IMG_1708Mgogoro mkubwa umeibuka ukiwahusisha wafanyabiashara ya uwindaji wa kitalii na Serikali.

Chanzo cha mtafaruku huo ni uamuzi wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, siku chache kabla kuachia ofisi, kufuta Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2010 na kutunga Kanuni mpya.

Kanuni hizo mpya ambazo hazikuwashirikisha wadau zimeshaanza kutumika kupitia Tangazo la Serikali Na. 414.

Nyalandu alihakikisha anatunga Kanuni mpya Septemba 18, mwaka huu akitambua kuwa hakuna wa kumhoji kwa kuwa Bunge lilikuwa limeshavunjwa.

Wataalamu wa sheria katika Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekiri kushinikizwa kuandaa Kanuni hizo ambazo zinakinzana moja kwa moja na vifungu katika sheria mama.

Kwa kanuni mpya, wawindaji wanaruhusiwa kuchukua kila kitu kutoka kwa mnyama waliyewinda kisheria, isipokuwa nyama.

Kwa uamuzi huo, Kanuni mpya zinakinzana na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo tafsiri ya “neno” nyara inahusisha pembe, meno, mifupa, kwato, ngozi, nywele, manyoya, nyama na sehemu nyingine zote za mnyama.

Uamuzi wa sasa unawaruhusu wawindaji, kuchukua kila kitu wanachokitaka kutoka kwenye mnyama waliyemwinda, isipokuwa nyama.

Kifungu cha 3 cha Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kinaihusisha “nyama” kama nyara, lakini Kanuni zilizotungwa na Nyalandu Septemba 18, 2015 ambazo zimefuta Kanuni za mwaka 2010 zinaiondoa nyama kwenye orodha hiyo.

“Hakuna mahali ambako Kanuni imeweza kuwa juu ya sheria. Nyara hizi zinakuwa zimelipiwa mamilioni ya fedha, ni uamuzi wa mwenye kibali cha kuwinda kuamua nyama anaila, anaitupa au anafanya anavyojua. Uamuzi wa Kanuni mpya unaiondoa nyama kwenye orodha ya nyara, lakini pia hazielezi hiyo nyama ifanywe nini…itupwe, igawiwe kwa wananchi, ipelekwe serikalini au iwe vipi.

“Sheria haijabadilika, ndiyo tunayoifuata hadi sasa, lakini Kanuni zilizotungwa na bwana mkubwa (Nyalandu) sasa zinakinzana na sheria mama…uliona wapi haya mambo?” Amehoji mmoja wa wafanyabiashara hao.

Kwa uamuzi huo, baadhi ya wageni waliofika nchini kuwinda wameshindwa kusafirisha nyama licha ya kufuata sheria zote kwa kufanya malipo halali na kupata vibali kutoka mamlaka husika.

Pia Kanuni mpya zimelenga kumpa madaraka makubwa zaidi Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii, yakiwamo ya kuhakikisha kampuni asiyoitaka, haipati kitalu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kukwamishwa usafirishwaji wa nyama nje ya nchi licha ya wahusika kupata vibali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Miongoni mwa waliokwama kusafirisha ni Sheikh Hamdan bin Mohamed, wa Falme za Kiarabu aliyekwama kusafirisha kilo 350 za nyama licha ya kuwa na kibali kutoka Kituo cha Ukaguzi cha Arusha.

 

Wenye vitalu ‘wazawadiwa’

Katika hatua nyingine, Nyalandu kabla ya kuondoka katika Wizara hiyo, ameshafanya mipango ya kuwaongeza muda wa uwindaji wamiliki wa vitalu vya uwindaji.

Barua yake ya Agosti 13, mwaka huu kwenda kwa wawindaji hao, inawapongeza kwa “kuzingatia kwao masharti ya uwindaji”, na kwa sababu hiyo, anamhakikishia kila mwenye kitalu kwa kusema: “Ukiendeleza utendaji huu, moja kwa moja kampuni yako itakuwa imefuzu kupata kibali cha umiliki wa kitalu kwa mwaka 2018-2022.”

Kwa kawaida umiliki wa vitalu kisheria ni miaka mitano, ambako baada ya kuwa umeisha, mmiliki hukirejesha serikalini na kutangazwa ili kishindaniwe na watu wengine wenye nia ya kuwekeza kwenye tasnia ya uwindaji wa kitalii.

Pamoja na ahadi hiyo, tayari Nyalandu amebainika kugawa kitalu kwa kampuni za rafiki zake Wamarekani katika eneo la Lake Natron. Amefanya hivyo baada ya kumnyang’anya mmiliki ambaye ni Mtanzania.

Ugawaji huo haukufuata taratibu za kisheria ambazo zinaagiza tangazo litolewe na waombaji washindanishwe kwa vigezo vilivyo wazi.

“Barua ya Nyalandu ya Agosti 13 ya kuwahakikishia wamiliki wa vitalu kuendelea kuvimiliki mwaka 2018-2020 ilikuwa na malengo mahsusi. Haikuwa barua ya kawaida kwa sababu iliambatana na kuwataka wenye vitalu watoe fedha ambazo alisema zililenga kuisaidia CCM kwenye Uchaguzi Mkuu.

“Ilikuwa ni barua ambayo aliyepewa aliisoma, akafurahi, lakini mwisho akaombwa asaidie CCM. Nakuhakikishia wapo waliotoa mamilioni ya fedha, lakini wengine walikataa. Mimi ni mmoja wa watu tuliokataa kutoa fedha. Nilihoji iweje ahadi hiyo iambatane na utoaji fedha?

“Hapo wenye akili tukajua hii barua ilikuwa chambo tu, lakini mpango mahsusi ulikuwa wa kujipatia fedha tulizoambiwa ni za kuisaidia CCM. Tulisita kwa sababu tangu mwanzo tulijua Magufuli (Dk. John Magufuli) hakuwa na mpango wa kuwachangisha wafanyabiashara kuingia Ikulu, na ndivyo alivyofanya,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa za uhakika zinasema Nyalandu amewahakikishia wamiliki hao wa vitalu kwamba wasiwe na shaka yoyote na masuala yao kwa kuwa ana hakika atarejea kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.

Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ilipitishwa na Bunge baada ya kulalamiko ya miongo mingi kutoka kwa wafanyabiashara Watanzania.

Kwa miaka mingi, vitalu ambavyo ni biashara uenye ukwasi mkubwa vimekuwa vikilimikiwa na wafanyabiashara wa kigeni bila kuviachia. Hatua hiyo ilililazimu Bunge kupitisha sheria iliyosaidia kuwafanya wazawa wengi waweze kushiriki biashara hiyo.IMG_1708

By Jamhuri