Siku moja nilipokuwa nikisherehekea siku yangu ya kuzaliwa, mjukuu wangu mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alinizawadia kitabu kiitwacho ‘Waafrika Ndivyo Tulivyo?’

Kitabu hicho kimeandikwa na msomi mhandisi aliyebobea. Huyu mhandisi amechambua vizuri sana kiini cha uduni wa maendeleo ya Bara la Afrika. Ameonesha dhahiri mchango wa sisi Waafrika wenyewe namna tunavyosaidia kudunisha hali ya bara hili, hasa kusini mwa Jangwa la Sahara. Kila Mwafrika anajivunia kutambuliwa kama mwana wa bara hili, lakini katika Waafrika wa bara hili wapo wale wa kaskazini ambao ni Waarabu na wamestaarabika tangu karne nyingi.


Kwa vile wanapakana na Ulaya kwa Bahari ya Mediterranean, basi wameshabihiana sana na Wazungu kwa kila hali. Miji kama Tripoli, Algiers, Tunis, Alexandria hata Cairo kimtazamo wa maisha ni kama Ulaya. Hivyo Wazungu wanapoongelea Bara la Afrika wameongezea “JEUSI” au KUSINI MWA JANGWANI LA SAHARA. Wamezoea kuita “Bara Jeusi” (Black Continent) au tu “Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara” (Africa South of the Sahara). Huko ndiko tunakoishi watu weusi! Kwa hiyo kwa Ulaya, Marekani na kwingineko “Bara Jeusi” ni huku kwetu sisi, wala si huko Afrika Kaskazini.

 

Mwandishi wa kitabu hiki ‘Waafrika Ndivyo Walivyo’ ni Mtanzania mmoja wa hawa watu weusi. Anaitwa Malima M. P. Bundara. Kwa vile ni msomi na amefanya kazi sehemu mbalimbali, ana uzoefu wa kutosha na uchambuzi wake ni wa kina na una ukweli. Ana shahada ya Msc ya Uhandisi wa viwanda, na amepata kufanya kazi katika mashirika mbalimbali humu nchini Tanzania. Kafanya kazi pia Zambia, India na hata Italia – Ulaya kwa Wazungu.


Basi, ninachukua maelezo yake kama mzalendo na mlilia maendeleo ya kweli kwa wananchi wake. Amelinganisha na huko ughaibuni akaona kuna tofauti kubwa sana kifikra, kiutendaji, kiutamaduni na kimazoea katika maisha ya watu weusi wa nchi huru hizi za Afrika.


Maelezo, utafiti na matokeo ya kazi yake hii yameshabihiana sana na maelezo niliyowahi kuyasoma katika kitabu cha Mzungu mmoja, Profesa Mfaransa anaitwa RÉNE DUMONT kinachoitwa “False Start in Africa”. Kitabu kilielezea zaidi hali ilivyokuwa katika nchi za Afrika Magharibi. Huyu profesa kitabu chake kilitoka mwaka 1966. Maudhui ya kitabu kile na maudhui ya kitabu hiki cha Bundara yanashabihiana mno, utafikiri walishirikiana kuandika.


Wote wawili wametaja sababu zinazowafanya Waafrika weusi katika bara letu, tusiendelee kiuchumi licha ya kuwa nchi zetu zote ni tajiri na huru baada ya kutawaliwa na wakoloni Wazungu – Wafaransa, Waingereza, Wareno na Wabelgiji.


Hali ya maisha kwa ujumla wake ni duni sana. Wakoloni walijaribu kutubeba miaka kadhaa baada ya Uhuru wa nchi zetu kati ya miaka ya 1960-1970, lakini hali ya wananchi wengi katika bara hili “jeusi” inazidi kudidimia. Wataalamu hawa, Réne Dumont na Malima Bundara, wametoa sababu gani au zipi zinazofanya nchi zetu za Waafrika weusi kuwa duni?


Kisingizo kikubwa kinachotolewa na viongozi wote katika nchi zetu hizi ni kile cha KUTAWALIWA NA WAGENI WAZUNGU yaani UKOLONI. Kingine ni ile hali ya UTUMWA iliyosababishwa na hao hao wageni Wazungu na Waarabu. Ati kutokana na hayo mawili nchi zetu huru za Afrika zimenyonywa sana utajiri wao na hivyo zimeachwa hohehahe, ndiyo sababu tu maskini, si hivyo tu, bali zimekumbwa na baa la mara kwa mara la njaa na zimekumbwa na magonjwa chungu nzima, hali namna hiyo nayo inatufanya tubaki kuwa masikini.

 

Hawa wasomi wawili wanasema katika miaka yote hii ya Uhuru, kwa nini Waafrika wenyewe tusijitutumue na kupiga hatua? Wanatoa mifano kama nchi ya India ilitawaliwa na mkoloni, lakini baada ya Uhuru wake mwaka 1947, ilipofika mwaka wa 18 wa Uhuru wake (1965), ilikuwa imebadilika sana kiteknolojia, na hivi leo si nchi ya Dunia ya Tatu tena, bali ni li-nchi la kushindana na nchi za Ulaya! Wanasema Ghana (iliyokiitwa Gold Coast) ilipata Uhuru wake mwaka 1957 ikiwa na kipato kikubwa (per capital income) kwa kila mtu kupita kipato cha kila mtu kule Korea Kusini siku hizo.


Hivi leo Ghana bado duni kimapato na inaomba misaada kutoka Korea Kusini – nchi iliyoendelea kweli kweli hivi sasa. Hapa kwetu Tanzania tulipopata Uhuru mwaka 1961, mishahara yetu enzi zile ilikuwa inatutosheleza. Mimi nilikuwa Mwalimu Afisa Elimu Daraja la III, nikipata Sh. 820 kwa mwezi.


Lakini zilikuwa nyingi hizo, zikitosha kula kwangu na mahitaji karibu yote muhimu na masazo nikiweka benki ikiitwa The Standard Bank of South Africa mjini Songea. Kima cha chini kilikuwa Sh. 145 tu na wengine wakipata Sh. 280 kwa mwezi.  Lakini bila kutia chumvi fedha zile jamani zilitutosha.


Kwa hali ya maisha ya siku zile mishahara yetu ilitosheleza na tukiishi kwa raha mustarehe. Leo hii, mishahara inaanzia malaki na inakomea mamilioni, lakini haitoshi ng’o! Kila kitu bei juu, thamani ya fedha imeporomoka sana. Sasa hata ukipata hivyo vi-laki – ukilinganisha na gharama za leo – chakula, usafiri, kodi ya nyumba unashtukia baada ya wiki moja tu kale kamshahara kote kameyeyuka! Imekuaje hali namna hiyo?


Kilio kikubwa katika nchi karibu zote za Waafrika weusi ni “Umaskini uliokithiri na hali ngumu ya maisha”.  Miundombinu yote iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni, nyumba nzuri na safi sasa yameharibiwa na kuwa kama magofu tu. Angalia zile nyumba za Serikali kwa watumishi Waafrika kule Ilala, Magomeni na Temeke Mwisho tukijivunia kama “African Urban Quarters”, leo hii ni magofu ya kubomolewa. Hazifai kuishi mtu (condemned buildings). Ni nyumba hatarishi! Inakuwaje tushindwe hata kutunza kile tulichoachiwa na Wazungu?


Basi, wataalamu wetu wachambuzi hawa wawili wanapotafakari kwa nini Waafrika weusi hatuendelei, wanakuja na maelezo mbalimbali. Dumont anasema kwanza kabisa kinachotuharibu Waafrika weusi ni kuweka mkazo potofu kwa miradi katika nchi changa, namnukuu; “Any policy which prides itself on its social orientation in a backward country is sacrificing the hope of increasing production in order to gain immediate satisfactions…” (False Start in Africa, chapter III pg 48).


Hapa inaonesha fedha za misaada kutumika katika huduma za kitaifa kwa maana viongozi walitaka kuonesha maendeleo ya haraka haraka, lakini fedha zile hazikuzalisha! Hivyo uchumi wa nchi haukukua. Misaada ilipokoma hapo ndiyo ilipokuwa mwisho wa mafanikio. Majengo ya huduma yakibaki bila kutumika na wala hakukuwa na mtaji wa kulipia wahudumu kwenye miradi ile, ndiyo sababu umaskini haukupunguka kwa misaada. Miradi ilikufa na majengo kubakia magofu (white elephants).


Pili, Dumont anasema Waafrika walipenda sana anasa. Wakoloni waliwazawadia Waafrika ulevi au vinywaji vya Kizungu kama njia ya starehe, na Waafrika wakafikiri kilevi cha Kizungu kingewawezesha kukubalika upesi miongoni mwa Wazungu. (False Start in Africa pg 48 paragraph 2).

Sijui wangapi tunakumbuka pale Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokataliwa kupewa bia katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam miaka ile ya 1950! Na hata baada ya Uhuru, viongozi watatu wananchi wa Dar es Salaam walikataliwa kupewa bia hapo Palm Beach Hotel mwaka 1962.

 

Ulifika wakati viongozi wetu wa siasa, moja ya madai yao kabla ya Uhuru ni hilo la kuruhusiwa nao kunywa bia, yaani pombe ya Kizungu ilimradi nao wajisikie. Huu ni ulimbukeni.

1422 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!