Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi imeendelea kushuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kufuatia kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji madini katika Mgodi wa Namungo unaomilikiwa na kampuni ya Elianje Limited, huku wachimbaji wadogo na wananchi wa maeneo yanayouzunguka mgodi huo wakinufaika kupitia ajira, biashara na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ukuaji wa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo umechangia kuboresha huduma za maji, elimu, afya na miundombinu, hali iliyobadili maisha ya wananchi ambao miaka michache iliyopita walikabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Lindi, Mhandisi Dickson Joram amesema hali ya wachimbaji na wananchi wa Namungo imebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2019 alipowasili katika eneo hilo.

Amesema wakati huo shughuli za uchimbaji zilikuwa katika kiwango cha chini, huku wachimbaji wengi wakitumia njia duni za uzalishaji na kushindwa kumudu mahitaji muhimu ya kila siku.

“Wachimbaji wengi walikuwa wanapitia kipindi kigumu sana. Ulipowatembelea ilibidi wakati mwingine uwaachie fedha za chakula au kuwasaidia mahitaji muhimu. Lakini leo Namungo imebadilika kwa kiasi kikubwa; wananchi wanajitegemea na wanaendesha shughuli kubwa kupitia sekta ya madini,” amesema.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa kampuni ya Elianje Limited, Joseph Shayo amesema kampuni hiyo ilianza shughuli za utafiti na uchimbaji mwaka 2020 na tangu wakati huo imekuwa ikihakikisha jamii inayouzunguka mgodi inanufaika moja kwa moja kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Amesema kampuni imefanikiwa kuchimba visima na kusambaza maji katika Kijiji cha Tongwe na Kitongoji cha Namungo, huku maboresho ya huduma hiyo yakiendelea katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mbali na huduma ya maji, amesema kampuni imejenga shule ya awali, kuboresha madarasa, kujenga vyoo vya kisasa pamoja na kushiriki katika ujenzi wa shule ya msingi katika Kitongoji cha Namungo ili kupunguza adha ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata huduma za elimu.

Shayo amesema mgodi huo pia umechangia uboreshaji wa barabara zinazounganisha vijiji na kata jirani sambamba na kusaidia shule mbalimbali kwa kutoa vifaa vya elimu ikiwemo kompyuta na mashine za uchapishaji.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Chingumbwa, Kata ya Mbekenyela wilayani Ruangwa, Abdallah Manjakali amesema uwepo wa mgodi huo umefungua fursa nyingi za ajira, biashara na huduma za kijamii ambazo hapo awali zilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi.

“Leo wananchi wengi wanapata kipato na maisha yameimarika. Pia kampuni imenunua gari la wagonjwa linalowahudumia wananchi bure wakati wa dharura bila kuchangishwa fedha yoyote,” amesema.

Manjakali ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya mgodi na vijiji vinavyouzunguka unapaswa kuwa mfano kwa wawekezaji wengine wa sekta ya madini, huku akizitaka kampuni zenye leseni ambazo bado hazijaanza uzalishaji kuharakisha uwekezaji ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.