Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inayo kazi ya ziada kudhibiti uvujaji wa mapato, kwani imebainika kuwa waliokabidhiwa kazi ya kukusanya kodi, wamejipanga kuhujumu mapato ya nchi, uchunguzi wa gazeti JAMHURI kwa mwaka mmoja umebaini.

Imebainika kuwa makontena yanayoleta sintofahamu kuanzia Novemba, mwaka jana pale Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini, mtandao wake ni mpana kuliko ilivyotarajiwa.

“Leo wamemwondoa Kamishna Mkuu wa TRA (Rished Bade) na watendaji wakuu wengine. Wamemwondoa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, lakini uhalisia majipu bado yapo Bandari na TRA. Serikali ina mkono mrefu. Ikachunguze kampuni zilizotoa makontena baadhi zinamilikiwa na wafanyakazi wa TRA.

“Kinyume kabisa na sera ya TRA, kuna mgongano wa maslahi wa wazi. Leo pale Long Room, kuna watu wana matumbo joto. Baadhi ya wafanyakazi wamesajili kampuni za uwakala (clearing and forwarding companies) kwa majina ya mama zao, wake zao, watoto wao, na hizi ndizo zilizotoa makontena. Pa kuanzia Waziri Mkuu aagize kampuni zote za clearing and forwarding zichunguzwe kubaini wamiliki halisi wa hizo kampuni ni akina nani,” anasema mmoja wa wafanyakazi wa TRA.

Uchunguzi unaonesha kuwa baadhi ya wafanyakazi wa TRA wenye utajiri mkubwa, wamepata fedha nyingi kutokana na kumiliki kampuni za uwakala, ambazo baadhi zilishiriki kutoa makontena yaliyopotea bandarini. “Huu ni mchongo tu. Tunakuta watu wanaunganishana kutokea Bandari hadi TRA mizigo yao inapitishwa kwa kasi.

“Hapa wanawasakama wafanyabiashara wachache, kumbe hata wenye kontena moja, mawili nao walikuwa wanakwapua makontena kupitia mtandao usio mtakatifu na kuitia nchi hasara,” anasema mtoa taarifa mwingine.

Uchunguzi wa kina unaonesha kuwa mchezo wa makontena kupotea haujaanza leo. Mwaka 2010 yalipotea makontena yapatayo 460. Ripoti ya Ukaguzi wa Ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ilimtaja Naibu Kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani wa TRA, Generose Bateyunga, kuwa alitumia mamlaka yake kisheria kupitisha makontena ambayo hakujua idadi yake.

Taarifa hiyo ya uchunguzi wa ndani wa TRA iliyoandaliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Tubagile S. Namwenje (nakala tunayo), inaonesha kuwa kati ya Januari 1, 2010 na Mei 13, 2010, Bateyunga kwa kutumia kifungu cha 37 & 38 cha Sheria ya Ushuru ya Afrika Mashariki, aliruhusu Kampuni ya Nyazoro Safety Cargo Limited kuchukua makontena.

Machi 16, 2010 aliidhinisha hati 64 za malipo kuruhusu makontena 64 kutolewa bandarini, ila alipohojiwa na timu ya uchunguzi akasema yeye aliruhusu makontena 72. Hata hivyo, hadi kufikia Aprili 12, wakala kwa kutumia hizo hati 64 aliziingiza kwenye mtandao mara 121 na hivyo kutoa makontena 137. Awamu ya pili, Bateyunga aliidhinisha Aprili 13, 2010 ambapo kwa uchache makontena 259 yalitolewa.

“Uchunguzi wa kina, maelezo binafsi ya DC-CETFP (Naibu Kamishna) na mahojiano, vinaonesha Naibu Kamishna [Bateyunga] hana uhakika ni makontena mangapi/hati za malipo ngapi aliziidhinisha. Orodha iliyopitishwa ya hati za malipo, wakaguzi hawakuzipata, na hazikuingizwa katika ASY-SCAN kurahisisha rejea.

“Orodha pekee iliyopatikana kwa Naibu Kamishna na Meneja wa Kituo cha Forodha ni zile zilizowasilishwa na wakala zikiwa na barua ya maombi. Orodha zote mbili zilikuwa hazijasainiwa au kuwekewa vifupisho vya majina ya Naibu Kamishna, na hazikuwa na mhuri wa TRA ikitoa fursa kwa yeyote mwenye nia ya kubadili viambatanisho kufanya hivyo kwa uhuru,” inasema sehemu ya ripoti ya Namwenje.

JAMHURI lilipowasiliana na Naibu Kamishna Bateyunga alisema: “Mimi ninachofahamu kuhusu hilo, ni kwamba nilikuwa na powers za kuapprove kama ulivyosema, na approval ya provisional inatolewa na kifungu cha 37 na 38 cha Sheria ya East African Community Customs Management Act kama ulivyosema. Naaa sijaapprove za mtu mmoja, nimeapprove za mahospitali, za mashule, na hivyo vilivyokuwa vinakuja mezani kwangu,” amesema.

Bateyunga anasema baada ya hapo aliweka utaratibu wa kukagua mizigo moja kwa moja, kwani mizigo inapopewa idhini ya awali kuondolewa bandarini inakuwa haina vielelezo, hivyo aliweka utaratibu wa kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa mara baada ya kuruhusiwa kutoka bandarini.

“Kwa hiyo walikagua makontena yote, wakaingiza taarifa kuwa kwenye kila kontena wamekuta nini, kodi zilizolipwa ni kiasi gani… sasa ninachotaka kukueleza kaka ni kwamba, hiyo ripoti unayoisoma ndiyo iliyofanyiwa kazi, baada ya kuwa wamezifanyia kazi, ndiyo ikagundulika kwamba mimi nilizoziapprove zilikuwa hazina matatizo. Mimi nina barua kwamba I am cleared from every charge (nimesafishwa kila tuhuma). Baada ya hapo walichunguza na kuona sina tatizo lolote, and I was cleared (nilisafishwa).

“Ukiangalia hiyo ripoti, mwisho wake one of the comments (moja ya maoni) ni kwamba sikuonekana na kosa lolote la kimaadili. Na hiyo ndiyo ninayoweza kusema mbele ya Mungu tunaongea mimi na wewe, siwezi kukosa integrity (uadilifu) kwenye kazi yangu, nimekuwa mwangalifu sana katika utendaji wangu, nimekaa mikoa mingi sana kwa uadilifu mkubwa.

“Nimekuwa Regional Manager Dodoma, nimekuwa Regional Manager Mkoa wa Mwanza, nimeongeza makusanyo, hadi nimekuwa Deputy Commissioner (Naibu Kamishna) wa Trade Facilitation, wa Compliance and Enforcement… nisingeweza kufanya kitu ambacho kiko kinyume na maadili. Kwa hiyo na hiyo ambayo walikuwa wanaandika, ndiyo walikuja kukuta wakati wa uchunguzi, na kimsingi mimi ndiyo niliiyefanya kazi ambayo ni sawa sawa na Serikali inavyotaka.

“Sasa hao wengine unakuta anakwamba assuming (kwa kudhani) hii inakuwa hivi na hivi, ukiishakuwa auditor huwezi kufanya kazi kwa assumption, bali una-audit unapata facts, unabase kwenye facts, huwezi kufanya kazi kwa assumption. Lakini however, bado waliona hakuna element yoyote ya mimi kukosa integrity. Kwa hiyo mimi naomba kama utakuwa fair na kama una Mungu mimi ninayemjua, uliangalie hilo katika totality yake.

“Kwa kweli na mbele ya Mungu, hicho unachokiona hapo siyo chenyewe. Actually, nilikuwa natafutiwa njia tu ya kuondolewa tu pale. Na nilitamkiwa kwamba hapo wewe hapakufai. Hayo hatuwezi kuyaongelea sana, yaache,” amesema Bateyunga.

Anasisitiza kuwa kama angekuwa amepitisha makontena hayo 460 tayari angekuwa ameondolewa katika nafasi hiyo kwani wengi waliokuwa wanamtafuta wangeliyatumia kumwondoa haraka. Kilichomwokoa, kwa maelezo yake ni kutunza kumbukumbu kwani hata ukaguzi ulipofanyika kila kitu kilibainika wazi.

Alipoulizwa taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wa TRA wenye kampuni za kupokea na kusafirisha mizigo bandarini, alisema kama yupo mfanyakazi anayemiliki kampuni ya hivyo ni wazi anatenda kosa la kisheria kwani TRA wanayo sera inayozuia mgongano wa maslahi. “Kwa mfano mimi hapa siwezi nikafungua kampuni ya tax consultancy (ushauri wa kodi). Sasa wewe uko TRA unafungua kampuni ya clearing and forwarding ni kosa,” anasema.

 Uchunguzi wa Gazeti JAMHURI umebaini pia kuwa maeneo ya Ukanda Maalum wa Uzalishaji (EPZ) nalo limekuwa jipu jingine. Wakati wawekezaji kupitia EPZ wanapewa nafuu ya kodi kwa nia ya kuzalisha bidhaa za kuuza nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni, wakubwa hawa wanafanya kinyume chake. Wanazalisha bidhaa kama nguo, mashuka, khanga na nyinginezo kisha wanaziuza hapa nchini.

“Kwa kufanya hivyo wanapata faida kubwa maana bidhaa zao au malighafi wanazotumia zinakuwa hazijalipa kodi na hivyo mwisho wa siku hawa wanapata faida kubwa, Serikali inakosa kodi. Lakini si hilo tu, Serikali inakuwa ikitarajia kupata fedha za kigeni, kwa hawa kuuza nchini bidhaa za EPZ lengo la kupata fedha za kigeni halifikiwi. Serikali sasa ijiridhishe kama wenye leseni za EPZ wanauza bidhaa nje ya nchi,” anasema mtoa habari wetu.

Eneo jingine lililobainika kupoteza mapato makubwa ya Serikali ni utoaji wa risiti. Katika maduka mengi na sehemu za huduma, wafanyabiashara walio wengi ama hawatoi risiti kabisa au wakitoa wanamwandikia mhusika risiti yenye kiasi pungufu na fedha alizotoa.

“Tena wengine hawana aibu kabisa. Wanakwambia hiyo ni ya kutembelea. Unanunua bidhaa za Sh 1,800,000 dukani, ukiingalia risiti vizuri unaona amekuandikia Sh 18,000. Kwa mtindo huu wafanyabiashara wanakwepa mamilioni ya kodi,” alisema mtoa taarifa mwingine.

Katika kudhibiti hilo, wamependekeza Tanzania iige mfano wa Kenya. Kenya ilihamamisha watu kudai risiti kwa kutumia utaratibu wa kusimamisha askari polisi katika milango ya maduka karibu yote jijini Nairobi. “Ilikuwa mtu akitoka dukani hana risiti, askari anamuuliza wapi risiti, ikiwa hana, anamwambia rudi kwa duka upeane risiti,” anasema mmoja wa wananchi kutoka Kenya anayeishi hapa nchini.

Wananchi kwa kuogopa kupambana na polisi, mwisho wa siku walianza kudai risiti kwa nguvu hadi ikazoeleka kuwa kila bidhaa anayonunua mtu ni lazima apewe risiti halali.

Kwa upande wao, madereva walio wengi waliozungumza na JAMHURI wamesema Serikali inapoteza fedha nyingi kwa madereva walio wengi hapa nchini kutokuwa na mikataba. “Fikiria nchi hii ina madereva wasiopungua 200,000. Wote hawa wangekuwa na mikataba na kila mtu akalipa angalau Sh 20,000 kama kodi mwa mwezi, Serikali ingekusanya Sh bilioni 4 kila mwezi,” anasema mmoja wa madereva.

Anasema Serikali inaacha kuwatetea madereva ikidhani wanaumia wao, kumbe nayo ingekuwa imejikita katika kuwatetea wakalipwa vizuri ingepata kodi kubwa kutoka kwao.

Katika eneo la Mbagala, zipo supermarkets mbili ambazo kila mtu akinunua bidhaa wahusika hawataki kutoa risiti. “Ukiwauliza wanasema tatizo lako ni risiti au bidhaa. Sisi tunasema, kama Serikali ikidhibiti vyema, mapato yapo nchi hii. Inaweza kukusanya hata Sh trilioni 4 kwa mwezi,” anasema mkazi wa Mbagala.

Ukiacha ulipaji wa kodi, wananchi walio wengi wanaonekana kuwa na hofu kuonekana wanamtaja mtu au mfanyabiashara fulani kuwa anakwepa kodi kwa hofu ya kuuawa, jambo ambalo walimwambia mwandishi katika maeneo kadhaa kuwa Serikali inapaswa kudhibiti nguvu ya wafanyabiashara kwanza kwani wengi wao wanaonekana kuwa juu ya sheria.

 

Uchunguzi huu umefanywa na Gazeti JAMHURI kwa ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF). Mwandishi wa Habari hii anapatikana kwa Na. 0784 404827.

3240 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!