Seif_hamad(17)Wagombea wa urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wameikaba koo Serikali.

Licha ya vikao kadhaa na viongozi wa Serikali, wote kwa pamoja hawakubaliani na matakwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachofurahia kurudia Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar baada ya Jecha Salim Jecha ambaye ni Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Maalim Seif, ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, ameliambia JAMHURI kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi huo na kwamba baraka hizo pia wamezipata kutoka kwa Lowassa.

Maalim Seif aliyetea na Lowassa mwishoni mwa wiki kwa zaidi ya dakika 90, anasema CUF haina wasiwasi na msimamo wake ingawa inafahamu kuwa baadhi ya vyama vya siasa vitajitokezaa kushirikiana na CCM kwenye uchaguzi huo kubariki dhana ya vyama vingi.

“Tamko letu ni msimamo ambao ni kutoshiriki uchaguzi huo. Na ndugu yetu Bwana Lowassa ameridhia. Kwa hiyo, tuna msimamo wa kukataa kurejewa uchaguzi. Hilo halikubaliki,” anasema Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ.

Maalim Seif ameliambia JAMHURI kuwa “Ninachokiona CCM hawakujiandaa kuwa chama cha upinzani. Sisi kwa miaka yote tulijindaa na nilikuwa nakubali kushindwa… Kosa liko wapi kusema kwamba wananchi wameamua niongoze Zanzibar mwaka huu?” anahoji Maalim Seif.

Anasema miaka yote Katiba na marekebisho ya Katiba yamefanywa na Serikali iliyopo chini ya CCM; “Bila shaka hawakufahamu kwamba ipo siku watakuwa wapinzani…

“Sasa wanaacha kutangaza mshindi, wanageuka na kusema kurudia uchaguzi. Kwa dosari gani? Safari hii upande mmoja wa Bara utaongozwa na Upinzani. Lowassa naye kasema, basi uchaguzi wa Bara nao urudiwe. Haya ndiyo tuliyokubaliana.”

Anasema kinachofanywa na CCM ni kudhibiti kusitokee upande mmoja ukaongozwa na Upinzani, jambo ambalo ridhaa ya wananchi haiko hivyo katika nchi inayoheshimu na kuitekeleza demokrasia.

Anasema kwamba katu hatayaachia matokeo yake akishutumu kwamba CCM iliwekeza akili kwenye uchaguzi wa Muungano, na kusahau Zanzibar ambako yeye anadai ameshinda.

Anasema Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba iliandaa rasimu mbili nzuri ambazo moja waliitoa Juni 3, 2013 na nyingine Desemba 31, mwaka huo, lakini kwa mujibu wa Maalim Seif, “zilipuuzwa.”

Rasimu hizo zilipendekeza muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, na Maalim Seif anasema, “CCM walikataa na hata Katiba ambayo hata haikwenda kwa wananchi. Haina mapendekezo ya Jaji Warioba.”

Moja kwa moja Lowassa anaunga mkono msimamo wa Maalim Seif, kupinga kabisa kurejewa Uchaguzi Mkuu Zanzibar, mapema mwakani kama ambavyo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza baada ya kufuta matokeo.

“Seif atangazwe mshindi mara moja,” anasema Lowassa huku akisifu kwamba mwanasiasa huyo wa visiwani Zanzibar anastahili pongezi kwa ustamilivu na busara.

“Wakuu wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi ule ule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na urais Tanzania, lakini batili kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar. Dhana hii haina mantiki yoyote bali ni ubabe wa kisiasa tu.

“Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja. Hali si shwari nchini licha ya ukimya wa wananchi. Wananchi bado wanauguza makovu ya matokeo batili ya uchaguzi yaliyotangazwa na NEC,” anasema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), Profesa Abdallah Safari, anasema kwamba kinachoendelea Zanzibar hasa upande wa CCM ni hofu ya madaraka.

“Tunasubiri kwa hamu faraja ya Maalim Seif kutangazwa mshindi. Na hili CCM linawauma,” anasema Prof Safari na kuongeza:

“Ukawa, unaoundwa na vyama vinne vya siasa vya NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chadema wanasubiri ushindi mkubwa wa Zanzibar. CCM hawataki kukiri kuwa wameshindwa ili mshindani wao CUF aachiwe Ikulu. Unajua… kwa mujibu wa sheria na taratibu, Rais huyo wa SMZ atakuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri litakaloundwa na Dk. Magufuli wa CCM, eeh,” anasema.

Ibara ya 54 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia Baraza la Mawaziri na Serikali: “Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na mawaziri wote.”

Anasema CCM hawakujua kama siku moja watakuwa wapinzani na kwa hali halisi mambo yote yatakayozungumzwa na kujadiliwa ndani ya Baraza la Mawaziri CUF watayasikia kwa Maalim Seif kuwamo. “Hofu ya CCM ni kufahamika kila kitu.”

Profesa Safari anasema CCM ina hofu ya mabadiliko ya Katiba kwani katika historia tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Rais wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba alikuwa Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasema hali hiyo iliendelea hadi mwaka 1985 ambako Zanzibar ilitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano huku Makamu wa Rais akitoka Tanganyika. Anasema marekebisho ya Katiba yaliyosababishwa na mfumo wa vyama vingi kulianzishwa nafasi ya Mgombea Mwenza.

Miaka yote tangu mwaka 1995, Rais amekuwa akitoka upande wa Bara na Makamu amekuwa akitoka Zanzibar.

Mwaka 1995, Rais alikuwa Benjamin Mkapa na Makamu wake alikuwa Dk. Omar Ali Juma. Baada ya kifo cha Dk. Omar, nafasi hiyo ilichukuliwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

Wakati Jakaya Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, Dk. Shein aliendelea kuwa Makamu wake, na aliporudi tena mwaka 2010, alimchukua Dk. Mohamed Gharib Bilal. Dk. Shein alichaguliwa kuwa Rais wa SMZ.

Kada mmoja wa CCM kutoka Mkoa wa Dar es Salaam anasema kwa sasa wameshindwa kujipanga zaidi kwa ajili ya kukinusuru chama hicho, ambacho kimekwishameguka vipande zaidi ya vitatu kutokana na nguvu kubwa waliyokuwa nayo wapinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Anasema Lowassa bado ana mtandao mkubwa ndani ya CCM, na sasa haijulikani ni kitu gani kitajitokeza kwa siku chache zijazo. Serikali inafanya kila jitihada kutafuta mikakati yote inayoendelea ndani ya Ukawa hasa mipango yao baada ya uchaguzi wa mwaka huu uliojaa changamoto nyingi.

“Tumetafuta mbinu nyingi za Lowassa tumeshindwa zaidi ya kuona mke wake, Regina Lowassa akijiengua miongoni mwa wabunge wa Viti Maalum waliokuwa wamependekezwa na Chadema,” anasema.

Regina, ambaye awali hakuwa na rekodi ya siasa za majukwaani na hakujitokeza hadharani alipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari hii aliamua kuonesha uwezo wake wa kisiasa kwa kumpigia kampeni mumewe, Lowassa, aliyekuwa akiwania urais kupitia Chadema akiungwa mkono na Ukawa.

Kabla ya kukataa nafasi hiyo, gazeti hili lilikuwa la kwanza kuufahamisha umma juu ya mipango ya Chadema kupitisha jina la Regina Lowassa ikiwa ni hatua ya kumtunuku nafasi ya ubunge wa Viti Maalum kutokana na mchango wake mkubwa wa kisiasa alioutoa wakati akiwapigia debe wagombea wa Ukawa kipindi cha kampeni.

Uamuzi huo uliungwa mkono na wajumbe wote wa kikao cha Kamati Kuu lakini baada ya wajumbe kuwasiliana naye na kumjulisha kuhusu suala hilo, inaelezwa kuwa alishtushwa na taarifa hizo ambazo hakuwa na mamlaka ya kuzipinga kutokana na msimamo wa wajumbe wa kikao hicho.

Hata hivyo, baada ya siku chache aliikataa nafasi hiyo aliyopewa na Kamati Kuu ya chama chake kwa nia njema ya kuthamini mchango wake mkubwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, huenda akatangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika Februari 6, mwakani.

Tayari Jecha ametangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN) la Novemba 6, mwaka huu, kuwa amefuta matokeo ya Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 hivyo kinachofuata ni kutangazwa kwa tarehe rasmi ya uchaguzi.

Jecha alifuta uchaguzi huo kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa akidai kuwa Maalim Seif, alijitangaza mshindi katikati ya mchakato wa kuhesabu kura uliokuwa ukifanywa na ZEC.

Vyama 14 vya siasa vilishiriki Uchaguzi Mkuu, lakini ushindani wa dhati ulikuwa kati ya CCM na CUF ambayo katika chaguzi nne zilizopita, kimekuwa kikitoa upinzani mkali.

By Jamhuri