Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu watano, akiwemo mganga wa kienyeji anayejulikana kwa jina la Saidi Ally ‘Side’ Mzigua (31), kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, huku kichwa chake kikikutwa kikiwa kimefukiwa ardhini katika eneo la Kitunda Kibeberu, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema kuwa Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi wa kisayansi, limefanikiwa kupata sehemu ya kichwa cha marehemu James Temba baada ya kufanya uchunguzi wa kina kufuatia tukio la mwili wake kukutwa ukielea kwenye maji ya Mto Msimbazi kabla ya kuzikwa mkoani Kilimanjaro.
Amesema kichwa hicho kilikutwa katika eneo la Kitunda Kibeberu kikiwa kimefukiwa ardhini, huku taratibu za kisheria zikiendelea kukamilishwa ili watuhumiwa hao wafikishwe katika mamlaka husika za kisheria.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwashukuru wananchi pamoja na mamlaka nyingine za uchunguzi wa kisayansi kwa ushirikiano wao uliofanikisha upatikanaji wa kichwa hicho,” amesema Kamanda Muliro.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha kusambaza taarifa za upotoshaji wakati uchunguzi wa matukio ya kihalifu ukiendelea, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na uhalifu huo.
Jeshi hilo pia limelaani vikali mauaji hayo na kusisitiza kuwa linaendelea kufuatilia jalada la kesi hiyo ili kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua za kisheria na kupata adhabu wanazostahili.


