila moja ikiniletea wikiendi Sh 20,000). Niliuza biashara zote hizi na kuunganisha nguvu na mtaji wa kuanzisha biashara ya IT na ya pamba (kama wakala). Mwaka wa pili tulikopa Benki ya CRDB na kununua kiwanda chetu wenyewe. Leo hii tuna viwanda viwili (cha kuchambua pamba (ginnery), na cha kukamua mafuta (ya pamba na alizeti), tuna matrekta (saba) na malori (zaidi ya 30).

Biashara ya taksi niliianzisha kutokana na pesa zangu nilizoweka akiba kutokana na kazi za kibarua nilizokuwa nafanya baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari – nilikuwa nafundisha tuition, shule moja ya sekondari ya Badri iliyopo Nzega mjini, na kibarua mgodini. Aliyeniuzia gari nilimpa pesa nusu akanipa gari nikafanya kazi ya taksi huku nikimlipa kidogo kidogo hadi deni likaisha. Nakumbuka Wakili Alex Mgongolwa ndiye alisaini mkataba huu wa mauziano.

Kueleza kwa ufupi hivi ni rahisi. Ndani yake kuna details kama za kukosa hela ya pango. Kama ya kwenda kusoma nje ya nchi na kusambaza magazeti kwenye baridi ya asubuhi. Kama kukosa hela ya mafuta ya gari na kutembea kutoka Msasani (nilipokuwa naishi) kwenda mjini (Upanga) kwenye ofisi yetu. Kama kutapeliwa. Kuzunguka benki zaidi ya 10 kutafuta mkopo na kunyimwa. Kuna mengi.

Wengine watasema hata Ubunge 2010 nilibebwa, sawa tu. Lakini sisi Wakimbu huwa tuna msemo wetu mmoja, kwamba ‘lifti humkuta mtu aliye njiani’.

 

Makala hii imeandikwa na Dk. Khamis Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM) na Naibu Waziri waNaibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto. Anapatikana kupitia simu 0782636 963.

By Jamhuri