Siri zavuja Bandari

 

*Orodha ndefu ya watumishi aliowaonea Kipande yatajwa
*Wafanyakazi wambatiza ‘Last King of Scotland’ – Idi Amin
*Takukuru yachunguza unyanyasaji huu, malipo mishahara
*Aliyerejeshwa kwa nguvu ya wakubwa apanga kumhamisha
*Mgogoro wazidi kutanuka, amsukia zengwe mshindani kazini
*Yeye, Mwakyembe, wabunge wiki watumia Sh milioni 360
Na Deodatus Balile
Siri nzito zimeanza kuvuja jinsi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mzee Madeni Kipande (58), anavyofanya unyanyasaji kwa wafanyakazi wa Bandari hiyo, hasa wanawake, vyanzo vimeifahamisha JAMHURI.
Pia, wafanyakazi waliozungumza na JAMHURI (majina yanahifadhiwa kwa sababu za wazi), wamesema katika viambaza vya Bandari hiyo sasa wanamuona Kipande kama aliyekuwa kiongozi wa taifa la Uganda dikteta Idi Amin Dada.
“Chini kwa chini wafanyakazi wamembatiza jina IDI AMIN, na wengi wanarejea filamu ya ‘Last Kingo of Scotland’ inayoigiza udikteta aliokuwa akifanya Idi Amin, wanasema Kipande naye amejielekeza katika mlengo huo. Sasa Gawile [Kaimu Mkurugenzi wa Utumishi] amekuwa kama Kapteni Yamungu ambaye Idi Amin alikuwa anamwelekeza amkamate na kumuua nani kwa muda gani.
“Kipande amesema kwenye mkutano wa uongozi kuwa yeyote ambaye anapingana naye atamng’oa. Taarifa tulizonazo amesema yeyote asiyekubaliana na afanyacho yeye [Kipande] bila kujali hoja anayotoa aandikiwe barua ya kuondolewa kazini. Anasema itakayolipa fidia ni Serikali na si Bandari hivyo hajali,” kilisema chanzo chetu.
Katika mkondo huo, mwishoni mwa mwezi uliopita Kipande alianzisha mchakato wa kumsimamisha kazi Meneja wa Bandari ya Tanga, Hassan Kyomile. Habari za uhakika zilizoifikia JAMHURI, zimesema Kipande aliagiza Kyomile asimamishwe kazi kwa maelezo kwamba mwandishi wa habari hizi [Balile] ni Mhaya na Kyomile aliyeomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu TPA ni Mhaya, hivyo anaamini Kyomile ndiye anayevujisha siri za TPA kwa JAMHURI.
Kipande alimshusha cheo Kyomile mwezi Machi, mwaka huu kutoka Ukurugenzi wa Ununuzi na kumfanya Meneja wa Bandari ya Tanga, lakini kadiri joto la habari nzito zinazohusu madudu yake Bandari kupitia gazeti hili JAMHURI linaloanzia wanapoishia wengine linavyozidi, sasa anapanga kumsimamisha kazi. Ikumbukwe, Kyomile alijaza fomu kuomba nafasi ya Ukurugenzi Mkuu wa TPA mwaka jana, nafasi ambayo Kipande anaamini yeye kama Kaimu Mkurugenzi ndiye anayestahili kuijaza na hivyo ni kosa ‘nafasi yake’ kuombwa na mtu yeyote.
Aliagiza nafasi ya Kyomile na Franciscas Muindi ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko wa TPA zitangazwe na kujazwa mara moja kwa kuwa walikuwa wameomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu anayoikaimu. Nakala ya barua ya maelekezo yake, ambayo JAMHURI inayo, ilipingwa vikali na Bodi ya Wakurugenzi waliomwambia si kosa mtu yeyote ndani ya TPA kuomba nafasi yoyote ya kazi ilimradhi awe na sifa. Hata hivyo, hadi Jumapili (Mei 4), Kyomile alikuwa hajakabidhiwa barua ya kusimamishwa kazi, ambayo JAMHURI imehakikishiwa na vyanzo vyake kuwa imeandikwa siku 10 zilizopita.
Kwa upande wake Mama Muindi, aliyejaza fomu ya kuwania nafasi hiyo mwaka jana, Kipande amemsimamisha kazi kwa tuhuma kuwa anavujisha siri (madudu ya) za TPA kwenye vyombo vya habari. Hata hivyo, hadi leo si TPA wala Kipande waliojitokeza kukanusha kwa vielelezo tuhuma nyingi zinazohusiana na utendaji mbovu wa kiongozi huyo, ikiwamo kuhatarisha usalama wa Bandari kwa kutokuwapo CCTV camera na mita za kupima mafuta yanayoingia nchini kutofanya kazi kwa miaka mitatu sasa.
Orodha ya wafanyakazi aliowaonea Kipande ambayo sasa inachunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ni pamoja na Vulfrida Teye. Huyu kwa cheo chake ni Meneja wa Masuala ya Bodi ya Wakurugenzi.
Mama huyu alisimamishwa kazi na Kipande Agosti 2013 kwa tuhuma za kuondoa kipengele cha kununua vipuri vya SPM na mtu aliyewauzia Bandari Boya. Hajahojiwa na wala kurudishwa kazini.  Tuhuma zake zinaelezwa kuwa za uonevu kwani yeye si aliyekuwa na mamlaka ya kuihitimisha mkataba husika. Anaendelea kupokea mshahara na marupurupu mengine bila kufanya kazi hadi sasa na wala hajahojiwa na vyombo stahiki.
Mfanyakazi mwingine Ndugu Msemo, aliyekuwa Afisa Ununuzi, naye alisimamishwa kazi Agosti 2013 kwa tuhuma sawa na za Teye. Anaendelea kulipwa mshahara, na Kipande ameshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake, lakini anaapa kuwa milele hatarudishwa kazini wakati yeye akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu au Mkurugenzi Mkuu, ikiwa atabarikiwa kupewa nafasi hiyo. Msemo hajahojiwa na uongozi kwa tuhuma hizi.
Isaac Godson amehamishiwa Kigoma. Huyu ni Afisa Ununuzi Mwandamizi ambaye kwa cheo chake hakustahili kuhamia kwenye bandari ndogo kama Kigoma.
Erasto Lugenge ni Mwanasheria Mwandamizi wa TPA, ambaye Kipande ameagiza asimamishwe kazi, lakini hajui ni tuhuma zipi amwandikie kama mashtaka ya kusimamishwa kwake kazi. Bado analipwa mshahara na marupurupu bila kuwa kazini.
Mwingine ni Mama Nyirabu, alisimamishwa mwaka 2012, Eng. Mhayaya alikuwa Mhandisi Mwandamizi na Marcelina Kisanko Mhando. Huyu alisimamishwa kazi Desemba, 2012 lakini baada ya JAMHURI kuchapisha tuhuma hewa alizosimamishwa nazo na jinsi Kipande alivyokuwa anakiuka maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kumrejesha kazini, kwa shinikizo amemrejesha kazini. Lakini pamoja na kwamba ni Meneja Mifumo wa TEHAMA, mpango unasukwa kumhamishia mikoani. Awali Kipande alikuwa ameapa kuwa huyu asingerejea kazini wakati wa uhai wake.
Eng. Johnson Mutalemwa alikuwa Meneja wa Bandari Mwanza aliyesimamishwa kazi tangu mwaka 2013, lakini hadi leo kama wengine analipwa mshahara na mashitaka yake hayapo — ni hewa. Kilichobainika ni chuki binafsi za Kipande dhidi ya kabila la watu kama Mutalemwa.
Mwingine ni Kulwa Masaga, huyu alikuwa Karani wa ICT, amesimamishwa muda mrefu, lakini hatimaye baada ya shinikizo la gazeti JAMHURI, Aprili mwaka huu amemrejesha kazini.
Joseph Singano alikuwa Mkuu wa Ulinzi Bandari ya Mwanza, lakini taarifa ilizopata JAMHURI, zinaonesha barua ya kusimamishwa kazi ya Singano, inaonesha kuwa alizembea kusimamia ushuru wa mizigo Bandari Mwanza, wakati hilo ni suala la uhasibu kitu kisichokuwa sehemu ya kazi yake. Lucas Magomola wa Mwanza na Kassimu Mori wote wamesimamishwa miaka miwili iliyopita.
Cha kushangaza ni maelezo ya mdomo aliyotoa Kipande wakati anawasimamisha watumishi hawa wa Bandari ya Mwanza kuwa Mwanza ilikuwa wanajiendesha kwa hasara, hivyo ikamlazimu awasimamishe kazi lakini anaendelea kuwalipa mishahara kwa miaka miwili sasa. Hajawafungulia mashtaka wala nini.
Waliohamishwa kwa tuhuma hewa
Henry Arika, aliyekuwa Meneja Biashara wa Bandari ya Dar es Salaam, alihamishiwa Makao Makuu na kuambiwa kuripoti Idara ya Utawala tangu April 2013 hadi leo hii. Analipwa mshahara na marupurupu yake bila kufanya kazi kwa mwaka mmoja sasa, kwa sababu Kipande hamtaki.
Sasa anajulikana kama “freelance manager”.  Alituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa Mohammed Enterprises kiasi cha sh milioni 100 baada ya kuwa ameruhusu kuondolewa makontena bandarini yaliyokuwa yameweka msongamano mkubwa na kupunguza nafasi ya kushushia mizigo.
Arika aliruhusu makontena 70 baada ya kushauriana na Kaimu Meneja wa Bandari wakati huo, Mama Mosha, na hivyo kukubaliana kuruhusu makontena 70 ya sukari kati ya 100, ili 30 yabaki kama dhamana iwapo Mohammed Enterprises wangeshindwa kulipa.
“Huu ni utaratibu wa kibiashara uliozoeleka, na lengo ni kusaidia wateja waendelee na biashara zao, na wakati huo huo TPA isipate hasara. Hata Kipande anafanya hivyo hivyo kwa sasa. SUMATRA walichunguza sakata hili na kubaini kuwa Arika hakuwa na kosa, ila Kipande ameapa kuwa hampangii kazi ataendelea kuripoti kwa Mkurugenzi wa Utumishi na kurejea nyumbani kila siku.
“Hana meza, kiti wala ofisi. Anaripoti na kuondoka. Ni udhalilishaji wa hali ya juu kwa mtu aliyekuwa Meneja leo anatendewa kama kinyangarika. Inauma sana,” alisema mtoa habari wetu.
Kakusa, aliyekuwa Meneja wa Bandari Mtwara, alihamishiwa Bandari ya Kyela. Baadaye uamuzi ukabatilishwa na Bodi, kwa kuwa cheo chake kilikuwa kikubwa, na hii ingelikuwa kama kumshusha cheo.  Alikaa bila kazi yoyote tangu April 2013 na kuwajibika kuripoti makao makuu hadi alipostaafu mwishoni mwa mwaka jana.  Alituhumiwa na Kipande bila ushahidi kuwa alikuwa anauza kinyemela ardhi ya TPA Mtwara kwa wawekezaji.
Aliyekuwa Mkuu wa Bandari ya Kigoma, Nandi, naye yalimkuta. Alihamishiwa makao makuu  bila kazi yoyote na kuwajibika kuripoti Utumishi hadi alipostaafu mwanzoni mwa mwaka huu.  Alituhumiwa na Kipande kuwa alikuwa anakula rushwa kutoka kwa kampuni ya MUAPI iliyokuwa ina zabuni ya kuendesha Bandari ya Kigoma wakati huo, na sasa haipo tena.
Beatrice Jairo alihamishiwa Bandari Ndogo ya Nansio, Ukerewe nje ya Ikama. Alikuwa Afisa Mawasiliano Makao Makuu na hivi sasa kasimamishwa kazi bila mshahara eti alitoroka kazini (abscond). Alichukua ruhusa ya dharura, na alipoomba kuongeza ikacheleweshwa, na Kipande akasema ni mtoro kazini.
Levina Msia  alihamishiwa Bandari Ndogo ya Kasanga nje ya Ikama. Alikuwa Afisa Mawasiliano Mwandamizi Makao Makuu na hivi sasa kasimamishwa kazi bila mshahara eti alitoroka kazini (abscond), kwa kuwa alikuja Dar es Salaam kwa rufaa kutibiwa Muhimbili. Kipande anasema kwa nini hakupelekwa Mbeya.
Francisca Muindi, Mkurugenzi wa Masoko;  anachukiwa na Kipande kwa kutaka kuchukua “nafasi yake” ya CEO kwa vile aliiomba kazi hiyo ilipotangazwa. Kipande amemsimamisha kazi Aprili mwaka huu na anafanya uchunguzi wa tuhuma kuwa ana hujuma alizofanya kwa TPA bila kuzitaja.
Makatibu Muhtasi, Ms Rabia Mahfudhi , Zuhura Maganga, Mwantumu Ngoda na Michael Mganga anawahamisha ofisi moja hadi nyingine kila habari zinapochapishwa kwenye gazeti lolote, akiwatuhumu bila ushahidi kuwa ndiyo wanaovujisha siri za ofisi.
Wanawake waliokumbana na manyanyaso ya Kipande
Wanawake walioorodheshwa hapa chini, wamepata kunyanyaswa na Kipande kwa nyakati tofauti, ila kutokana na ufinyu wa nafasi leo tunaorodhesha majina yao tu na nafasi zao. Apolonia Mosha (Meneja Bandari Msaidizi, Dar es Salaam), Francisca Muindi (Mkurugenzi wa Masoko), Kokutulage Kazaura (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Adelaide Lukaija (Meneja Ununuzi) – huyu kaomba kustaafu mapema, Janet Ngowi (Meneja TEHAMA), Vulfrida Teye (Meneja wa Mambo ya Bodi), Marcelina Kisanko (Mhando) na Winnie Mulindwa ambaye alistaafu kama Meneja Bandari Msaidizi, Dar es Salaam (Utekelezaji).
Ajira za upendeleo
Kama kuna mgogoro unaofuka moshi ndani ya Bandari basi ni huu unaotokana na ajira za Mhandisi  Alois Matei, ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu (Maendeleo ya Miundombinu) na Mhandisi William Shilla, ambaye ni Mkurugenzi wa Uhandisi. Taarifa zilizopo bandarini ni kuwa wahandisi hawa wawili waliajiriwa na Kipande kupitia mlango wa nyuma. Hawakushiriki mchakato wa usaili bali waliletwa na kupewa barua za ajira. JAMHURI bado inakamilisha orodha ya wafanyakazi wa aina hii walioajiriwa katika Kurugenzi ya Sheria bila kufuata mkondo sahihi pia.
Wanawake wasio watumishi wa Bandari aliowadhalilisha
Ukiacha wafanyakazi wa Bandari, Kipande amekuwa hana staha hata kwa wafanyakazi wanaofika ofisini kwake bila kuwa watumishi wa Bandari. Prediganda Assenga, ambaye ni Meneja Biashara wa TICTS,  alionja joto ya jiwe la Kipande.
Mwaka juzi Prediganda alifika ofisini kwa Kipande akifuatana na bosi wake mpya, yaani Mtendaji Mkuu wa TICTS, kwa minajili ya utambulisho, yakamkuta. “Mara tu alipomuona, Kipande alitamka kwa jazba na hasira mbele ya Mtendaji Mkuu wa TICTS kuwa Prediganda aondoke ofisini kwake, kwa kuwa anafahamu ni mwizi mkubwa na alimtaka huyo bosi wake aliyefuatana naye, amfukuze kazi mara moja pamoja na mameneja wote weusi hapo TICTS. Mama huyu ni mwaminifu haijapata kutokea. Kila aliyekuwapo alishangaa Kipande kwa nini alifyatuka hivyo.
“Mgeni huyo alimsihi Kipande kumruhusu Prediganda afanye utambulisho, naye alikubali kwa sharti kuwa asioongee lolote. Isingelikuwa busara za Mtendaji Mkuu wa TICTS, bila shaka pangelichimbika,” kilisema chanzo chetu.
Pia Kipande alimdhalilisha Rukia Shamte ambaye ni Mtendaji Mkuu wa “Central Corridor Transit Transport Facilitation Agency”. Mara kadhaa amekuwa akimdhalilisha mbele ya watu kila mara.  Kipande anamtuhumu kiongozi huyo wa kike, tena mwenye sifa na uzoefu uliotukuka katika sekta ya usafirishaji hapa nchini na hata nje ya nchi; kuwa ni “mdandiaji wa mambo” yasiyomhusu.
Fikra hizi potofu zilijengwa na Kipande kwa sababu hakutaka kuthamini mchango wa Rukia na wala kupata ushauri wake. Ilifikia hatua Kipande kumtuhumu Rukia kwa maandishi kwamba anamwamuru kazi wakati si bosi wake!
Je, unafahamu hatua wanazotaka kuchukua wafanyakazi baada ya ahadi aliyowapa Waziri Mwakyembe, kutokana na ushauri potofu na wa uongo wa Kipande kuwa wangelipwa bonasi? Usiikose JAMHURI, wiki ijayo.
Kipande, Mwakyembe watumia milioni 360
Katika hatua nyingine, habari za uhakika kutoka TPA zinasema Kipande, Mwakyembe na wabunge kadhaa wametumia dola 200,000 (Sh milioni 364) kwa wiki moja katika ziara ya kufungua ofisi ya biashara ya TPA mjini Lubumbashi, DRC.
Ziara hii, Kipande ameifanya wakati siku za nyuma alikuwa akipinga ziara za kuitangaza TPA akidai ni wizi. Nakala za maandishi ya Kipande kwenda Idara ya Masoko siku za nyuma, zilikuwa zikielekeza kuwa kwenda kuitangaza Bandari Zambia au kufungua ofisi ni kupoteza mapato na wizi wa wazi.
“Bandari ya Dar es Salaam Zambia wanaifahamu tangu enzi za Mwalimu Nyerere, hivyo hakuna sababu ya kukutana na wafanyabiashara kuitangaza,” aliandika Kipande katika moja ya madokezo kupinga mipango ya kuhamaisha watumiaji wa bandari.
Wabunge wawili, ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu, Zainabu Madabida na Peter Serukamba, walishiriki ziara hiyo iliyoteketeza mamilioni ya shilingi. Zipo tuhuma pia kuwa baadhi ya wajumbe katika safari hiyo wamelipwa posho mara mbili. Wamelipwa kwenye vituo vyao vya kazi, na Bandari imewalipia pia.