Sitta-KiapoMwanasiasa wa siku nyingi, Samuel Sitta, ametangaza nia ya kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuna sentesi maarufu ya: “ni haki yake ya kikatiba.” Sawa, ni haki yake, lakini hata sisi wananchi tuna haki ya kutoa maoni yetu.

Mzee Sitta (73) alizaliwa Desemba 18, 1942.

Amekuwa Mbunge kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1995. Ameshakuwa Waziri wa wizara mbalimbali, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005-2010) na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Umri wa Mzee Sitta, si hoja sana kwa sababu hata sisi tunaomkosoa, Mola akitujalia maisha marefu tutakuwa wazee kama yeye. Wala sitaki kuutumia uzee wake kama kigezo cha haya niliyokusudia kuyaeleza hapa.

Mwaka 2005 nilikuwa miongoni mwa tuliomuunga mkono Mzee Sitta kuwania kiti cha Spika. Pamoja na kigezo cha umri, kwa wakati huo alionekana mtu sahihi ambaye angeweza kufanya kazi hiyo kwa kasi na kwa viwango kama alivyojinasibu.

Spika wa wakati huo, Mzee Pius Msekwa, mapema alishatangaza kutowania nafasi hiyo mwaka 2005. Kauli yake ikatoa mwanya kwa wananchi kuanza kutafakari jina la nani angeweza kuziba nafasi.

Ghafla Mzee Msekwa, akabadili mawazo. Akatangaza kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingi, licha ya ukweli kwamba amekuwa mtumishi wa Bunge tangu mwaka 1960! Hoja yake ikawa kwamba kwa vile nchi ilikuwa inampata Rais mpya, Waziri Mkuu mpya, wabunge wengi wapya, lingekuwa jambo la busara kama angeendelea kuwa Spika ili kuisaidia Serikali mpya!

Hoja yake ikawa haina mashiko. Wapo waliomshauri aachane na mpango wa kuwania nafasi hiyo, lakini utamu wa madaraka ukamsukuma au ukampofusha hata akakosa kuona hatari ya aibu ya kushindwa iliyokuwa dhahiri.

Akaingia kwenye mchuano. Sitta akamshinda kwa aibu kubwa. Huo ukawa mwanzo wa heshima ya Mzee Msekwa kutetereka.

Mwanasiasa mwingine, John Samuel Malecela, akiwa Mbunge wa Mtera, na mtu aliyeshika nyadhifa nyingi hadi ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naye kwa kupuuza ushauri wa wananchi, akajikuta akichuma aibu.

Akiwa ameshatangaza kuwa mwaka 2005 ndiyo ungekuwa mwaka wake wa mwisho kuwatumikia wana Mtera kwa nafasi ya ubunge, akajikuta akikolewa na utamu wa Bunge na hivyo akaingia ulingoni mwaka 2010. Akapambana na Livingstone Lusinde, kijana mdogo ambaye mara zote amekiri kuwa hata hakufanikiwa kuhitimu vema elimu yake ya msingi. Kwenye kura za maoni, Lusinde akambwaga kwa aibu kubwa Mzee Malecela, na huo ukawa mwanzo wa kuporomoka kwa heshima ya kiongozi huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa Tanzania, Afrika na duniani kwa jumla.

Matukio ya “wazee” kuaibishwa kwa sababu tu ya tamaa za madaraka ni mengi, na kwa kweli hakuna dalili zozote za kuonyesha kuwa kuna wanafunzi (wazee wengine) wanaofaulu somo hilo.

Sitta, anatangaza nia yake ilhali akiwa na kumbukumbu njema ya wiki mbili hivi ya kuangushwa kwa mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira kwenye ubunge.

Wasira, alionywa na watu waliompenda asigombee ubunge Jimbo la Bunda. Kulikuwa na sababu nyingi za kumtaka apumzike. Ukiacha ile ya ukweli kwamba amekuwa kiongozi kwa miaka mingi, alipaswa kukubaliana na takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba waliokuwa wamejiandikisha kwa wingi ni vijana.

Alipaswa kutambua Bunda kuna vijana wengi kama ilivyo kwenye miji mingine nchini. Vijana wanazungumza “lugha moja” ya mabadiliko kwa hiyo ingekuwa vigumu sana kwake kuwavutia vijana wanaoimba wimbo huo.

Tena basi, Mzee Wasira alipaswa atafakari kwa kina kweli kweli kibwagizo cha Makongoro Nyerere, cha “Yupo Tu” alichokitumia wakati wa mchuano wa kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Ingawa maneno ya Makongoro yalionekana mepesi, lakini ujumbe wake ulikuwa mkali na wa kweli. Sijui, lakini nadhani kauli ya “Yupo Tu”, itakuwa ilisaidia kuamsha hamasa kwa vijana na wananchi wa Bunda kumwangusha Mzee Wasira maana tangu enzi za Mwalimu Nyerere yupo tu uongozini.

Wote waliomshauri akawapuuza. Tena basi, hata chama chake nacho hakikuwa na ujasiri wa kulikata jina lake pengine kwa hofu ya kuibua mpasuko. Akaachwa aogelee mwenyewe. Kilichomkuta hakiwezi kuondoka kwenye fikra zake kwa kipindi chote cha uhai wake.

Sasa amekuja Mzee Sitta. Tulidhani aibu iliyowafika wenzake ingetosha kuwa somo murua kwake; lakini imekuwa tofauti. Kwa mara nyingine anataka apitishwe na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili aweze kushindana, na bila shaka yoyote ile, ashinde kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwenye maelezo, hoja anazozitumia kuhalalisha matamanio yake ni kama zile zile za Mzee Msekwa za mwaka 2005.

Ukweli wa kisayansi unathibitisha kuwa umri mkubwa unampunguzia binadamu uwezo wa kufikiri na kutenda. Kadri umri unavyokuwa mkubwa binadamu anapungukiwa mbinu mpya za kukabiliana na mazingira ya wakati huo na hata kwa wakati ujao.

Umri wa miaka 73 kwa Mzee Sitta, ulitosha kumfanya apumzike, na abaki kufaidi matunda ya utumishi wake wa muda mrefu kwa Taifa lake.

Kasi ya mabadiliko ya dunia hii ya sayansi na teknolojia haimpi fursa tena ya kuongoza kizazi hiki. Sana sana alichobaki nacho ni rejea ya mambo ambayo kama ilivyo kwa wazee wengine, wanachokumbuka mara zote ni kile walichokifanya enzi zao.

Sijathibitisha, lakini naweza kuamini kuwa Mzee Sitta, kama wazee wengine wa umri wake, hana uwezo wa kutosheleza kuendana na mabadiliko ya sasa katika ulimwengu huu wa mitandao. Kama hilo analiweza, basi ni kwa kiwango kidogo.

Mzee Sitta, alithibitisha pasi na shaka namna alivyoanza kuchoka pale alipoongoza Bunge Maalumu la Katiba. Kwa kujua, au kwa kutojua, alihakikisha anasimamia kuondolewa kwa mambo mengi mazuri yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Alihakikisha mambo mengi ya maana yanaondolewa kwenye Katiba inayopendekezwa, na kwa maana hiyo akawa ndiye injini ya kuanzishwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa umekuwa mwiba mchungu kwa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Kama si Mzee Sitta, Ukawa usingekuwapo, na kwa maana hiyo CCM isingepata wakati mgumu.

Litakuwa jambo la ajabu na aibu kwa Chama Cha Mapinduzi kumpitisha mtu huyu huyu aliyesababisha kitaabike kwenye Uchaguzi Mkuu.

Ukiacha hilo, sasa tuna uongozi wa Awamu ya Tano katika nchi yetu chini ya Rais John Pombe Magufuli. Dk. Magufuli wakati wote wa kampeni aliwaahidi Watanzania Mabadiliko ya Kweli. Ingawa hakulisema hilo moja kwa moja, bila shaka miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuondokana na sura za miaka yote za watu aina ya Mzee Sitta kwenye uongozi wa nchi.

Sisi tulioko huku mitaani tunawasikia wananchi wanavyozungumza. Miongoni mwa mambo wanayoomba Rais Magufuli, ayashughulikie ni hili la kuziweka kando sura ambazo kwa kweli zimekuwa kama sehemu ya msamiati kwenye kitabu cha uongozi wa Tanzania.

Watu wa umri wangu tumemsikia Sitta tangu tukiwa shule za awali. Tumesoma shule za msingi na kuhitimu. Tumeingia shule za sekondari, tumejiunga vyuo na hatimaye tumeajiriwa na kujiajiri. Tumefanya kazi kwa miaka mingi, kiasi cha sasa kuwekwa kwenye kundi la “wakongwe”. Muda wote huu, Sitta yupo tu.

Ana lipi jipya la kuwaletea Watanzania ambalo hakuweza kulitenda kwa kipindi chote alichokuwa mbunge? Ndiyo maana tupo tunaohoji, ni kitu gani ambacho Sitta kakiacha ndani ya Bunge, na sasa anataka akichukue?

Kama nilivyosema hapo awali, Watanzania wanahitaji mabadiliko. Mabadiliko ya kweli yanapaswa yaendane na sura tofauti kwenye nafasi ya uongozi, ukiwamo uspika. Mzee Sitta, aingie kwenye klabu ya wenzake ili wawe washauri nje ya uongozi.

Tumeona Sitta alipokuwa Spika, aliweza kujenga Ofisi ya Spika jimboni kwake Urambo kana kwamba huko ndiko makao makuu ya Bunge. Hilo ni tukio lisilo la kawaida, na pengine linathibitisha kuwa alishajiandaa kuwa Spika wa maisha wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wazee aina ya Sitta si wa kuwa katika Awamu ya Tano ya Dk. Magufuli, kwa sababu bado wanaweza kuendeleza mambo yale yale ya mitandao ambayo kwa bahati nzuri Rais wa sasa hana kabisa.

Uchaguzi Mkuu uliomalizika tulidhani ungeweza kuwa ndiyo kaburi la Mtandao ule uliovuma mwaka 2005; lakini kwa kujitokeza watu aina ya Mzee Sitta, tusitarajie kufa kwa mtandao huo.

Huyu bado ana mtandao ambao unaamini unapaswa kujimaarisha ili kama si mwaka 2020, basi 2025 uweze kushika uongozi wa nchi.

Kwa kuwa nchi sasa iko mikononi mwa Dk. Magufuli, ni wajibu wake kuhakikisha anajitahidi kuvikwepa vimelea vyote vya mitandao ambavyo vikiendelea kustawi vitamsumbua kwenye uongozi wake wa miaka hii mitano.

Lakini Sitta ana sifa nyingine ya ziada. Anapenda sana “kuwafurahisha” wabunge, hasa kwenye suala la mishahara, posho na marupurupu. Ukimsikiliza Rais Dk. Magufuli, mpango wake mkuu ni kuhakikisha watumishi wote wa umma wanalipwa vizuri, lakini sidhani kama atakuwa tayari kuona wabunge tu ndiyo wakijipendelea.

Endapo Sitta atataka apendwe, njia ya mkato kwake ni kuongeza marupurupu. Hili alishathubutu wakati akiwa Spika, na likazua mvutano mkubwa kati yake, Serikali na wananchi.

Kwa hiyo Dk. Magufuli, akae tayari akijua kuwa Sitta akiwa Spika, atakachofanya ni kufanya hayo yaliyoshindikana wakati huo ili apendwe na wabunge, na kwa kuwa Serikali itakuwa haijapata uwezo wa kuwaridhisha watumishi wa umma wote kwa mishahara minono, Dk. Magufuli atagoma kuidhinisha. Akishagoma tu, basi Sitta anaweza kumwibulia zengwe zito hata la kupigwa kura ya kutokuwa na imani naye. Kwa ufupi, Sitta ni wa kuogopwa kwenye suala hili la uspika.

Akubali kuwa umri umeshamtupa mkono. Ametumikia awamu zote nne za uongozi wa Taifa letu. Awamu hii ya Tano ajiweke kando. Apishe nguvu na akili mpya ziweze kuijenga Tanzania mpya.

Kwa namna ya kipekee na kwa unyenyekevu namuomba Mzee Sitta, aache mpango wake wa kuwania uspika kwa sababu mbili: Mosi, umri wake umemwezesha kulitumikia Taifa hili kwa nafasi nyingi. Mchango wake kwenye uongozi umetosha. Abaki kuwa mshauri tu kwenye klabu ya wastaafu wenzeke.

Pili, aina yake ya uongozi inaweza kulivuruga, si Bunge pekee, bali Serikali yote ya Dk. Magufuli kwa sababu bado anaamini kama si yeye, basi kwenye mtandao wake wapo wanaostahili kuanza kujiandaa kuongoza Awamu ya Sita. Atakachokifanya Mzee Sitta ni maandalizi ya Awamu ya Sita. Mzee Sitta imetosha. Pumzika. Usichume aibu.

 

0759 488 955

2133 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!