Polisi waomba Kitwanga, IGP wawanusuru

Charles   Kitwanga,  Naibu Waziri Nishati na Madini  (M)Baadhi ya askari polisi katika maeneo mbalimbali wamewaomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu kuingilia kati kuwanusuru na unyanyasaji wanaofanyiwa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs), wanaowahamisha vitengo kwa uonevu.

Wakati wakieleza kuwa IGP Mangu ametoa agizo askari wapanguliwe kwa baadhi kutolewa Trafiki na Upelelezi kwenda General Duties, askari wanaodaiwa kuwa wala rushwa wakichafua sura ya Jeshi la Polisi, Mangu ameliambia JAMHURI kuwa kinachofanyika ni uhamisho wa kawaida na wala hajatoa agizo la aina hiyo.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI, zinasema katika safishasafisha ndani ya Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wasiofanya kazi kwa uadilifu wanaondolewa, kumejitokeza uonevu mkubwa kwani askari wachapakazi ndio wanaoondolewa na wenye maadili yanayotiliwa shaka wanabakizwa kwenye vitengo.

“Wengi tumehamishwa kutoka traffic kwenda general duties. Wala sisi hatulalamiki kuhamishwa, ila tunalalamika kuhamishwa watendaji bora na kuacha wanaonuka rushwa au wenye udugu na wakubwa. Na hili linafanywa na ma-OCD wanaopendekeza majina kwa ma-RPC kisha ma – RPC wakafanya uamuzi,” anasema mmoja wa maaskari waliohamishwa.

Kilio kama hiki JAMHURI imekipata kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo askari wanasema maagizo ya IGP yametumiwa na wachache wenye chuki kukomoa askari wanaogoma kutekeleza maagizo ya ma-OCD yaliyo kinyume na sheria.

“Tayari kuna malalamiko mengi na mengine yamefika mezani kwa IGP, tukieleza uhamisho ulivyotumika kukomoana. Tunaamini IGP akiingilia kati maana mafaili yapo mezani kwake, tunaweza kupata ufumbuzi wa haki katika suala hili. Inaumiza na kukatisha tamaa,” alisema askari mwingine anayesema yeye hakuguswa na uhamisho huo isipokuwa marafiki zake.

JAMHURI lilipowasiliana na IGP Mangu, alisema: “Hatuhamishi watu, watu wanabadilishiwa majukumu. Na ni utaratibu wa kawaida, wala hauhitaji ceremony au hauhitaji, utaratibu, sijuhi mpangilio. Hauhitaji, kwa sababu hakuna mtu aliyeairiwa polisi akatakiwa afanye kazi ya traffic au general duty. Aliajiriwa polisi kufanya kazi ya upolisi tu. Kwa hiyo hakuna permanent section kwenye utendaji. Kwa hiyo siyo issue.

“Kama kuna fulani kaachwa ni mbaya, tujue ubaye wake tumshughulikie. Yaani haihitaji kuwa ni issue general ikaripotiwa tu hivi hivi. Kwa sababu haya ni mambo yanayohitaji uthibitisho kwamba kama kuna OCD mmoja ameacha watu wabovu na ubovu wao unajulikana, akachukua watu wazuri, tupatiwe taarifa, tumshughulikie.

“Lakini pia sisi tunajua hayo ni malalamiko ya askari, kwani askari hawataki kutoka kwenye hivyo vitengo, wanavyoita vitengo wao, ndiyo maana wanakuja huko kwenu. Lazima tukubali kujenga hii nchi… kama kuna askari ni wala rushwa, wameguswa mahali wanapiga kelele… sasa kama kweli ameonewa si kuna utaratibu wa kulalamika ndani ya Jeshi la Polisi kwa nini aje kwenu?

“Wale waliokupigia simu ni wale askari ambao, hawataki kutoka kule trafiki, ehee. Na mimi pia nasema kama ni kweli, kwa sababu hata ma-OCD wangu inawezekana wapo wabovu, kama kweli wapo, tupate hizo taarifa kwa utaratibu unaoeleweka wala sisi hatuna OCD ambaye naye amegeuka Mungu mtu. Tutamshughulikia kama yule askari ambaye tumembadilishia majukumu yake. Na yeye tunamuondoa kwenye huo u-OCD tunampeleka majumu tofauti,” anasema Mangu.

IGP Mangu amesema amejipanga kuhakikisha jeshi la polisi linakuwa la kisasa, linalofanya kazi kwa uadilifu bila kuonea askari wala raia au askari kuonewa na viongozi wao, hivyo akaomba iwapo kuna askari anayeamini kumetokea uonevu amfikishie hilo kwake mara moja na litapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga kwa upande wake alisema wanaoweza kuwa na majibu sahihi juu ya suala hilo ni makamanda wa mikoa, ambao ndiyo wenye jukumu la kufanya uamisho huo baada ya kupata ushauri kutoka kwa ma-OCD, na yeye kama Mkuu wa Kikosi anapewa nakala ya majina ya askari waliohamishiwa au kuondolewa kwenye kikosi hicho.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso amesema ukiona askari anatoka nje ya polisi kulalamika badala ya kufuata utaratibu wa malalamiko uliowekwa kwa mujibu wa sheria ndani ya Jeshi la Polisi, basi ujue ana tatizo binafsi kwani utaratibu wa kuwasilisha malalamiko uko wazi na ufumbuzi umekuwa ukipatikana kwa haraka.

Katika hatua nyingine, baadhi ya askari wamemwomba Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli, kupitia watendaji wake hasa Waziri Kitwanga na IGP Mangu, kuwasaidia kupata haki zao.

Madai makubwa yameelekezwa katika hoja kuwa baadhi ya askari hawalipwi mishahara inayolingana na vyeo vyao, stahiki zao wanazozitolea ‘jasho’ na madai mengine.

Vyanzo vya uhakika vimelidokeza JAMHURI kwamba masuala hayo yanawafanya askari polisi kupunguza morali wa kazi na kuwafanya wachache wenye roho nyepesi kuishi kwa mgongo wa rushwa.

“Tumekuwa tukipunjwa stahiki zetu ambazo tumekuwa tukizitolea jasho; kwa mfano tulikuwa tukichaguliwa kujiunga na kozi ya ngazi ya Diploma ya Polisi Sayansi na ya ngazi ya Cheti ambazo tumemaliza Agosti mwaka huu katika Chuo cha Taalumu cha Polisi Dar es Salaam (DPA), lakini ninavyokwambia tangu tuingie hatukuwahi kupewa pesa za nauli ya kwenda kwenye mazoezi ya vitendo sehemu mbalimbali wala nini.

“Zaidi tuliambiwa tujilipie na baadaye Jeshi litaturejeshea, lakini hadi tunamaliza mafunzo ambayo tuliyaanza mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana hadi Agosti mwaka huu hatukurejeshewa pesa hizo wala hatukupewa nauli kwa ajili ya kurejea katika maeneo yetu ya kazi, huu ni uonevu kwa kweli

“Kila tukidai haki zetu tumekuwa tukitishwa na wakubwa kutii amri yao, lakini hivi sasa kutokana na utawala wa Rais mpya wa awamu ya tano Dk. Magufuli ambaye amekuja na staili ya aina yake tumeamua kufunguka na kumweleza ukweli wa mambo ili aliangalie kwa jicho la pekee jeshi hili,” ameeleza mmoja wa askari walioshiriki mafunzo kutoka mikoani.

Askari hawa wanadai Sh 150,000 kwa kila mmoja. Kozi ya Diploma walikuwa 92, na habari zinazopatikana kutoka vyanzo mbalimbali zinasema fedha hizo zilitolewa ila kitengo cha fedha wanajua jinsi zilivyotumika bila kufika mikononi mwa walengwa.

Pamoja na hilo askari hao ambao wamekuwa wakisoma katika chuo cha DPA wamesema kwamba hata wanafunzi wa ngazi ya cheti ambao waliochukua mafunzo katika chuo cha Polisi Kidatu walikwenda Dar es Salaam kufanya mazoezi kwa vitendo, lakini hawakurejeshewa pesa walizotumia kama nauli na ilifikia hatua walitaka kugoma uongozi wa chuo ukawatisha wakasalimu amri.

Pia kuna tatizo limejitokeza baada ya jeshi kubadili utaratibu wa kuwalipa askari mishahara kupitia benki badala ya kupokea mkononi, ambapo wanawatuhumu watumishi wa idara ya mishara kuwa wanakaa na fedha zao na kuzifanyia matumizi binafsi huku wakidai namba za akaunti za benki za polisi waliostahili kulipwa zimekosewa.

Kwa kufanya hivyo, baadhi ya askari hawajalipwa mishahara hadi miezi minne, na kila wakilalamika wanaambiwa waandike upya namba za akaunti za benki. “Hata hivyo, ukipeleka namba yako, wanapotaka kuiingiza kwenye kompyuta unakuta ni ileile. Tumelalamika kila mahala, hakuna ufumbuzi tatizo linaendelea.

“Kwa mfano mimi binafsi nimeshindwa kulipwa mshahara wa mwezi mmoja na nimeshazunguka sana kuudai hadi Makao Makuu ya Polisi Kitengo cha Mishahara yapata mwaka wa tatu sasa, lakini hadi sasa sijaambulia chochote hivyo nikaamua kukata tamaa,” anasema mmoja wa maaskari hao.

Kwa mujibu wa askari huyo anayefanyia kazi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, tatizo la kutolipwa mishahara lilijitokeza miezi kadhaa tangu askari polisi walipoanza kupitishiwa mishahara yao benki na kwa kiasi kikubwa limewaathiri.

“Miaka ya nyuma tulikuwa tukilipwa posho na mishahara yetu mkononi, lakini miaka kadhaa baadaye ndipo mchezo huo wa kutozikuta pesa zetu benki ulianza kuchezwa na kila tulipodai na hata kufuatilia hadi Makao Makuu Kitengo cha mishahara walitueleza kwamba tatizo hilo lilitokana na kukosewa kwa namba zetu za akaunti ambako mishahara na posho inaingia. Hata tulipopeleka namba zetu kwa mara nyingine hakuna kilichofanyika hadi wengine tuliamua kukata tamaa kufuatilia,” amesema askari mwingine.

Habari zinaeleza kwamba baada ya baadhi ya polisi wanaodai mishahara zaidi ya miezi miwili kuja juu wapo ambao waliingiziwa mshahara wa mwezi mmoja na wengine miezi miwili na kubaki wakidai miezi kadhaa ambayo hadi sasa wameisamehe.

Suala jingine wanalolilalamikia polisi ni kitendo cha baadhi yao wanaopelekwa kusomea vyeo mbalimbali mfano U-koplo na U-Sajenti kutopandishwa mishahara baada ya kuhitimu wakabaki kulipwa mishahara sawa na Konstebo.

“Kwa mfano ninavyokwambia mimi binafsi mwaka juzi nilipelekwa kusomea kozi ya Koplo, lakini hadi leo hii ninavyoongea na wewe sijawahi kuongezwa mshahara unaolinagana na cheo cha Koplo, nalipwa mshahara sana na anaopokea Konstebo, ingawa nimeshapeleka madai yangu kwa uongozi hadi leo hakuna kilichobadilishwa,” anasema askari mwingine.

Askari hao wamemuomba mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwasaidia kupata stahiki zao waweze kufanya kazi kwa moyo mkunjufu.

JAMHURI lilipowasiliana na Sendo kuhusu madai ya mishahara, posho za nauli na kupanda vyeo bila kupandishwa mishahara alisema yuko kwenye kikao na kwamba angelifafanua baadaye.