Serikali ya Kongo imetangaza kuwa idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa Ebola katika eneo la Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo inaendelea kuongezeka na kufikia 204 .

Tangu kuanza kwa mlipuko huo, jumla ya visa 867 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola vimeripotiwa, vikiwemo vifo 204, serikali ilisema. Hiyo ni zaidi ya maambukizi ya watu 100 na zaidi ya vifo 30 ikilinganishwa na siku iliyotangulia.

Hadi sasa maambukizi 91 yamethibitishwa kupitia vipimo vya maabara, ambapo watu 10 wamefariki dunia. Katika nchi jirani ya Uganda, visa vitano vilivyothibitishwa vimeripotiwa kuhusiana na mlipuko huo mashariki mwa Kongo. Hata hivyo Uganda haijatoa takwimu za visa vinavyoshukiwa.

Shirika la Afya Duniani, WHO, linaamini kuwa idadi halisi ya visa vya maambukizi huenda ni kubwa zaidi, kwa sababu mlipuko huo mashariki mwa Kongo haukutambuliwa kwa wiki kadhaa, na si visa vyote vilivyoripotiwa. Idadi kadhaa ya vifo visivyoeleweka katika jamii ilikuwa tayari ikichunguzwa.

Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, lenye makao yake Geneva, lilisema kuwa wahudumu watatu wa kujitolea wa Msalaba Mwekundu wanaaminika kuambukizwa mapema tarehe 27 Machi walipokutana na miili ya watu wanaoamikia kufariki na Ebola katika jimbo la Ituri, Kaskazini mashariki mwa Kongo.