Kipande abanwa Bandari

*Nguvu za ajabu alizokuwa nazo zaanza kuyeyuka, alalamika Kikwete hamsaidii
*Marafiki zake wamtaka asimsingizie Rais, wasema amejiharibia mwenyewe
*Ashinikizwa awarejeshe kazini aliowafukuza kibabe, wafanyakazi washangilia
*Aanza kuogopa kivuli chake, ajitolea ‘photocopy’, adai wanaomsaliti anao TPA
*Mtawa asema asihusishwe na Kipande, bandarini wasema JAMHURI mkombozi
*Mwakyembe aweweseka, adai Lowassa, Profesa Tibaijuka hawamtakii mema
Nguvu za ajabu alizokuwa nazo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (58), zimeanza kuyeyuka kwa kasi baada ya GazetiJAMHURI kuchapisha mfululizo maovu anayotenda kwa kutumia wadhifa wake.
Vyanzo vya kuaminika vilivyopo karibu na Kipande, vinasema kwa sasa ameacha kumwamini kila mtu na hasa baada ya JAMHURI kupata habari za ndani ya kikao alichokuwa anatamba kuwa amemng’oa Mkurugenzi wa Masoko, Francisca Muindi, kitu ambacho hakutarajia kuwa kingelifikia gazeti hili.
“Jana [Jumanne iliyopita] siku nzima alikuwa anaweweseka ofisini. Anazungumza mwenyewe na ametangaza kuwa maadui wake wamo humu humu ndani ya TPA. Bila kufikiria, akasema alidhani mbaya wake ni Mama Muindi, lakini anashangaa kwa nini Gazeti JAMHURI linaendelea kupata habari za ndani ya vikao hata baada ya Mama Muindi kuondoka,” kilisema chanzo chetu.
Kutokana na hali hiyo, hata baada ya kumfukuza kazi mmoja wa makatibu muhtasi akidhani ndiye anayevujisha siri za ofisini kwake, ameshangaa kuona JAMHURI limeendelea kupata nyaraka anazoamini kuwa ni za siri kwake na zipo mikononi mwake tu.
“Sasa hivi ana mkoba, anaotembea ameubeba. Anafika ofisini saa 12 asubuhi, tena juzi aliingia amebeba vitu ambavyo hatukufahamu ni nini. Akifika amavua viatu, anatembea mwenyewe na soksi anakwenda kujitolea ‘photocopy’ (kurudufisha) anasema hamwamini tena mtu yeyote,” kilisema chanzo chetu kingine.
Kipande adai Rais Kikwete hamsaidii
Mmoja wa watu walio karibu na Kipande, ameiambia JAMHURI kuwa yeye na marafiki zake wengine wameshangazwa na kauli aliyoitoa Kipande wiki iliyopita kuwa “Rais Kikwete hamsaidii.” “Hii lilitushangaza sana. Alisema tatizo la watu wa Bagamoyo hawasaidiani. Akasema kuna kila dalili kuwa watu wa Bagamoyo hawapendani, ila sasa amebaki kusaidiwa na Waziri Dk. Harrison Mwakyembe.
“Akasema kama si Dk. Mwakyembe angekwishaondolewa bandarini. Kauli hii inaunganishwa na kitendo alichokuwa amekifanya bandarini kwa kuwafokea mameneja kuwa wanavujisha habari kwenye vyombo vya habari na wanataka aondolewe Bandari. Hii ilishangaza wengi,” kilisema chanzo chetu.
Mmoja wa wafanyazi aliye karibu na Kipande, ameiambia JAMHURI kuwa Kipande hapaswi kumsingizia Rais Kikwete hata chembe.
“Rais Kikwete anataka amsaidie nini? Hakuzuia na pengine aliwezesha ateuliwe kukaimu nafasi ya ukurugenzi mkuu Bandari. Katika kipindi hiki ambacho Kipande alipaswa kufahamu kuwa ni cha uangalizi, yeye ameanza tambo, majigambo na kufanya vituko visivyokubalika.
“Leo unakaimu unafukuza watu bila kufuata taratibu za kisheria. Tena anasema Serikali haiwezi kukosa fedha za kuwalipa hata wakishinda kesi mahakamani. Bodi ya Wakurugenzi imebaini kuwa baadhi ya wafanyakazi kama Marcelina Mhando aliwaonea na kuagiza awarejeshe kazini, kwa mwaka mzima sasa hajawarejeshwa amekaidi maelekezo ya Bodi.
“Bodi ilimtaka aanze na mradi wa kufunga CCTV cameras na kusitisha miradi 21 ya kiujanja ya ICT inayotumiwa kutafuna fedha, akakaidi maagizo ya Bodi. Bodi ilimtaka awe anaipa taarifa kila wiki, hadi leo amegoma kufanya hivyo. Bodi ilimkataza asitangaze kazi za watu walioomba kazi ya ukurugenzi mkuu, leo amemsimamisha kazi Mama Muindi, amemshusha cheo [Hassan] Kyomile.
“Kamati ya Mbakileki aliyoiunda Waziri Mwakyembe kuchambua utendani wa Bandari ilitoa maelekezo mengi tu, lakini hadi leo hajatekeleza hata moja. Mpango wa Big Results Now (BRN) Kipande ameutelekeza, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kuhamisha mizigo kama BP hawatapitisha tena mafuta yao hapa Dar es Salaam kutokana na vurugu zake na megine mengi. Sasa Rais Kikwete anahusishwaje katika utendaji huu mbovu wa Kipande? Akubali kuwajibika binafsi, asianze kutafuta visingizio,” kilisema chanzo chetu.
Ashinikizwa awarejeshe kazini aliowafukuza
Kwa upande mwingine, wiki iliyopita ilikuwa wiki ya furaha ya aina yake kwa wafanyakazi wa Bandari, baada ya Kipande ‘kulamba matapishi yake’ na kulazimika kuwarejesha kazini wafanyakazi aliokwishaapa kuwa wasingerejea kazini wakati wa uongozi wake.
Mzee Kipande mara kadhaa kwenye mikutano rasmi ya watumishi na nje ya vikao, alikuwa akiapa kuwa pamoja na Bodi ya Wakurugenzi kuelekeza amrejeshe kazini Marcelina Mhando, aliyethibitika kufukuzwa kazi kutoka Kurugenzi ya ICT kwa majungu, asilani asingefanya hivyo.
“Aliapa kuwa asingewarejesha. Na kweli kama si nyie JAMHURI kuchapisha habari zake, alikuwa ameikaidi Bodi. Bodi ilielekeza Mama Mhando arejeshwe kazini tangu Mei 15, 2013 lakini hakufanya hivyo hadi Jumatano wiki hii. Mama Mhando na mfanyakazi mwingine, Kulwa Masaga, wamerejeshwa kazini kwa shinikizo kutoka juu siku ya Alhamisi, wiki hii (Arili 24, 2014).
“Kimsingi tunawashukuru kwa dhati JAMHURI mmewezesha haki kutendeka na wale waliokuwa wameporwa haki sasa imerejeshwa na tunapotembea tunajisikia tunaye mtetezi wetu [JAMHURI] nasi tunatembea kifua mbele. Tumebaini kuwa kalamu ina nguvu. Kwa kuwa kila mnachoandika ni ukweli mtupu, hata wakubwa wanapata fursa ya kumfahamu vyema Kipande na inatusaidia wao kumbana,” kilisema chanzo chetu kingine.
JAMHURI imejiridhisha kwa asilimia 100 kuwa kweli wafanyakazi hao wawili wamerejeshwa kazini wiki iliyopita kwa shinikizo na kadri maelekezo yalivyo, wafanyakazi wote walioondolewa kazini bila kufuata taratibu au kuwapo sababu za msingi imeelekezwa warejeshwe kazini mara moja.
Chanzo chetu cha habari kinasema hatua hiyo imetokana na Rais Kikwete kumwagiza Dk. Mwakyembe ‘aondoe’ matatizo yaliyopo bandarini kwani hataki kusikia jina lake linachafuliwa wakati yeye hahusiki kwa hali yoyote na utendaji mbovu wa Kipande.
Baada ya kuwapo kwa taarifa hizo, wafanyakazi kadhaa waliosimamishwa kazi katika Bandari ya Mwanza, waliwasiliana na JAMHURI na kuijulisha kuwa hata wao Kipande alipofika aliwaondoa kazini, akisema Bandari ya Mwanza haizalishi, ila ajabu ameendelea kuwalipa mishahara, posho na stahiki nyingine zote kwa muda wa miaka miwili sasa.
“Sasa tunajiuliza utimamu wa Mkurugenzi huyu ukoje? Unawaondoa watu kazini kwa maelezo kuwa Bandari ya Mwanza haizalishi, unaendelea kuwalipa mishahara kwa miaka miwili wakati hawafanyi kazi, sielewi huu ni mfumo au fikira za aina gani katika uongozi. Tusaidieni wana-JAMHURI, mjulisheni Rais wetu Kikwete afahamu kuwa Kipande anaiua Bandari,” kilisema chanzo chetu kutoka Mwanza.
Mtawa akana kumbeba
Msaidizi Binafsi wa Rais Kikwete, Kassim Mtawa, ilipofika saa 4:19 siku ya Alhamisi (Aprili 24) alimpigia simu Mwandishi wa Habari hizi akitumia simu ya mezani, pamoja na vitisho na matusi aliyomporomoshea mwandishi, akaeleza kuwa yeye hamkingii kifua Kipande na hapendi kuhusishwa naye.
“Mimi ndiye Mtawa unayemwandika kwenye magazeti yako kila siku kuwa nambeba Kipande. Nashangaa waandishi wa siku hizi hamna maadili kabisa. Unaandika upande mmoja huniulizi, unadai mimi nambeba Kipande. Nikiwashitaki nitawafilisi. Kwanza gazeti lenu hilo halina kitu. Nasema kama mna ugomvi wenu na Kipande muendelee, ila msinihusishe. Sitaki kuandikwa kwenye gazeti lenu,” baada ya kutamka hayo akakata simu.
Gazeti hili kwa wiki ya nne sasa linachapisha habari za utendaji mbovu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mzee Madeni Kipande (58), ambaye ana kiburi, jeuri na ambaye muda wote amekuwa akiwatisha wafanyakazi walioko chini yake kuwa yeye ni ndugu wa karibu wa Rais Kikwete, hivyo akiwaburuza atakavyo.
JAMHURI imeeleza kwa ufasaha kuwa hata baadhi ya malalamiko yanayopelekwa Ofisi ya Rais Ikulu hayamfikii Rais Kikwete, kwani Kassim Mtawa na Mnikulu Shaaban Gurumo wametuhumiwa kuwa mara zote wamekuwa wakimkingia kifua Kipande kutokana na ukabila kwa kuwa wote wanatoka Bagamoyo.
Mtawa na Gurumo kupitia gazeti moja la kila wiki [si JAMHURI] walikanusha taarifa hizo na JAMHURI ikarejea kanusho hilo wiki iliyopita. Juhudi za JAMHURI kuwapata Mtawa na Gurumo awali ziligonga mwamba, baada ya kuwa hawapokei simu zao na hata gazeti hili lilipokwenda lango kuu la Ikulu kuomba miadi ya kuzungumza na wakubwa hawa, liliambiwa kuwa liandike maswali na kuyawasilisha.
Mtawa kwa kujua kuwa anayo mambo asiyotaka yafahamike, baada ya matusi hayo na kukata simu wiki iliyopita akikwepa kuulizwa maswali, mwandishi aliendelea kupiga simu hiyo ya mezani zaidi ya mara tano lakini Mtawa hakuipokea.
Ukiacha Mtawa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alipata kuiambia JAMHURI wiki mbili zilizopita kuwa Ikulu haina mpango wa kumbeba Kipande kwa njia yoyote.
“Ikulu haikingii mtu yeyote kifua. Hawezi kufanya mambo yake ovyo, akasema ana kinga ya Ikulu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ina Bodi ya Wakurugenzi na Waziri mwenye dhamana na masuala ya uchukuzi, ambao wanapaswa kuhakikisha kuwa utendaji unakwenda kwa mujibu wa sheria. Balozi Sefue aliahidi kulifuatilia suala hilo kubaini uhalisia wa kinachoendelea.
Hata hivyo, kwa muda mrefu kabla ya JAMHURI kuanza kuchapisha habari hizi kwa kina, Kipande na mmoja wa wakurugenzi swahiba wake, walikuwa wakiidharau Bodi ya Wakurugenzi kwa kiwango cha kutisha. Kipande alipata kuiambia Bodi ya Wakurugenzi, Agosti 2013 wakiwa Dodoma kuwa atahakikisha asiowapenda katika Bodi anawaondoa.
Kwa nguvu alizokuwa nazo, alikuwa akipuuza karibu kila analoagizwa na Bodi, na kweli kama lilivyochapisha gazeti hili wiki iliyopita Bodi hiyo aliyokuwa haitaki alimshinikiza Dk. Mwakyembe akaivunja na kuondoa wakurugenzi watano aliokuwa hawataki, huku akiunda Bodi mpya ya Bandari isiyo na mwanamke hata mmoja.
Kinyume na taratibu za kisheria, Mwakyembe kwa ushawishi wa Kipande alimteua mmoja wa wafanyazi ambao ni wahudumu wa ofisi kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari. Mfanyakazi wa kawaida, Edmund Njowoka, aliteuliwa kwenye Bodi mpya ya wanaume sita, wakati Sheria inamtambua Mkurugenzi Mkuu tu kuwa ndiye anayepaswa kuwa Katibu wa Bodi na wala hapigi kura katika uamuzi.
Baadhi ya wanasheria wameiambia JAMHURI kuwa kitendo cha Njowoka kuteuliwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari, kinavunja misingi ya utawala wa sheria kwani mbali na kwamba Njowoka kicheo hana mamlaka ya kumsimamia hata mfanyakazi mwenzake ukiacha jukumu alilonalo kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini, Bodi ya Wakurugenzi ni chombo cha kusimamia utendaji wa Mamlaka, hivyo mfanyakazi kuwa Mjumbe wa Bodi inampa fursa ya kupotosha au kupindisha uhalisia wa utendaji wa Mamlaka, hivyo Bodi hiyo si halali.
Bodi iliyovunjwa na Kipande alikuwa akiwatukana wakurugenzi kuwa hawana elimu ya kutosha, ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kwamba wengi, bila kujali sifa zao, walikuwa ni Wachagga hivyo wanaweza kusuka mkakati wa kuiibia Bandari.
Wafanyakazi waishukuru JAMHURI
Kwa wiki mbili mfululizo, Gazeti JAMHURI limekuwa likipata rundo la salamu za pongezi kutoka kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, wanaosema gazeti hili limewawezesha kujisikia nao ni binadamu katika Jamhuri huru ya Tanzania.
Wafanyakazi hao wanaipongeza JAMHURI kwa maelezo kuwa kila linachoandika gazeti hili ikiwamo CCTV camera kutofanya kazi, mita za kupima mafuta ya petroli yanayoingizwa nchini kutotumika, viongozi kubuni miradi ya ulaji kama ujenzi wa yadi ya magari ya CCM SUKITA uliopangiwa Sh bilioni 10 za kuanzia na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akaukana, kunyanyasa wafanyakazi na hasa wanawake kuwa ni za kweli.
“Sisi sijui tuwape nini. Mazingira tuliyomo hayaturuhusu, ila mwelekeo ulivyo tutaandamana kulipongeza Gazeti la JAMHURI si muda mrefu. Hapa bandarini kuna uozo mwingi. Huyu Kipande katudanganya kuwa tungepata bonasi, kamtumia Dk. Mwakyembe kututangazia hilo wafanyakazi wote, Hazina wakasema hatujatimiza malengo hivyo hatuwezi kulipana bonasi. Hakika mmethibitisha kaulimbiu yenu kuwa MNAANZIA WANAPOISHIA WENGINE.
“Huyu bwana anatuonea kama nini. Ametoa waraka kuwa hairuhusiwi yeye anapopanda kwenye lift mfanyakazi yoyote kupanda naye. Huyu baba ni mbaguzi sijapata kuona. Tunawapongeza JAMHURI, endelezeni kazi hii nzuri na hata wafanyakazi wenzetu, Marcelina na Kulwa, waliporudishwa kazini baada ya kazi yenu nzuri tumesherehekea. Tunasema kurejea kwao ni sawa na kuwa JAMHURI imejifungua mtoto ajulikanaye kama HAKI, yaani imeleta heshima na kurejesha utawala wa sheria bandarini.
“Sisi hatumuombei mabaya baba huyu, wala hatusemi aondolewe kazini lakini aheshimu watu, aheshimu sheria, aache ubaguzi kwa wanawake, tunapanga kama tutaweza kuandamana kudai lazima Bodi ya Wakurugenzi ya TPA iwe na Mkurugenzi mwanamke, hatuutaki mfumo dume. Anaturudisha miaka mingi nyuma na mapato ya Bandari hayakui kwa kasi inayostahili kutokana na vurugu zake,” kisema chanzo chetu kingine.
Mwakyembe awarukia Lowassa, Tibaijuka
Habari za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema kuwa Dk. Mwakyembe anaapiza mbingu na mizimu kuwa gazeti hili linachapisha kashfa za Bandari kwa nia ya kuonesha kuwa utendaji wake [Dk. Mwakyembe] ni mbovu. Anasema linatumwa na Waziri Mkuu (mstaafu), Edward Lowassa, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuanika uozo huo.
“Huyu Dk. Mwakyembe tumemshangaa sana. Anasema mbele ya watu, tena kwa sauti kuwa Lowassa na Tibaijuka ndiyo wanaochochea habari hizi zichapishwe, ili aonekane hawezi kazi. Hii yote ukimwangalia Dk. Mwakyembe, anasema haya akilenga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Anaona Lowassa ni tishio kwa yeye kuteuliwa na CCM na akimwangalia Profesa Tibaijuka, anaona kwa uwezo wake kitaaluma na kiutendaji, akiamua kugombea urais atamtupilia mbali Mwakyembe.
“Ndiyo maana kwa mkakati huo, anamtumia Kipande kufanya mbinu za kumfukuza kazi Mama Muindi ambaye ni mdogo wake Profesa Tibaijuka kama njia ya kumpa kashfa profesa. Wala pale hakuna kingine zaidi ya ugomvi wa urais mwaka 2015. Lakini sisi tunajiuliza mengi. Hivi Lowassa na Tibaijuka ndiyo wanaomwambia Kipande akaidi maagizo ya Bodi? Hivi ndiyo wanaofanya Kipande anyanyase wafanyakazi? Hivi ndiyo wanaofanya Kipande na yeye Mwakyembe watoe ahadi hewa ya bonasi kwa wafanyakazi?
“Ninachoona hapa, Mwakyembe aseme tu kuwa anamtetea Kipande kwa sababu ya Sh milioni 400 alizomtengea kwenye bajeti azitumie kujenga ‘rest house’ kule Matema Beach jimboni kwake Kyela, na ukarimu mwingine anaomfanyia, lakini asianze kurusha shutuma kwa watu wasiohusika,” kilisema chanzo chetu.
Mwakyembe kwa upande wake hataki kuzungumza na Gazeti JAMHURI, huku akidai kuwa hapewi nafasi kuzungumza aliyonayo, na gazeti hili limekuwa tayari muda wote kumpa nafasi ya kuchapisha chochote anachotaka kusema kuhusiana na kinachoendelea bandarini akitaka hata sasa, huku Kipande akisema maswali anayoulizwa kuhusiana na yanayoandikwa ni ya kitoto. Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Msambichaka, aliyeko Mbeya hataki kupokea simu.
Suala hili limewagawa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, na taarifa zilizoifikia JAMHURI zinasema, wiki iliyopita wakurugenzi watatu kati ya sita ndani ya Bodi ya sasa ya Bandari, walikuwa wanafikiria kujiuzulu kwani Bodi hiyo haionekani kuwa na meno wala kazi yoyote mbele ya Kipande zaidi ya kuwaharibia sifa. Usikose mwendelezo wa habari hii wiki ijayo.